Rufaa ya DPP dhidi ya Sabaya, wenzake kusikilizwa leo

Muktasari:

  • Hukumu anayoipinga DPP ilitolewa Mei 6, 2022 na Jaji Sedekia Kisanya wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma ambaye alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuona kulikuwa na mkanganyiko kwenye mwenendo wa usikilizwaji wa shauri kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Arusha. Mahakama ya Rufani leo Novemba mosi, 2023 imepanga kusikiliza rufaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, (DPP) dhidi ya aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili.

Katika rufaa hiyo Jamhuri inapinga hukumu ya Mei 8, 2022 iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, iliyomuachia huru Sabaya na wenzake Sylvester Nyegu na Daniel Mbura baada ya mahakama hiyo kubaini kulikuwa na upungufu katika mwenendo wa kesi hiyo, ikiwepo hali ya kutofautiana kwa ushahidi.

Rufaa hiyo namba 231/2022 itasikilizwa na jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Jacobs Mwambegele, Ignas Kitusi na Leila Mgonya.

Leo Sabaya ameingia mahakamani hapo akiwa na mke wake ambapo baada ya kuwasili mahakamani hapo majira ya saa tatu kasoro, alipokelewa na baadhi ya ndugu na jamaa waliokuwa wamekusanyika nje ya mahakama hiyo kwa ajili ya kufuatilia kesi hiyo.

Baada ya kuingia mahakamani hapo ambapo kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa saa tatu asubuhi ila mmoja wa majaji hao ameeleza kuwa wanaanza na kesi za madai kisha kesi hiyo itasikilizwa ya mwisho kwa kuwa itasikilizwa muda mrefu.

Awali Sabaya na wenzake walikata rufaa kupinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Oktoba 15, 2021 katika kesi hiyo ya jinai namba 105/2021.

Hukumu anayoipinga DPP ilitolewa Mei 6, 2022 na Jaji Sedekia Kisanya wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma ambaye alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuona kulikuwa na mkanganyiko kwenye mwenendo wa usikilizwaji wa shauri kwenye mahakama ya haki mkazi Arusha.

Alieleza kuwa kulikuwa na  kutofautiana kwa mashahidi na kuufanya ushahidi kuwa batili na Mrufani namba mbili  Nyegu na tatu Mbura hawakupewa haki ya kumhoji shahidi namba mbili wa Jamhuri hivyo kunawanyima haki yao msingi.

Awali Oktoba 15, 2021 Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, aliwahukumu Sabaya na wenzake wawili kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Amworo alisema ameridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi ya Sabaya na wenzake ambapo katika kesi hiyo Jamhuri ilikuwa na mashahidi 11 na vielelezo vinane.

Sabaya alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 4, 2021 baada ya kukamatwa Mei 27 wilayani Kinondoni jijini Dar Es Salaam.

Mara ya mwisho Sabaya kuwa mahakamani ilikuwa Aprili 6, 2023, ambapo aliachiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi,kwa masharti ya kutofanya kosa la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja na kulipa fidia ya Sh 5milioni baada ya kukiri kosa la kula njama na kuzuia utekelezaji wa haki.