Ruto awa mbogo kuhusu kujiuzulu

Muktasari:

Wakati mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga na timu yake wakimtaka William Ruto kujiuzulu unaibu Rais, cheo alichokuwa nacho kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini humo, Ruto ameng’aka kuhusu pendekezo hilo.

Wakati mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga na timu yake wakimtaka William Ruto kujiuzulu unaibu Rais, cheo alichokuwa nacho kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini humo, Ruto ameng’aka kuhusu pendekezo hilo.

Ruto, anayewania urais kwa tiketi ya United Democratic Alliance (UDA) akiungwa mkono na muungano wa vyama vya Kenya Kwanza, akihutubia mkutano wa hadhara juzi (Ijumaa) katika viwanja vya Soko la Buchifi lililopo Jimbo la Mumias alisema hatajiuzulu.

Licha ya Raila, kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Mei Mosi, Rais Uhuru Kenyatta pia alimtaka Ruto kujiuzulu kwa sababu majukumu ya nafasi ya naibu Rais yamemshinda na ameyakimbia.

Mbele ya mamia ya hadhira sokoni hapo, Ruto alisema anatekeleza majukumu yake yote vizuri, hivyo hawezi kujiuzulu na akamtaka Raila aache kumwambia ajiuzulu.

“Nataka niwaombe waonyeshe kazi yoyote ile, ushauri wowote ule au maelekezo yoyote kutoka kwa Rais kuja kwenye ofisi yangu ambayo yalifeli. Nimetimiza kila wajibu ambao Rais alinielekeza au aliuelekeza ofisini kwangu kama ilivyotakiwa,” alisema Ruto.

Aidha, Ruto alimtupia lawama Rais Uhuru Kenyatta kuwa amekuwa akimpaka matope kumfanyia kampeni Raila ambaye ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

“Fisi akitaka kula watoto wake husema wananukia kama mbuzi. Hivyo ndivyo Rais alifanya ili kuniweka kando,” alisema Ruto.

Kingine, Ruto alimtaka Raila ajiuzulu siasa kwa sababu amefilisika mawazo ya kuijenga nchi.

Ruto alirudia kauli yake ya mara kwa mara kuwa mkono wa mapatano kati ya Uhuru na Raila ulisababisha mkwamo wa ajenda kubwa nne ambazo Jubilee walipanga kuzitekeleza kwa Wakenya katika uongozi wao.

Ajenda hizo za Uhuru na Ruto, maarufu kama “Big Four Agenda” ni usalama wa chakula, nyumba za bei rahisi kwa kila raia, huduma sawa za afya, viwanda na ajira.

Ruto alisema mapatano ya Uhuru na Raila chini ya kile kinachoitwa “The Handshake” yamepoteza fedha nyingi za walipakodi.

Akiendelea kushusha lawama, Ruto alimtuhumu Raila kwa kukibomoa chama cha Jubilee na kupoteza miaka mitano ya urais wa Uhuru bila mradi wowote wa maendeleo.

Jubilee ni chama kilichoasisiwa na Uhuru pamoja na Ruto, enzi za upacha imara wa kisiasa. Hata hivyo, Ruto alijiondoa Jubilee na kuanzisha UDA baada ya maelewano yake na Uhuru kwenda mrama.

“Umeshakuwa mtu mzima kiasi cha kutosha kustaafu siasa,” Ruto alimweleza Raila, akisema The Handshake iliwasaidia Wakenya kumfahamu vizuri Kiongozi huyo wa ODM na jinsi alivyo, na asivyojali kuhusu mwananchi wa kawaida.

“Hivi sasa tunajua kuwa vita yake ya uongo kuhusu rushwa ni ya mdomoni tu kwa sababu vibaraka wake walivamia Mamlaka ya Ugavi wa Dawa Kenya na kuiba fedha ambazo zilipaswa kutumika kununua dawa na vifaatiba muhimu kwa ajili ya Wakenya,” alisema Ruto.

Katika mkutano huo, Ruto aliambata na Kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi na yule wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula walioponda takwimu za kukua kwa uchumi zilizotolewa na Serikali Ijumaa iliyopita (Mei 6). Mudavadi alisema hali ya uchumi kwa sasa ni mbaya kulinganisha na ilivyokuwa kabla Jubilee haijaingia madarakani.

“Ni uongo na Serikali inatakiwa kuomba msamaha kwa sababu kila Mkenya anaelewa hali ya uchumi sasa ni mbovu,” alisema.

Ruto aliahidi kuwa akichaguliwa kuwa Rais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, ataongeza kasi ya kuunganisha umeme, kujenga barabara na kuboresha huduma za afya.


Awashambulia magavana

Ruto pia aliwashambulia wabunge na magavana wa Jubilee wanaomuunga mkono Raila kuwa wanakidhalilisha chama hicho.

“Tumeunda Serikali mara mbili, kweli tumekosa mtu wetu wenyewe wa kutuongoza mpaka tumgeukie huyu mzee muongea mafumbo? Hilo ni tusi. Raila hajawahi kuwa na rekodi yoyote ya maendeleo,” alisema Ruto.

Mwenyeji wa mkutano huo alikuwa mbunge wa Thika Mjini, Patrick Wainaina wa Jungle ambaye hivi karibuni alijiunga UDA kisha akatangaza kugombea ugavana wa Kiambu mwaka huu.

Kiambu ni kaunti yenye utajiri wa kura na katika siku za hivi karibuni limekuwa eneo la mapambano kwa kila mgombea urais akitaka kuungwa mkono ili kujikusanyia mtaji wa ushindi.

Ruto pia aliongozana na wabunge, akiwamo Kimani Ichungwah (Kikuyu), Aden Duale (Garrissa Mjini), Ndindi Nyoro (Kiharu) na gavana wa zamani wa Kiambu, Ferdinard Waititu.

Ruto alimshambulia Gavana wa Kiambu aliye madarakani, James Nyoro kuwa amekuwa akifanya makosa kumpokea Raila na kumfanyia kampeni.

Alimweleza Nyoro kuwa watu wa Kiambu wanafahamu ni kiongozi wa aina gani wanamtaka na hawawezi kulazimishwa kumchagua yeyote wasiyemtaka.

“Nataka nimwambie James Nyoro kuwa sisi tuna ubongo, amekuwa akimleta hapa Raila wakati anajua hana rekodi yoyote ya maendeleo,” alisema Ruto.

Hivi karibuni Nyoro alitoboa siri jinsi Raila alivyowaongoza maseneta wa chama cha Orange kupiga kura ya kutokuwa na imani na aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Ferdinard Waititu kabla haijapitishwa na Bunge la Kaunti ya Kiambu kutokana na kashfa ya rushwa.