Ruto, Gachagua kukutana na viongozi waliochaguliwa

Muktasari:

  • Rais mteule wa Kenya, William Ruto na Naibu Naibu Rais mtarajiwa, Rigathi Gachagua kesho Jumatano, Agosti 17 watakutana na viongozi wote waliochanguliwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022 kupitia muungano wa Kenya Kwanza.

Dar es Salaam. Rais mteule wa Kenya, William Ruto na Naibu Naibu Rais mtarajiwa, Rigathi Gachagua kesho Jumatano, Agosti 17 watakutana na viongozi wote waliochanguliwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022 kupitia muungano wa Kenya Kwanza.
Hatua hiyo imekuja siku moja tu, baada Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, Wafula Chebukati kumtangaza Ruto kuwa mshindi wa kiti cha urais
Chebukati alimtangaza mgombea urais kupitia Kenya Kwanza Dk William Ruto kuwa mshindi kwa kupata kura milioni 7.1 (asilimia 50.49) dhidi ya kura milioni 6.9 (asilimia 48.85) alizopata Odinga.
Wagombea wengine kwenye uchaguzi huo ni George Wajackoyah aliyepata kura 61,969 (asilimia 0. 44) na David Waihiga alipata kura 31,987
Taarifa ilitumwa kiwa vyombo vya habari leo, Jumanne Agosti 16, 2022 na Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Veronica Maina imeeleza kuwa Ruto ambaye ni Naibu Rais atakutana na magavana na manaibu, maseneta wabunge na wawakilishi wa wanawake.
“Rais mteule (Ruto) na Naibu wake (Gachagua) anapenda kuyaalika  katika kikao cha kwanza makundi  yafuatayo yaliyochaguliwa kuhudumu useneta, ubunge na ugavana. Kikao hiki kitafanyika kesho katika makazi ya naibu rais saa tatu asubuhi” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Maina, Ruto na Gachagua baadaye watakutana na pia wajumbe wa baraza la madiwani waliochaguliwa chini ya muungano wa Kenya Kwanza.
Wakati Ruto akitarajia kukutana na viongozi hao, mpinzani wake Odinga anatarajia kufungua kesi ya kupinga ushindi huo kwa madai ulitawaliwa na hila chini ya uratibu wa Chebukati.