Ruto, Odinga uso kwa uso warushiana vijembe msibani

Rais wa Kenya, Dk William Ruto (kulia) akisalimiana na kiongozi wa Azimio, Raila Odinga (kushoto) leo Jumamosi Mei 13, 2023 walipokutana katika hafla ya maziko ya Mukami Kimathi katika Kaunti ya Nyandarua nchini Kenya.

Muktasari:

  • Tangu uchaguzi mkuu wa Kenya ulipofanyika Agosti 9, 2022 na William Ruto kuibuka mshindi dhidi ya Raila Odinga, wawili hao wamekuwa wakionyesha kutofautiana majukwaani ambapo Raila anaongoza maandamano nchi nzima kuishinikiza serikali kupunguza gharama za maisha.

Nyandarua. Rais wa Kenya, Dk William Ruto na kiongozi wa Azimio, Raila Odinga wamekutana katika hafla ya maziko ya Mukami Kimathi, mjane wa mpigania uhuru wa Kenya, Dedan Kimathi aliyefariki Mei 5, 2023 akiwa na umri wa miaka 96.

 Wawili hao walipeana mikono huku wakitumia jukwaa hilo kurushiana vijembe kuhusu masuala ya kisiasa yanayoendelea nchini humo ikiwawamo kupanda kwa gharama za maisha na kuongezeka kwa kodi.

Ingawa lilikuwa tukio la muda mfupi, Ruto na Odinga walipeana mikono wakati Waziri Mkuu huyo wa zamani alipoingia katika ukumbi wa ibada ya mazishi kutoa heshima zake za mwisho kwa marehemu Mukami.

Shughuli ya mazishi tayari ilikuwa imeanza wakati Raila alipowasili na kusababisha taharuki alipokuwa akielekea kuketi viti vya mbele ambapo wakati wote watu walikuwa wakimshangilia na kuondoa usikivu ukumbini hapo.

Raila alikuwa wa kwanza kupatiwa nafasi ya kuzungumza kwenye hadhira hiyo ambapo alieleza jinsi alivyomfahamu marehemu Mukami na pia hakusita kurusha vijembe kwa Rais Ruto kuhusu masuala ya kodi na kupaa kwa gharama za chakula.

“Wakenya wanatakiwa kuwaambia ukweli walio madarakani, hakuna kutishwa, hakuna kuogopa, unaogopa nini. Sisi kama wana Azimio si wendawazimu, tunaweza kuelewana.

“Huyu Ruto nimefanya naye kazi kwa muda mrefu sana, yeye ananijua mimi, akipiga kelele huko naangalia tu, najua atapoa.

“Sisi tumetuma watu wetu, naye ametuma watu wake, waongee. Wakielewana sawasawa, lakini nimewaambia ukweli, gharama za maisha zimepanda, ushuru (kodi) imekuwa mingi zaidi...punda amechoka,” amesema Raila.

Akijibu hoja za Raila, Rais Ruto ameeleza kwamba anafahamu ugumu wa maisha, ndiyo maana amepunguza kodi katika maeneo 20. Pia, amesema Serikali yake imepunguza kukopa na mwaka huu ameondoa Sh500 bilioni za Kenya (Sh8.72 trilioni) ambazo wangekopa.

“Ndugu yangu Raila amesema namjua sana, ntapigapiga kelele halafu nitatulia...na mimi pia namjua sana na nimemsoma sana ndiyo maana nilimshinda akiwa na Uhuru.

“Na kwa sababu namjua sana, najua ataendesha hizi mambo za maandamano lakini najua itaishia wapi, najua,” amesema Ruto wakati akizungumza kwenye hafla hiyo ya mazishi.