Ruto anapojifunza maridhiano kwa maandamano

 Rais wa Kenya, William Rutto.

Jumapili, Aprili Pili, 2023, jua la Magharibi, Rais wa Kenya, William Rutto, alitoa hotuba ya kumwomba Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga na timu yake ya Azimio la Umoja One Kenya, kusitisha maandamano.

Wakati Ruto akitoa ombi hilo kwa Raila na Azimio, tayari hali ilishakuwa mbaya. Watu watatu walishapoteza maisha kutokana na maandamano yaliyoitishwa na Raila. Mali za watu ziliharibiwa na kuporwa na waandamanaji bandia. Biashara zilisimama na kuharibiwa.

Nyumba za ibada zilichomwa moto, kuna watu waliteka gari la polisi na kutokomea nalo Oyugis, Homa Bay. Watu zaidi ya 400, waliripotiwa kujeruhiwa, wengine majeraha yakiwa mabaya mno. Tamko lilikuwa maandamano ya amani, ila vitendo havikuakisi amani. Polisi walipotaka kutumia nguvu kudhibiti, machafuko yakawa makubwa. Polisi walikufa na kujeruhiwa.

Ombi la Ruto kwa Raila lilikuwa, maandamano yasitishwe ili kuruhusu mazungumzo ya vyama bungeni katika madai ambayo aliyatoa na kuyatumia kushawishi maandamano nchi nzima, vilevile na yeye (Ruto), milango yake ipo wazi kukutana na kiongozi huyo wa upinzani.

Saa moja baadaye, Raila alijibu hotuba ya Ruto kwa kutoa tamko la kusitisha maandamano ili kuruhusu mazungumzo ya vyama kuchukua nafasi. Vilevile kuheshimu mfungo wa mwezi wa Ramadhan, Kwaresma na ujio wa Pasaka.

Raila alisema, kama mazungumzo hayataleta matunda, watarudi tena kwenye maandamano baada ya wiki moja. Hivyo, aliomba wananchi wasiendelee na maandamano kupisha nafasi ya mazungumzo.

Kiini cha maandamano; Raila alikuwa na hoja mbili. Mosi, ikiwa ni manung’uniko ya kutotendewa haki kwenye Uchaguzi Mkuu Kenya uliofanyika Agosti 9, 2022 na mazingira yake. Pili, ni kupaa kwa gharama za maisha.

Awali, Raila alitoa muda wa siku 14, Ruto kushughulikia malalamiko hayo. Kipindi hicho alichokitoa kilipopita pasipo maombi aliyoyatoa kushughulikiwa, ndipo aliitisha maandamano na yakaitikiwa.

Nyakati za mwanzo za maandamano, ungemwona Ruto akihutubia makundi ya watu, akicheka na kufanya mzaha kuwa Raila amwache arekebishe nchi kwa sababu mapatano yake na Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta, ndiyo yaliyoharibu nchi.

Naibu Rais, Rigathi Kachagua, alikuwa mkali. Alisema, Raila aliitisha maandamano kumtisha Ruto ili waketi na kugawana mamlaka ya kuongoza, kama ilivyokuwa wakati wa Rais wa pili, Daniel Moi, Rais wa tatu, Mwai Kibaki na Uhuru.

Rigathi alisema, Ruto na yeye sio watu wa kutishwa. Aliongeza kuwa Uhuru, mtoto wa Rais wa Kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta, amekuzwa kwa virutubisho vya kiwandani (cerelac), ndio maana alipotishwa na Raila, aliketi wakazungumza.

Si hivyo tu, Rigathi aliahidi kuwa hata siku ambayo Ruto angekubali kukutana na Raila, yeye (Rigathi), angekwenda Ikulu ya Kenya na kuzuia mageti yote, kuhakikisha kiongozi huyo wa upinzani, hapati nafasi ya kupeana mkono na bosi wake.

Kinachotokea sasa, ni tofauti mno na mtazamo wa Ruto na tambo za Rigathi. Dirisha la mazungumzo limefunguliwa. Muhimu zaidi, aliyeomba ni Ruto. Kisha Raila akapokea. Rigathi akampongeza bosi wake kwa uamuzi wake wa busara.

Ruto alipotoa hotuba yake, alisema kuwa alifanya mazungumzo na viongozi wengi wa dini. Kauli kama hiyo pia aliitoa Raila. Na hotuba zao zilitpofautiana saa moja tu. Hiyo ikupe picha kuna mchakato nyuma ya pazia ulishaanza. Ruto na Raila walipojitokeza, ilikuwa utekelezaji wa makubaliano, ndio maana matamko hayakutofautiana.

Mwisho wa hotuba yake, Ruto aliulizwa kuhusu gharama za maisha kwa sababu wananchi wengi waliandamana kwa msukumo wa bidhaa kupanda bei. Alijibu kuwa mipango ya kupata ufumbuzi wa kudumu inaendelea kutekelezwa, ila hata sasa bei imeshuka, kutoka Shilingi ya Kenya 230 (Sh4,600), bei ya unga hadi Sh180 (Sh3,600).

Raila naye, mwisho wa tamko lake, aliulizwa kuhusu hoja zao kwenye mazungumzo kama zitazingatia gharama za maisha, akajibu kuwa hilo ni moja ya agenda yao muhimu. Kwamba hawatakubali maelezo tofauti zaidi ya serikali kuweka ruzuku ili bei za bidhaa zipungue kama alivyofanya Uhuru kabla hajatoka madarakani.


Kutoka Uhuru hadi Ruto

Tamko la Ruto kumwomba Raila kusitisha maandamano, bila shaka, Uhuru alilitazama kwenye televisheni, akiwa nyumbani kwake, Caledonian House, Barabara ya Dennis Pritt, Nairobi. Nina uhakika, lilimfanya achanue tabasamu la ushindi.

Uhuru alionekana mkosefu mbele ya Ruto, alipofanya mapatano na Raila Machi 2018, katika tukio ambalo vyombo vya habari Kenya vililiita “The Handshake”. Ruto alisema, kupatana baina ya Uhuru na Raila, kulididimiza uchumi wa nchi. Hata matokeo ya kupanda kwa gharama za maisha, huelekeza lawama kwa Uhuru na Raila.

Ruto alikuwa Naibu wa Uhuru. Alitofautiana na bosi wake kwa kila mpango wake wa maridhiano. Aliwaamisha Wakenya kwamba kama si Uhuru na Raila kupatana na ‘kushikana mikono’, maisha yangekuwa mazuri na changamoto za kupanda kwa bei za bidhaa zisingekuwepo.

Uhuru alisema, aliamua kufungua mlango wa maridhiano na Raila kwa sababu hali ya kisiasa baada ya Uchaguzi Mkuu Kenya 2017 ilikuwa mbaya. Kuna maeneo ya nchi, watu hawakumtambua Uhuru kama rais, isipokuwa Raila.

Utetezi wa Uhuru siku zote ni kwamba baada ya kupatana na Raila, ilikuwa rahisi kuongoza nchi na kukubalika kuliko kabla. Daima aliamini kuwa nchi ikiwa tulivu, ndipo kiongozi aliye madarakani, anaweza kufanya kazi vema.

Sasa, Uhuru akiwa Caledonian House, akiishi na kufanya kazi zake za ustaafu kwenye ofisi ya nyumbani kwake, anamwona Ruto akikiri hali ya nchi ni mbaya, hivyo anaitisha mazungumzo. Ni kipindi hiki, Ruto anatamka kuwa uchumi wa Kenya upo hatarini na mambo hayawezi kwenda bila maandamano kusitishwa.

Bila shaka, Ruto hatamki, lakini moyoni anakiri kuwa Uhuru alipoamua kumeza kiburi chake cha mamlaka ya urais na kuomba mazungumzo na Raila, hakuwa mjinga. Kupambana na mwanasiasa ambaye ana nguvu za kuigawa nchi pande mbili, inahitaji kumheshimu.

Uhuru, alitaka kuondoka madarakani akiacha nchi ambayo mifumo yake ya uchaguzi na siasa inakuwa salama kwa vizazi vingi vijavyo. Dhamira hiyo ipo ndani ya Mpoango wa Kujenga Daraja la Maridhiano (Building Bridges Initiative ‘BBI’), ambao Ruto aliupinga.

Machi 2018, baada ya Uhuru na Raila kufanya maridhiano, kiliundwa kikosi kazi cha wajumbe 14, kikapewa agenda tisa. Kikazunguka majimbo (counties) 47 ya Kenya kukusanya maoni ya Wakenya kuhusu hatima ya nchi yao.

Agenda tisa ni mosi, jinsi ya kumaliza mgawanyiko wa kikabila. Pili, ushirikishwaji wa vyama vya upinzani katika muundo wa Serikali, tatu, jinsi ya kutatua misuguano ya uchaguzi, nne, ulinzi na usalama, tano, namna ya kupambana na rushwa.

Sita, kushughulikia ukosefu wa moyo wa utaifa kwa wananchi, saba, haki na uwajibikaji, nane, mgawanyo sawa wa matunda ya nchi na tisa ni kutanua nguvu ya mamlaka kwa wananchi na uwakilishi.

Ni agenda hizo zilisababisha kikosi kazi cha BBI kije na mapendekezo ya mabadiliko ya vifungu vya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, vipo vinapendekezwa kufutwa, vingine kubadilishwa matamshi na vipo vinaongezwa.

Ruto na washirika wake walipinga lakini sasa wanajua umuhimu wake