Saa tatu ‘Producer’ wa Ditto akitoa ushahidi mahakamani

Lameck Ditto (mwenye kofia) akiingia kwenye moja ya chemba za Mahakama Kuu, kanda ya Dar es Salaam kusikiliza kesi yake ya madai dhidi ya DSTV.
Muktasari:
- Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Ditto ameishtaki Multchoice Tanzania Limited akiilalamikia kukiuka hakimiliki na kutumia wimbo anaodai kuwa wake kwenye kampeni ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 bila ridhaa yake.
Dar es Salaam. Mzalishaji wa muziki Emmanuel Maungu, aliyetengeneza wimbo wa Nchi Yangu wa msanii wa muziki wa Bongo fleva, Lameck Dotto Bernard Bwakeya maarufu kama Ditto, ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jinsi alivyotengeneza wimbo huo.
Maungu ametoa maelezo hayo leo Machi 21, 2024 mahakamani hapo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya madai iliyofunguliwa na Ditto dhidi ya Kampuni ya Multchoice Tanzania Limited (DSTV), huku akitumia saa tatu kutoa ushahidi huo.
Ditto ameishtaki kampuni hiyo akiilalamikia kukiuka hakimiliki, kwa kutumia wimbo wake kwenye matangazo ya biashara kipindi cha kampeni ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 bila ridhaa yake.
Hivyo, ameiomba Mahakama iiamuru Multchoice imlipe fidia ya Sh6 bilioni na pia imlipe Sh200 milioni kama fidia ya madhara ya jumla na riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua shauri hilo.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Dare es Salaam, Salma Maghimbi imeendelea leo Alhamisi, Machi 21, 2024 kwa Maungu kutoa ushahidi wake akiwa ni shahidi pili kati ya mashahidi watano wanaotarajiwa kuitwa katika kesi hiyo upande wa madai.
Katika ushahidi wake akiongozwa na wakili wa Ditto, Ally Hamza; Maungu ameieleza Mahakama hiyo kuwa aliutengeza wimbo huo katika mfumo wa sauti mwaka 2017.
Ameeleza kuwa mwaka 2019, alipigiwa simu na Ditto akamuuliza endapo yeye (Maungu) ndiye alitoa idhini kwa DSTV kuutumia kwenye matangazo yao, yeye akamjibu kuwa hajawahi kutoa idhini hiyo kwa kampuni hiyo, ndipo Ditto akamtumia viunganishi kuona DSTV walivyoutumia kwenye matangazo hayo.
Maungu ameeleza kuwa alianza kutengeneza wimbo wa Nchi Yangu, ambao awali uliimbwa na Ditto pekee, kisha akaurudia (remix) huku Ditto akiwa amewashirikisha wasanii wengine baadhi baada ya Ditto kuombwa uchanganywe kwa ajili ya Tamasha la Urithi.
Baada ya kutoa ushahidi wake, alihojiwa maswali kadhaa ya dodoso na Wakili wa DSTV, Thomas Mathias. Sehemu ya mahojiano hayo baina ya shahidi huyo na wakili wa Mathias ilikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Nikisema kwamba wewe ndiye uliyeingiza beat (midundo) kwenye wimbo wa Nchi Yangu niko sahihi?
Shahidi: Niliingiza sauti.
Wakili: Unafahamu masuala ya haki miliki?
Shahidi: Nazijua za kwangu kama producer.
Wakili: Tutajie haki kadhaa kama producer.
Shahidi: Ni kuwa na umiliki sehemu ya muziki nilioingiza.
Wakili: Unataka kuiambia Mahakama katika wimbo wa Nchi Yangu una haki?
Shahidi: Hayo ni makubaliano yangu na Ditto.
Wakili: Ditto aliiambia Mahakama kuwa hakuwahi kuwalipa wasanii wote walioimba kwenye huo wimbo ni sahihi?
Shahidi: Ndio.
Wakili: Kwa kuwa hakukulipa, zile haki bado ziko kwako?
Shahidi: Hayo ni makubaliano yangu na Ditto.
Wakili: Unaiambia Mahakama hii kuwa mlishindwa kuendelea na production kwa sababu Mult Choice kuutumia huo wimbo? Unafahamu kama ulikuwa published (ulichapwa) na Clouds Media Group mwaka 2018?
Shahidi: Ndio.
Wakili: Soma hii email (barua pepe) ni ya lini, ilitoka kwa nani na inakwenda kwa nani? (akimpa nyaraka)
Shahidi: Sio yangu ukisema niitambue!
Wakili: Nimesema usome.
Shahidi: Imetoka kwa Emmilian Mallya kwenda kwa Ditto, ni forwarded message (meseji iliyotumwa), ilitoka kwa Ruge Mutahaba Agosti 27, 2018.
Wakili: Soma content (maudhui).
Shahidi anasoma, baada ya kumaliza kusoma wakili anaendelea kumuuliza:
Wakili: Umesema ulikuwa published mwaka 2018 na All Stars, ni sahihi?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Nikisema kabla sehemu ya wimbo huo haujatumika na DSTV tayari ulishakuwa published muda mrefu ni sahihi?
Shahidi: Ndio.
Shahidi: Ushahidi wa kwamba mlishindwa kuendelea na albamu sio kweli?
Shahidi: Ni kweli tulishindwa kuendelea.
Wakili: Mheshimiwa (Jaji), naomba kama nitapata Youtube Channel ya Clouds.
Kutokana na ombi hilo, wakili Ditto, Hamza amesema kuwa links zipo kwenye flashi. Hivyo kwa idhini ya Mahakama flashi hiyo imeunganishwa kwenye runinga, ikafunguliwa na kuoneshwa maudhui yaliyomo, baada ya kumaliza kuiangalia, wakili wa Multchoice akaendela na maswali.
Wakili: Katika tasnia ya muziki unaweza kukubaliana na mimi unaweza kuwa mtunzi lakini sio mmiliki?
Shahidi: Inawezekana.
Wakili: Pia, inaweza kuandika lakini sio kumiliki?
Shahidi: Inategemea kama umeuza haki miliki.
Wakili: Usiseme inategemea, sema inawezekana au haiwezekani.
Shahidi: Inawezekana
Wakili: Kwa tafsiri rahisi unaweza kuwa mwandishi, lakini sio mmiliki?
Shahidi: Inategemea kama uliuza, ulikubaliana na mmiliki kama uliuza hiyo haki miliki.
Wakili: Katika hizi media unafahamu kama huwezi ku-publish content (kutangaza/ kuchapisha maudhui) kama huna haki miliki?
Shahidi: Hilo sijui, lakini kwa mujibu wa email wimbo uliombwa kutumika (akirudi kusoma email)
Wakili: Kwenye hiyo e-mail kuna sehemu uliombwa?
Shahidi: Hii e-mail hakuomba, ila Ruge alimuomba Ditto utumike kwenye Urithi Festival, lakini kwenye e-mail Ruge alikuwa akitoa maelekezo huko kwa watu wake.
Wakili: Ditto hakuleta hayo makubaliano, wewe umeyaleta hapa mahakamani?
Shahidi: Hayo ni yeye (Ditto) na Ruge, alipokuja kwangu kuuomba nilimuuliza mmekubaliana akasema ndiyo, hivyo sijui walikubaliana kwa namna gani?
Wakili: Asante mheshimiwa, tunaomba tufungulie akaunti ya Ditto ya Youtube, (baada ya akaunti kufunguliwa, akaendelea).
Wakili: Ionyeshe Mahakama wimbo wa Nchi Yangu wa All Stars kwenye akaunti ya Ditto.
Shahidi: Hapo haupo.
Wakili: Nitakuwa niko sahihi kwamba ulisema wimbo huu una version (toleo) mbili?
Shahidi: Ndio.
Wakili: Ni upi ulitumika na Dstv?
Shahidi: Nchi yangu version ya pili ulitumika
Wakili: Hiyo iliimbwa na nani?
Shahidi: Uliimbwa na Ditto kwa kushirikiana na wasanii wengine.
Wakili: Unaweza kuwataja?
Shahidi: Ndio ila siwezi wote, sababu ni muda mrefu, lakini ni Joel Lwanga, J Melody, Jux, Nandy, Lameck Ditto mwenyewe, Kundi la Weusi na Vijana wengine walikuwa wanatoka chuo sio rahisi kuwakumbuka.
Wakili: Je kule Cosota (Chama Hakimiliki) ni wimbo upi ulisajiliwa.
Shahidi: Nchi Yangu.
Wakili: Version ipi?
Shahidi: Hakuna version, mfano Tanzania umeimbwa na watu wa ngapi? Mwenye original version (toleo halisi) ndiye ameandika.
Wakili: Jibu swali.
Shahidi: Wimbo wa Nchi Yangu ndio ulioandikishwa Cosota.
Wakili: Mheshimiwa nitaomba sasa ile Version anayomiliki Ditto (ikawekwa).
Wakili: Inasema Lameck Ditto-Nchi Yangu Official Audio. Naomba niambie ilikuwa published lini?
Shahidi: Januari 10, 2019.
Wakili: Bado unaendelea kushikilia, wimbo huu wakati unakwenda kusajiliwa haukuwa kwenye domain media?
Shahidi: Haikuwa na mantiki yeye (Ditto) kukaa nao wakati tayari ninyi mmeshautumia.
Wakili: Nitakuwa niko sahihi nikisema huo wimbo ilibidi usitoke kwa kuwa DSTV walikwishautumia ni kweli?
Shahidi: Sahihi.
Wakili: Unakubaliana na mimi wimbo uliotumika sio uliosajiliwa na Cosota?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Unavyodhani ni wimbo upi ulitumiwa na DSTV.
Shahidi: Nchi yangu.
Wakili: Version ipi?
Shahidi: Ya pili
Wakili: Unakubaliana huu wimbo ambao ni wa Nchi Yangu All Stars haupo kwenye machapisho ya Ditto?
Shahidi: Hizo ni chaneli zake mwenyewe Ditto siwezi kujua, zingekuwa zangu ningejua.
Wakili: Ulijuaje kama ulirushwa DSTV?
Shahidi: Ditto alinipigia simu kuniuliza kama nimetoa idhini, sababu tulikubaliana usitoke bila idhini yake.
Wakili: Utakubaliana na mimi, aliyekuwa anasambaza wimbo huu ni marehemu Ruge Mutahaba?
Shahidi: Sikubaliani na wewe.
Kesi hiyo itaendelea tena kesho Ijumaa, Machi 22 Mahakama Kuu, Ditto akiwakilishwa na mawakili wawili, Elizabeth Mlemeta na Ally Hamza.