Sababu Jacob Zuma kwenda jela miezi 15
Muktasari:
- Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amehukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani kwa kosa la kuidharau Mahakama baada ya kutofika kwenye mahojiano ya uchunguzi wa tuhuma za ufisadi zinazomkabili mapema mwaka huu.
Afrika Kusini. Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amehukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani kwa kosa la kuidharau Mahakama baada ya kutofika kwenye mahojiano ya uchunguzi wa tuhuma za ufisadi zinazomkabili mapema mwaka huu.
Zuma (79) ambaye alikuwa Rais kwa karibu miaka tisa hadi 2018, hakuwepo kusikiliza Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini ikitoa uamuzi na hukumu dhidi yake. Jaji aliamuru Rais huyo wa zamani ajisalimishe mwenyewe ndani ya siku tano.
Zuma alishindwa kuhudhuria kwenye uchunguzi wa ufisadi ulioongozwa na Naibu Jaji Mkuu, Raymond Zondo Februari. Uchunguzi huo unafuatilia madai ya ufisadi wa kiwango cha juu uliofanyika wakati Zuma akiwa madarakani. Mwanasiasa huyo mkongwe amekana makosa na amedai Zondo ana chuki binafsi.
Jana, Jaji Sisi Khampepe alisema: “Mahakama ya Katiba haiwezi kufanya chochote isipokuwa kuhitimisha kwamba Zuma ana hatia ya uhalifu wa kuidharau Mahakama.”
Aliongeza: “Aina hii ya utabiri na uasi ni kinyume cha sheria na utaadhibiwa. Sina chaguo lingine ila kumtia Zuma kifungoni na matumaini kwamba kufanya hivyo kunapeleka ujumbe bila shaka...utawala wa sheria na usimamizi wa haki vipo.
“Hukumu ya wengi inaamuru adhabu isiyosimamishwa ya kifungo kwa miezi 15,” alisema Khampepe kama alivyonukuliwa na gazeti la The Guardian.
Uchunguzi wa ufisadi ulianzishwa na Zuma mwenyewe kutokana na kuongezeka kwa shinikizo la wananchi kwenye kashfa hiyo, muda mfupi kabla ya kuondolewa madarakani mwaka 2018 na chama tawala cha African National Congress (ANC).
Hata hivyo, alitoa ushahidi mara moja tu, Julai 2019, kabla ya kupuuzia mialiko kadhaa ya kujitokeza tena, huku akitoa sababu za matibabu na maandalizi ya jaribio lingine la ufisadi.
Mara ya pili, alijisalimisha kwa muda mfupi Novemba, lakini aliondoka kabla ya kuhojiwa.
Februari, Zondo alisema atatafuta amri ya Mahakama ya Katiba kwamba Zuma alikuwa akiidharau korti na atasisitiza kifungo cha gerezani.
“Hii ni mbaya kwa sababu ikiruhusiwa kuendelea, kutakuwa na uvunjifu wa sheria na machafuko katika Mahakama. Kunaweza kuwa na watu wengine ambao wataamua kufuata mfano wake wakati wanapewa wito katika michakato mingine ya Mahakama,” alisema Zondo.
Sehemu kubwa ya ufisadi unaodaiwa kuchunguzwa na Tume unawahusu ndugu watatu kutoka kwa familia tajiri ya wafanyabiashara wa India, Gupta, ambao walishinda kandarasi yenye fedha nyingi za Serikali na inadaiwa walikuwa na uwezo wa kuchagua mawaziri katika Baraza la Mawaziri la Rais Zuma.