Sababu mashine za kukusanyia mapato kuzimwa
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Deogratius Ndejembi akijibu swali la msingi la Mbunge wa Meatu (CCM), Leah Komanya ambaye ameuliza mashine ngapi za kukusanyia mapato zilibainika kutokuwa hewani na hazikutambuliwa na halmashauri kwa mwaka 2018-2021leo Jumanne Mei 16, 2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo
Muktasari:
- Katika kipindi cha 2020/21 jumla ya mashine 1,355 katika halmashauri 46 hazikuwa hewani, bunge limeelezwa leo Mei 16,2023.
Dodoma. Katika kipindi cha 2020/21 jumla ya mashine 1,355 katika halmashauri 46 hazikuwa hewani, bunge limeelezwa leo Mei 16,2023 huku ikitaja sababu ya kuzimwa ikiwa ni baadhi ya watendaji kutokuwa waaminifu.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Deogratius Ndejembi amesema kuwa kwa sasa ofisi ya Rais Tamisemi imefanya maboresho ambapo matumizi ya mashine za kukusanyia mapato kupitia mfumo wa LGRCIS yatakoma ifikapo Juni 30,2023.
Naibu Waziri ametoa majibu hayo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Meatu (CCM), Leah Komanya ambaye ameuliza mashine ngapi za kukusanyia mapato zilibainika kutokuwa hewani na hazikutambuliwa na halmashauri kwa mwaka 2028/19,2019/20 na 2020/21.
Naibu Waziri amesema kuanzia Julai Mosi, 2023 hakutakuwa na PoS zinatakazokuwa Offline zaidi ya masaa 24 kuwepo na taarifa kwani mfumo umewekwa vizuri sasa.
Kuhusu miaka ya 2018/19 alisema kulikuwa na mashine 14 za kukusanyia mapato (PoS) katika halmashauri 2 wakati mwaka 2019/20 kulikuwa na PoS 1,469 katika halmashauri 54 hivyo kusababisha mapato mengi ya Serikali kupotea.
Kuhusu nini chanzo cha kuzima kwa mashine hizo, amesema imekuwa ikitokana na baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu kupelekea hasara kwa serikali lakini wamekuwa wakiwashughulikia.
Hata hivyo Serikali haikutangaza hasara ya kiasi gani cha fedha kilichopotea kutokana na kuzimwa kwa mashine hizo.