Sababu ongezeko wagonjwa wa vifua, mafua
Muktasari:
- Wizara ya Afya imetaja sababu ya ongezeko la wagonjwa wanaougua vifua na mafua kuwa ni uwepo wa virusi wapya wa mafua na influenza, wanaotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema kuna ongezeko la virusi wanaosababisha homa kali ya mafua inayoambukiza maarufu influenza, waliyotaja kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Homa hiyo ambayo husababisha ugonjwa wa vifua inaongezeka katika baadhi ya maeneo nchini, huku wataalamu wa afya wakitoa angalizo kuacha kutumia kiholela antibaotiki na badala yake wakiwashauri wagonjwa kuhudhuria vituo vya afya na kunywa maji mengi.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne, Oktoba 1, 2024, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu amesema magonjwa ya vifua huongezeka na kupungua kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Amesema ikiangaliwa mwenendo wa mwaka jana na mwaka huu hakuna tofauti, lakini mara nyingi ni maambukizi ya virusi na wamekuwa wakifuatilia Uviko19 kote nchini kupitia maeneo ya ufuatiliaji zaidi ya 20 nchi nzima, kupitia sampuli za wagonjwa wanafika vituo vya afya kwa matatizo ya vifua.
“Ikiwa mgonjwa ana changamoto za homa na kifua labda kukohoa sanasana maabara hatuoni Uviko19 ni wachache sana na pengine wiki nzima tusipate mgonjwa kama wiki iliyopita.
“Lakini kuna virusi tofauti, kwa mfano tumegundua virusi wa mafua na influenza na virusi wengine tofauti tofauti na hii inaendana na mabadiliko ya hali ya hewa, lakini hakuna tofauti ukiangalia mwaka jana na mwaka huu katika magonjwa kama haya,” amesema Profesa Nagu.
Madaktari watoa angalizo
Wakati changamoto hizo zikiwakumba watoto na watu wazima, wataalamu wa afya wameshauri ni vyema tiba ikazingatia ushauri wa daktari na si vinginevyo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji, Elisha Osati amesema mara nyingi magonjwa hayo virusi wake husambaa kulingana na hali ya mazingira kutoka kwenye baridi kwenda hali ya joto ambapo wadudu pia hubadilika.
“Wanapobadilika husumbua mwili ni mabadiliko ya hali ya hewa, influenza hii hutokea hali inavyobadilika mfano tumetoka kwenye baridi tunaenda kwenye joto, wadudu wanaathiri njia ya hewa wanaweza kusababisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Dk Osati ambaye pia ni Mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya amesema ni vema kupima afya kabla ya kufanya maamuzi ya kununua dawa na kumeza.
“Wengi wanaenda kwenye famasi wanakunywa antibiotiki kwa ugonjwa usiohitaji nguvu hiyo ya dawa matokeo yake ugonjwa unazidi, tunashauri ni mpaka aende apimwe na mtaalamu wa afya apewe dawa inayohusika ili kuzuia usugu wa dawa.
“Virusi hivi husababisha maambukizi kwenye njia ya hewa, tunashauri mara nyingi unywe maji ya kutosha, inasaidia na dawa za kikohozi na hutakiwi kutumia antibiotiki,” amesema Dk Osati.
Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji Hospitali ya Aga Khan, Alex Masao amesema virusi hao huleta kero na homa kwa wagonjwa lakini hawana madhara makubwa.
“Bahati nzuri virusi hawaendi kwenye mapafu, huu ni msimu wa mafua ni vyema mgonjwa kumsikiliza mtaalamu wa afya amshauri nini cha kufanya.
“Kunywa dawa bila kumuona mtaalamu siyo sawa, tunatumia antibaotiki holela, ukipata mafua ukiitumia haisaidii mpaka pale utakapopona. Watu wajifunze, siyo kila unachoumwa unakimbilia kutumia antibiotiki unatengeneza usugu,” amesema Dk Masao.