Sababu panga pangua na maagizo ya Rais kwa wakuu wa mikoa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

 Rais Samia Suluhu Hassan ametaja sababu za kuwapo mabadiliko ya mara kwa mara ndani ya Serikali, huku akitoa maelekezo kwa kila mkuu wa mkoa aliyemteua


Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema mabadiliko ya viongozi yanayofanyika yanatokana na tathimini ya utendaji wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi).

Amesema Tamisemi imekuwa ikifanya tathimini hiyo kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala na pale kunapoonekana kuna shida hatua huchukuliwa.

Mbali na kufanyika kwa tathimini hiyo pia ametoa maelekezo ya kiutendaji kwa kila mkuu mpya wa mkoa aliyemchagua.

Ametoa kauli hiyo katika hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali wakiwamo wakuu wa mikoa walioteuliwa siku chache nyuma iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo Machi 13, 2024.

Samia amesema wakati mwingine mtu hafanyi vizuri kwa kuwa ndivyo alivyo na wakati mwingine ni mazingira yaliyopo katika eneo husika, mambo ambayo kwa pamoja huzingatiwa.

Amesema kupitia tathimini hiyo imemfanya Paul Chacha kuonekana amefanya vizuri ndiyo maana amepandishwa kuwa mkuu wa mkoa kutoka kuwa mkuu wa Wilaya ya Kaliua.

“Mkoa wa Tabora huna ugeni nao, ulikuwa mkuu wa Wilaya ya Kaliua na unakwenda kuongoza mkoa mzima, nenda kasimame vyema, Tabora ni wazalishaji wazuri wa mazao ya kilimo ndiyo maana miradi mingi ya kilimo ilipelekwa huko,” amesema Rais Samia.

Amemtaka mkuu huyo wa mkoa kusimamia mazao ya tumbaku na pamba huku akiitaja tumbaku kuwa na chagamoto ya mazingira kufuatia ukataji miti kwa ajili ya kukaushia tumbaku.

Amesema Serikali ilianza jitihada kwa kushirikiana na kampuni zinazonunua tumbaku ili kupeleka teknolojia mpya ya kukausha zao hilo.

“Anzia hapo, fuatilia teknolojia isimame ipunguze kukata miti, zao la pamba kalisimamie wakulima wanufaike na jasho lao,” amesema Rais Samia.

Pia, amemtaka Chacha kwenda kuongeza uzalishaji wa asali na kuweka viwanda vidogo mkoani humo ili wananchi wapate ajira.

 Kuhusu miradi ya kilimo amesema upo wa umwagiliaji eneo la Inara Tabora unaolenga kutatua changamoto ya upungufu wa chakula alimuagiza kuusimamia ili utekelezwe ipasavyo.

“Kuna migogoro kidogo kidogo katika mradi wa Inara, nenda kazisome, atakayekukabidhi atakuambia, kaa kitako kavisome, sikiliza pande zote na migogoro itatuliwe ili mradi ufanye kazi na tuboreshe uzalishaji wa mazao yatakayozalishwa pale,” amesema Rais Samia.

Pia, amesema lipo shamba la uzalishaji mbegu mkoani humo ambalo pia amemuagiza mkuu huyo mpya wa mkoa kwenda kulisimamia ili kupata matokeo kusudiwa.

Rais Samia amesema Luteni Kanali Patrick Sawala amepandishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kutokana na kazi nzuri aliyofanya alipokuwa mkuu wa wilaya.

Kutokana na Mkoa wa Mtwara kupakana na Msumbiji alimtaka kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama na kamati ya ujirani mwema kufanya vikao na kukubaliana kuondoa changamoto hasa za mpakani.

Amesema mkoa huo pia ni muhimu kiuchumi kutokana na  korosho, hivyo alimtaka kusimamia jitihada za Serikali kuongeza uzalishaji wa korosho kwa kuwa aliyeondoka amefanya vizuri licha ya kuwapo changamoto ndogo ndogo.

“Mbali na uongezwaji wa thamani wa zao la korosho, tumeamua korosho yote isafirishwe kutoka Bandari ya Mtwara, tumejaribu msimu uliopita na mpaka leo hatujapata lawama kutoka duniani kuwa korosho iliyopelekwa ni chafu,” amesema Rais Samia.

Amesema korosho inaporuhusiwa kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam mambo mengi yamekuwa yakifanyika katikati lakini ikisafirishwa moja kwa moja zao lenye sifa limekuwa likipelekwa.

Pia, amesema Serikali imeanzisha kongani ya viwanda vya kubangua korosho mkoani Mtwara  huku akimtaka mkuu huyo wa mkoa kusimamia vyema ili vijana wapate kazi.

Katika mazao ya mbaazi na ufuta, Rais Samia amesema Serikali imepata soko lake India na mwaka jana bei ilikuwa nzuri huku akieleza kuwa bei hiyo inaweza kufanya watu wengi kuzalisha zaidi.

Alimtaka mkuu huyo mpya wa mkoa, wakati wa ununuzi wa ufuta na mbaazi,  asimamie vizuri kwa kuwa Serikali imeamua mazao hayo yaingie ghalani licha ya kuwa yanauzwa kwa nchi moja lakini ina wanunuzi tofauti ambao lazima washindane Watanzania wapate bei kubwa.

 “Pia, Mtwara kuna fursa za kitalii ambazo bado hazijatumika unaweza kwenda kuwa na timu za kitaalamu kuangalia fursa zilizopo, kuziibua na kufanyiwa kazi, zamani Mtwara na Lindi ilikuwa inaitwa mikoa ya pembezoni, mikoa masikini lakini ni mikoa yenye rasilimali kubwa hivyo nenda kasimamie,” amesema Samia.

Mkoa wa Songwe

Samia amesema wamempeka Daniel Chongolo mkoani Songwe kwa sababu anaijua vizuri tangu akiwa ndani ya chama.

Amesema anaimani kuwa amempatia mkoa anaoufahamu na atausimamia vizuri.

Rais Samia amesema mkoa huo unaunganisha Tanzania na Zambia kupitia Tunduma huku akieleza kuwa eneo hilo mambo mengi ya kiuchumi yanatokea ikiwamo uhalifu mwingi wa kiuchumi ukwepaji kodi na ubadilishaji fedha usio halali.

 “Una mkurugenzi mzuri kidogo, ameweza kuongeza mapato, nenda kasaidiane naye, mfanye kazi vizuri pale Tunduma panaweza kuendesha mkoa na mkachangia vizuri serikalini,” amesema.

Shinyanga

Annamringi Macha ambaye amepewa kuungoza Mkoa wa Shinyanga, Rais Samia amesema miongoni mwa sababu za yeye kupewa cheo hicho ni uzoefu alionao katika uongozi na kukua kwake.

Samia alimtaka Macha kuongeza uzalishaji pamba, kupandisha hali za wananchi kujiletea maendeleo kwa kuwa kumekuwa na hali ya watu kulala na kufatilia kwa karibu Kongani ya Buzwagi inayotarajia kuanzishwa huku akimtaka kuisimamia kwa karibu ili ufanikiwe.