Panga pangua ya Rais Samia yapita, yampa Chongolo mkoa
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan ameteua wakuu wa mikoa mitatu na kuhamisha wengine wanne vituo
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameteua wakuu wa mikoa watatu akiwamo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, huku akiwahamisha makatibu tawala vituo vyao vya kazi.
Katika mabadiliko yaliyotangazwa leo Machi 9, 2024 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk Mosess Kusiluka, Rais Samia pia ameteua na kuhamisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa wilaya na mkurugenzi mkuu wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart).
Katika uteuzi huo, Chongolo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe akichukua nafasi ya Dk Francis Michael ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Chongolo aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM tangu Aprili 21 2021 alijiuzulu nafasi hiyo Novemba 30, 2023 na nafasi yake kuchukuliwa na Balozi Emmanuel Nchimbi.
Wakuu wengine wa mikoa wapya ni Luteni Kanali Patrick Sawala aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paul Chacha anakwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Rais Samia pia amewahamisha wakuu wa mikoa wanne katika vituo vyao akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed aliyehamishiwa Mkoa wa Ruvuma.
Pia, Halima Dendego aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa amehamishiwa Singida akibadilishana na Peter Serukamba aliyehamishiwa Iringa huku aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Batilda Burian akihamishiwa Tanga.
Naye aliyeuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Udart, akichukua nafasi ya Gilliard Ngewe atakayepangiwa kazi nyingine.
Pia, Rais Samia amewahamisha vituo vya kazi makatibu tawala saba akiwamo Msalika Makungu kutoka Mkoa wa Mara kwenda Rukwa, Gerald Kusaya kutoka Rukwa kwenda Mkoa wa Mara.
Makatibu tawala wengine wa mikoa ni Albert Msovela kutoka Kigoma kwenda Katavi na Hassan Rugwa kutoka Katavi kwenda Kigoma.
Wengine ni Rehema Madenge kutoka Dar es Salaam kwenda Ruvuma na aliyekuwa Katibu Tawala Ruvuma, Stephen Ndaki amehamishiwa Mkoa wa Kagera huku Toba Nguvila akitolewa Kagera na kuhamishiwa Dar es Salaam.
Katika ngazi ya wakuu wa wilaya, Rais Samia ameteuwa watano akiwamo Abdallah Nyundo (Kilwa), Festo Kiswaga (Monduli), Kanali Evans Mtambi (Mkinga), Almishi Hazali (Hanang) na Joachim Nyingo (Kilolo).
Pia, wakuu wa wilaya 25 wamehamishwa vituo, akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Godwin Gondwe, alihamishiwa Wilaya ya Singida, huku aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Joshua Nassari akihamishiwa Magu mkoani Mwanza.
Wengine ni Deusdedith Katwale aliyehamishwa kutoka Chato kwenda Wilaya ya Tabora, Janeth Mayanja kutoka Hanang' kwenda Chamwino, Johari Samizi akihamishwa kutoka Wilaya ya Shinyanga kwenda Misungwi, Hassan Bomboko kutoka Wilaya ya Ukerewe kwenda Ubungo.
Wengine ni Christopher Ngubiagai aliyehamishwa kutoka Wilaya ya Kilwa kwenda Ukerewe, Veronica Kessy kutoka Iringa kwenda Wilaya ya Mbulu, Kheri James amehamishwa kutoka Wilaya ya Mbulu kwenda Iringa, Paskasi Muragili akihamishwa kutoka Wilaya ya Singida kwenda Bukombe, Said Nkumba akitoka Bukombe kwenda Wilaya ya Chato.
Wengine ni Simon Chacha akitoka Wilaya ya Sikonge kwenda Tunduru, Hashim Komba kutoka Ubungo kwenda Geita, Cornel Lucas Magembe aliyehamishwa kutoka Geita kwenda Sikonge.
Wengine ni Peres Magiri kutoka Wilaya ya Kilolo kwenda Nyasa, Kisare Makori kutoka Moshi kwenda Mbinga, Zephania Sumaye kutoka Mafia kwenda Moshi na Luteni Kanali Michael Mtenjele kutoka Wilaya ya Tarime kwenda Tandahimba.
Kanali Maulid Surumbu amehamishwa kutoka Wilaya ya Mkinga kwenda Tarime, Zainab Issa akitoka Pangani kwenda Muheza na Faidha Salim akitoka Wilaya Itilima kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Busega.
Pia, Anna Gidarya amehamishwa kutoka ukuu wa Wilaya ya Busega kwenda Itilima na Gift Isaya Msuya kutoka Chamwino kwenda Bahi.
Wakurugenzi wa Halmashauri
Kwa upande wa wakurugenzi wa Halmashauri, Rais ametua wakurugenzi 10 akiwamo Dk Rogers Shemwelekwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Masud Kibetu Halmashauri ya Manispaa ya Kahama na Dk Amon Mkoga Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Wengine ni George Mbilinyi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Murtallah Mbillu Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Ummy Wayayu Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Wengine ni Dk Vumilia Simbeye Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Jamal Abdul Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Mashaka Mfaume Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na Fred Millanzi Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.
Kwa waliohamishwa ni Nassoro Shemzigwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwenda Longido na Said Majaliwa kutoka Halmashauri ya Jiji la Tanga kwenda Halmashauri ya Mji wa Kondoa.
Paul Sweya ametoka Halmashauri ya Mji wa Kondoa kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Stephen Katemba kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Naye Semistatus Mashimba ametoka Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Kasulu na Josephat Rwiza amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwenda Mbinga.
Juma Juma kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwenda Mji wa Bunda, Emmanuel John Mkongo kutoka Halmashauri ya Mji wa Bunda kwenda Manispaa ya Morogoro.
Wengine ni Stephano Kaliwa aliyehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kwenda Nsimbo, Mohamed Ntandu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwenda Magu.
Fidelica Myovella ametoka Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwenda Mji wa Mafinga na Ayubu Juma Kambi ametoka Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwenda Itigi.