Kihongosi wa UVCCM arudi kwenye mkeka wa Ma-DC

Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Kenan Kihongosi

Muktasari:

  • Rais Samia afanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa, amng’oa kigogo wa UVCCM na kumteua kuwa mkuu wa wilaya Urambo

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Kenan Kihongosi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo akichukua nafasi ya Said Mtanda aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Uteuzi wa Kihongosi ambaye alikuwa Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umefanyika ikiwa ni sehemu ya mabadiliko madogo ya baadhi ya Wakuu wa Mikoa yaliofanywa jioni ya leo na Rais Samia.

Kwa mara nyingine Kihongosi anarudi kwenye orodha ya wakuu wa wilaya akiwa alishawahi kuhudumu kama Mkuu wa Wilaya ya Arusha wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu wa UVCCM.

Katika mabadiliko hayo Mtanda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara akichukua nafasi ya Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, imesema aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Cuthbert Sendiga amehamishiwa Mkoa wa Manyara.

Sendiga ni kama amebadilishana na Makongoro Nyerere ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara na sasa katika mabadiliko haya, amehamishiwa mkoa wa Rukwa.