Rais Samia afanya uteuzi, yumo aliyewahi kuwa DC Hai

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa mabalozi wanane akiwemo aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa mabalozi nane wakiwamo maofisa wawili kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

 Pia, yumo Gelasius Byakanwa aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro na mkuu wa mkoa wa Mtwara. Kabla ya uteuzi huo Byakanwa aliwahi kuwa ofisa mkuu wa ubalozi Tanzania Korea Kusini.

Taarifa iliyotolewa leo Mei 22, 2023 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus imesema uteuzi huo ulianza Mei 10, 2023. Walioteuliwa ni pamoja na Meja Jenerali Ramson Mwaisaka, kabla ya uteuzi huo alikuwa mkuu kamandi ya Jeshi la Wanamaji.


Wengine ni Meja Jenerali Paul Simuli aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Jeshini, pia yumo Mohamed Awesu ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Konseli Mkuu, Konseli ya Jeddah Saudi Arabia.

Rais Samia amewateua Dk Mohamed Juma Abdallah, kabla ya uteuzi huo alikuwa katibu tawala wa mkoa wa Kaskazini Unguja. Pia ameteuliwa Hassan Mwamweta ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Ofisa mwandamizi wa Mambo ya Nje na Mkuu wa Utawala Ubalozi wa Tanzania, Uturuki.

Mbali na hao mkuu huyo wa nchi, amewateua Iman Njalikai ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Ofisa wa Mambo ya Nje Mkuu na Msaidizi wa Waziri Mkuu Hotuba.Pia yumo Khamis Mussa Omar ambaye alikuwa kaimu Mwakilishi wa Kudumu, Ubalozi wa Tanzania Ufaransa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, mabalozi hao wataapishwa kwa tarehe itakayopangwa baadaye.