Sababu shule binafsi kutoza ada kubwa

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Tamngosco, Aman Lyimo amesema ikiwa kodi zitapungua ada zitashuka kwa kiasi kikubwa.

Dar es Salaam. Wawekezaji katika sekta ya elimu wamesema uwepo wa kodi zaidi ya 20 wanazotozwa imekuwa mzigo kwao na chanzo cha kuweka ugumu katika uendeshaji wa huduma ya elimu wanayotoa.

 Pia, uwepo wa sera ya elimu bure umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia shule kukosa wanafunzi.

  Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika elimu (Tapie), Mahmoud Mringo katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika hivi karibuni.

Mringo amesema changamoto hizo zimegawanyika katika makundi manne makubwa la kwanza ni mtaji mkubwa unaohitajika wakati mtu anahitaji kuanzisha shule.

Amesema ili mtu apate kibali cha kuendesha shule anatakiwa kuwa na madarasa karibu saba ya kuanzia, maabara na bweni.

“Hii ni sawa na nyumba 20 hadi 30 ikiwa mtu akiamua kujenga, unatoa wapi hela ya kujenga nyumba zote hizi. Tatizo lingine lilipo ni unapohitaji mkopo utaweka rehani shule na viwanja vyote vilivyopo. Ukipewa mkopo pia, gharama yake ni kubwa kuliko hela uliyokopa karibu mara mbili na zaidi,” amesema Mringo. 

Pia, amesema jambo hilo linawaumiza watu wengi huku likichangia kuwafanya kutumia muda mwingi kulipa riba za taasisi za kifedha na kushindwa kukuza maendeleo katika huduma wanazotoa.

Akitolea mfano amesema alikopa Sh500 milioni lakini alipokuja kulipa ndani ya miaka saba  ilikuwa Sh1.2 bilioni gharama ambayo ni ngumu kuchochea ukuaji wa huduma.

Hilo linachangiwa pia na kukosekana kwa mtu anayelipia gharama, inafanya wao kuendesha shughuli zao katika hali ya ugumu tofauti na shule na vyuo vya Serikali ambavyo vinapata fedha kutoka serikalini. 

Amesema hali hiyo imefanya hadi sasa shule zaidi ya 300 kuwa sokoni kutokana na kushindwa kujiendesha kwa miaka tofauti huku nyingine zikibaki magofu, zikifungwa kwa miaka miwili, mitatu na zaidi.

“Ziko sokoni naweza kukutembeza kukuambia chukua hii chukua hii lakini hazipati wateja kwa sababu gharama iliyowekezwa huwezi rudishiwa hata asilimia 30,” amesema Mringo.

Kuhusu kodi amesema zipo zaidi ya 25 na uwepo wake umekuwa ukibeba takribani asilimia 15 ya gharama za uendeshaji wa shule husika huku akieleza fedha hiyo hiyo inapatikana katika kila ada anayolipa mwanafunzi. 

“Huku ndiyo usiseme, atakuja Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) anataka kodi, Wakala wa Usalama mahala pa Kazi (Osha) atakuja, halmashauri watataka, kodi ya ardhi, viwanja vya michezo ambavyo wanafunzi wanachezea mpira nitatakiwa nikilipie na hapa kiwanja cha 70 kwa 70 ni sawa na viwanja 12 vya Sinza vyote nivilipie kodi ya ardhi,” amesema Mringo.

Pia, amesema utaratibu wa ulipiaji wa viwanja hugusa viwanja vyote vya michezo huku Serikali ikienda mbali zaidi kwa kutaka hata maeneo ambayo bado hayajajengwa ndani ya shule hizo kulipiwa.

“Ukichanganya hizi zote unapata karibu asilimia 15 ya gharama za mwanafunzi anazolipia, ukijumlisha na kukosekana kwa mitaji hivyo ulikopa unatakiwa kulipa riba inakuwa kama Sh400,000 hivyo unakuta mwanafunzi anasoma kwa karibu Sh600,000, katika Sh1 milioni aliyolipa bado huduma nyingine hujatoa hapo,” amesema.

Akiwawakilisha wengine, anataka kulegezwa kwa masharti ikiwamo lile linalowalazimisha kujengwa kwa madarasa mengi ya mbele ikiwa tu ndiyo anaanza kutoa huduma.

“Mimi naanza darasa la kwanza unanilazimisha nijenge hadi darasa la saba la nini, nikifanya mwaka mmoja nikashindwa, au nikitaka kujenga shule unanilazimisha kuwa na eneo la heka 2.5 la nini Dar es Salaam hii, kwa nini usiwekee eneo naloweza kujenga shule ya ghorofa na masomo yakaenda,” amesema Mringo. 

Amesema sababu hizo zimefanya wawekezaji kutoka nje kuikimbia sekta ya elimu na kuita eneo hilo kama pasua kichwa.

Alipokuwa akichangia maoni katika jukwaa la kodi na uwekezaji wiki iliyopita, Katibu wa Chama cha Walimu wa Shule Binafsi Tanzania ((Tamongosco), Julius Mabula ametaka kodi zinazotozwa katika shule kuangaliwa upya ili kuweka ahueni kwa wawekezaji.

Mabula amesema mmoja wa meneja wa shule alimuorodhoshea kodi na tozo 20 za haraka wanazolipishwa jambo ambalo halina afya kwa wawekezaji.

“Leo hii shule inalipishwa kodi 20, Serikali imekazingira kashule kamoja, sheria za kodi zinawakandamiza wawekezaji wa ndani, mtu mwenye wivu namba moja ni sheria za kodi, shule nyingi zinakufa na hakuna anayehoji ukifa unaachwa, tunapoteza fursa za ajira nyingi,” amesema Mabula.

Akizitaja kodi hizo amesema ni leseni ya biashara, kodi ya huduma, zimamoto, mchango wa juma la elimu, kodi ya Pango la ardhi, ada ya ukaguzi wa magari ya wanafunzi, tozo ya Upimwaji wa wafanyakazi/wanafunzi (Afya), kodi ya majengo.

Nyingine ni kodi ya mabango ya shule, mchango wa utamaduni, kodi ya mazingira (NEMC), leseni ya kusafirisha wanafunzi inayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela fees), kodi ya kmapuni (Corporate tax), kodi ya zuio (withholding tax), income tax na uwepo wa mashine ya risiti za kielektroniki (EFD) kwenye shule.

 Ada ya ukaguzi wa shule (udhibiti ubora wa shule), ada ya mitihani ya Taifa kwa wanafunzi na mchango wa Mwenge.

Mmoja wa wamiliki wa shule, Yuston Ntungi amesema kuendelea kuwapo kwa utitiri wa kodi kwa shule zimekuwa zikiathiri utoaji wa huduma na elimu kwa jumla.

"Kuna changamoto, katika kodi, kuna utitiri ambao kiuhalisia unambana mmiliki wa shule ambaye ni mtoa huduma na si mfanyabiashara, hali hii inaathiri utoaji wa huduma na kuathiri ubora wa elimu, hivyo ni bora Serikali ikaangalia namna ya kuondoa kodi nyingine," amesema Ntungi.

Ntungi amesema baadhi ya kodi hulipwa kulingana na viwango vya halmashauri katika eneo shule inapotolea huduma.

“Lakini kodi nyingine zinajulikana kwa kuwa zimepangwa, kama leseni ya biashara gharama yake ni kati ya Sh300,000 hadi Sh1 milioni, kitu kama ada ya mitihani ni Sh10,000 kwa wanafunzi wa darasa la saba na kidato cha nne na sita ni Sh50,000, Serikali ilipoamua kufuta ada ya mitihani kwa nini watoto wa shule binafsi waliachwa,” amesema Ntungi.

Kodi nyingine ni majengo ambayo mtu hulipa kutokana  na aina ya miundombinu aliyonayo; kwa mujibu wa kanuni kila jengo lina kiwango chake.

Kwa mfano kwa upande wa halmashauri ya wilaya hutoza Sh90,000 kwa mwaka kwa nyumba ya ghorofa bila kujali idadi ya sakafu zilizopo.

 

Ada bei juu

Wakati wao wakilia na kodi, baadhi ya wazazi wamelia na ada kubwa zinazotozwa na shule hizo.

 Clementina Malcus, mkazi wa Mtoni Kijichi alipokuwa akizungumza na Mwananchi amesema ada zinazotozwa na baadhi ya shule zimekuwa kikwazo wanapotaka kuwasomesha watoto wao katika shule za mchepuo wa Kiingereza. 

Mfano mimi mwanangu, shule anayosoma si ile ya chaguo lake, shule aliyokuwa anaitaka kipato changu hakiwezi kumudu kulipa ada, ilibidi tuzungumze na kuahidi kumpeleka shule atakayohitaji akifika kidato cha kwanza kwa matokeo tutakayokubaliana,” amesema Clementina.

Mzazi mwingine, Leah Mtonga amesema hata kama wakipewa mwanya wa kulipa kidogo kidogo bado wanakuwa katika wakati mgumu kwa sababu baadhi ya shule ada zake ni kubwa hata inapogawiwa mara nne.

 “Kuna mtu asiyetaka kumpeleka mwanaye shule nzuri basi, kipato tu hakituruhusu na huenda hizo shule ni kwa ajili ya watu wa ngazi fulani ya maisha,” amesema Leah.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Tamngosco, Aman Lyimo amesema ikiwa kodi zitapungua ada zitashuka kwa kiasi kikubwa.

“Unakuta mmiliki mmoja wa shule anaambiwa alipe Sh100 milioni kwa mwaka kama kodi, TRA wakiona umekusanya ada nyingi wanadhani umepata hela nyingi ukiangalia kila ada ina matumizi yake, inunue mafuta ya kuzungusha wanafunzi mwaka mzima, vyakula, mahitaji ya shule yote yanayohitajika inaumiza,” amesema Lyimo.


Elimu Bure

 Mbali na kodi, pia kuanzishwa kwa sera ya elimu bila ada imetajwa kuwa moja ya sababu iliyochangia shule hizo kukosa wanafunzi na baadhi kufungwa.

Hiyo ni kutokokana na wazazi wengi kuacha kulipia hata kidogo walichokuwa wakitoa na kuwapeleka watoto wao katika shule za umma.

“Bado watu wapo kwenye kiwewe, ukiangalia matokeo ya ufaulu daraja la nne na sifuri ni nyingi, bado matokeo yake bado hayajaonekana vizuri kwa sababu zamani watu walikuwa wakifeli serikalini wanakimbilia shule za binafsi lakini sasa watu wakifeli bodaboda wanaongezeka, hakuna mtu anataka kusafisha cheti,” amesema Mringo ambaye ni mwenyekiti wa wawekezaji binafsi.

Amesema neno bure lilipokewa kwa namna tofauti na wananchi huku akieleza Serikali ilikuwa haijajipanga kuhakikisha inasimamia ubora unaotakiwa katika elimu.

Akizungumzia suala la kodi, Naibu waziri wa Fedha, Hamad Chande amesema huu ni wakati sahihi kwao kuandika maoni ya kile wanachotamani kifanyiwe marekebisho na kukiwakilisha serikalini.

Amesema katika kutambua mchango na umuhimu wao, Serikali iliandaa jukwaa la kodi na uwekezaji lililojumuisha watu kutoka sekta tofauti lililonga kusikiliza maoni yao ili yafanyiwe kazi.

“Wiki iliyopita tulikuwa na jukwaa la kodi na uwekezaji, watu walitoa maoni yao, hivyo hawajachelewa haya wao wanaweza kuandika na kuyawasilisha katika kamati ya bajeti au kwa katibu mkuu wizara ya fedha,” amesema Chande.

Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alipoulizwa juu ya suala hilo aliomba Waziri wa Elimu atafutwe.

 “Nipo mkutanoni nje ya nchi, kwa suala hili nashauri uwasiliane na mheshimiwa Waziri wa Elimu,” alijibu Profesa Kitila.

Alipotafutwa Naibu Waziri wa Elimu, Juma Kipanga amesema: “Wizara ya Elimu haikusanyi kodi. Sekta binafsi siyo mshindano wa Serikali katika kutoa huduma ya elimu, Serikali inashirikiana na wadau wote katika elimu.”