Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gharama za maisha zapaisha ada shule binafsi muhula mpya

Muktasari:

Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza mwaka mpya wa masomo kwa shule za msingi na sekondari nchini, wazazi wameanza kuhisi maumivu kutokana na kupanda kwa ada na gharama nyingine kwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi.


Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza mwaka mpya wa masomo kwa shule za msingi na sekondari nchini, wazazi wameanza kuhisi maumivu kutokana na kupanda kwa ada na gharama nyingine kwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi.

Jana Mwananchi lilipata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazazi ambao shule wanazosoma watoto wao ada imepandishwa kwa muhula utakaoanza Januari hivyo kutakiwa kujiandaa.

Mmoja wa wazazi hao (jina limehifadhiwa) alisema amepokea mabadiliko yaliyomshtua ya ada pamoja na gharama za sare kwani zimepanda bila wazazi kushirikishwa.

“Wiki iliyopita nilipewa taarifa ya mabadiliko ya ada kutokana na gharama za uendeshaji, pamoja na yote hakuna anayepinga hilo. Changamoto ni kwamba wazazi hatujashirikishwa, tumeletewa tu taarifa. Miaka ya nyuma tulikuwa tunalipa Sh2.2 milioni lakini sasa tunatakiwa kulipa zaidi ya Sh2.64 milioni. Pia, wanataka kubadilisha sare tuwe tunalipa Sh200,000 badala ya Sh100,000 ya sasa,” alisema.

Kuhusu sare ambazo alikuwa akilipia Sh130,000 kuanzia Januari zimepanda mpaka Sh200,000 mabadiliko ambayo aliyatafsiri kuwa “ni maumivu maumivu kwetu wazazi.”

Wakati mzazi huyo akilalamikia kutopewa taarifa, mzazi mwingine alikuwa na barua kabisa inayoonyesha kupata kwa gharama za shule kuanzia Januari inayosomeka “rejea mkutano wa wazazi uliofanyika Oktoba 15 ambapo uongozi wa shule uliwataarifu wazazi kuhusu ongezeko la ada litakaloanza mwaka 2023. Sababu ya ongezeko hilo ni kupanda kwa gharama za uendeshaji wa shule.”

Hata hivyo, mzazi mwingine aliimbia Mwananchi gharama za mtoto wake anayesoma shule ya awali zimepanda.

Mzazi huyo alisema kuanzia mwakani ameambiwa ada imepanda na atatakiwa kulipa Sh1.14 milioni kutoka Sh900,000 aliyolipa mwaka huu.

“Sikwenda kwenye mkutano wa wazazi, mambo yalikuwa mengi. Inawezekana walikubaliana huko. Siwezi kupinga makubaliano ya wengi, nitalipa hiyo ada japo itatoboa zaidi mfuko wangu,” alisema.

Wakati wazazi wakilia kuhusu ongezeko hilo la gharama za shule, Kamishna wa Elimu Tanzania, Dk Lyabwene Mtahabwa alisema Serikali haina mamlaka ya kuingilia kwani ni makubaliano kati ya mzazi na shule.

“Bodi ya shule inashirikiana na wazazi wenye watoto kuakubaliana, Serikali kwa sasa haina sauti kuamua kushusha bei, hatuna mamlaka hayo, ni kama ilivyo mfumo wa hospitali binafsi ndivyo ulivyo mfumo wa elimu.”

“Mzazi akiipenda shule wanakubaliana anapewa fomu ya mwanaye kujiunga, mwenye shule akiona maisha yamebadilika anaita kikao cha bodi ya shule wanakubaliana kazi inaendelea mbele,” alisema.

Dk Mtahabwa alisema, kama kuna shule inajiamlia mambo yake bila kufuata utaratibu vikiwamo vikao vya bodi ndio Serikali huwachukulia hatua.

Sheria ya Elimu iliyorekebishwa mwaka 2002 inasema uendeshaji wa shule unasimamiwa na kamati au bodi ya shule.

Mei 2016, aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansina Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisitisha mjadala wa ada elekezi kwa shule binafsi.

Akizungumzia kupanda kwa gharama hizo, mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tomongsco), Benjamin Nkonya alisema utaratibu wa kupandisha ada unazingatia sera ya elimu.

“Inategemea makubaliano kati ya mazazi na uongozi wa shule. Unakuta wazazi wanataka watoto wapande gari lenye kiyoyozi, aina ya chakula, mtaala wanaofundishiwa kama ni wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (Necta) au Cambidge hivyo kuna sababu nyingi za kupandisha ada,” alisema.

Kwa sasa alisema ada zitapanda kutokana na mabadiliko ya gharama za huduma mbalimbali nchini akigusia bei za nafaka, mafuta na walimu kuhitaji nyongeza ya mishahara.

“Wazazi wawe wavumilivu na wajali zaidi ubora wa elimu tunaoutoa ambao tumeelekezwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu,” alisema Nkonya.