Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu za Profesa Kabudi, Lukuvi kuteuliwa tena

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria (Kushoto) na William Lukuvi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge na Uratibu (Kulia) kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam Agosti 15, 2024.

Muktasari:

  • Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Palamagamba Kabudi (Kilosa) na William Lukuvi wa Isman wamerejeshwa tena katika Baraza la Mawaziri. Wadau wamewachambua na kueleza sababu zilizofanya warejeshwe.

Dar es Salaam. Ilionekana kama vile Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anampigia chapuo mbunge wa Kilosa (CCM), Profesa Palagamba Kabudi, achaguliwe tena na wananchi wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa mwakani kwa kauli yake mbele ya wananchi jimboni humo Agosti 2, 2024.

Aliwaambia wananchi hao: “Endeleeni kuniletea Kabudi.” Kabla ya kauli hiyo, akiwa Dumila mkoani Morogoro, aliwaeleza wananchi wa eneo hilo wamchagulie viongozi wazuri wanaotokana na CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba, 2024.

Hata alipozindua daraja la Berege wilayani Kilosa akiwa katika ziara ya siku sita mkoani Morogoro, alimnadi Profesa Kabudi akimsifu kwa utendaji wake akisema amekuwa akimtumia hata serikalini.

“Ndugu zangu, tunapozungumza wabunge Kilosa mmepata mbunge. Mbunge huyu si kwenu tu hata mimi namtumia kwenye mambo mengi. Nikikwamakwama huko nauliza jamani Kabudi yupo, nikiambiwa yupo nasema hebu muingizeni kamati hiyo anichapie kazi. Kwa hiyo nawashukuru sana wana-Kilosa endeleeni kuniletea Kabudi asanteni sana,” alisema.

Kauli hizi ni kama zilikuwa zikiwaandaa wananchi jimboni Kilosa kwa kile Rais Samia alichokifanya usiku wa Agosti 14, 2024 kwa kumteua Profesa Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, nafasi aliyowahi kuhudumu mwaka 2017-2019.

Novemba 13, 2020, Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli alimteua Profesa Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, nafasi aliyoitumikia katika Baraza la Mawaziri kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika 2020.

Awali, pamoja na William Lukuvi, aliyeteuliwa tena kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), nafasi aliyowahi kuhudumu, kwa pamoja waliachwa katika baraza jipya la mawaziri la Rais Samia lililotangazwa Januari 8, 2022.


‘Kaka zangu wawili’

Rais Samia Januari 10, 2022 akiwaapisha viongozi wateule, alieleza wawili hao watapangiwa kazi maalumu. Lukuvi wakati akichwa alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Nina kaka zangu wawili, William Lukuvi na Palamagamba Kabudi ukiwatazama hao umri wao ni kama wangu na niliowateua hamfanani kabisa, kwa hiyo kaka zangu hawa nimewavuta waje kwangu ili waje wanisimamie kuwasimamia ninyi kwa hiyo kuwaacha kwangu kwenye ile orodha hapo wote ni wadogo na mnahitaji kusimamiwa vizuri.

“Kaka yangu Kabudi amefanya kazi nzuri sana kusimamia mazungumzo ya Serikali na mashirika na ndiyo kazi ninayotaka nimkabidhi sasa kindakindaki aendelee na kazi hiyo, ila kazi yake kwa sababu haipo kwenye muundo haitangazwi, mashirika yote kazi zote zitakazoingia ubia na Serikali yeye ataongoza hiyo timu kwa hiyo yeye ni baba mikataba,” alisema Rais Samia.

“Kaka yangu Lukuvi yeye ana kazi na mimi mtaisikia baadaye lakini ninamvuta Ikulu kazi yetu ni kuwasimamia nyie, kwa sababu nikiwatazama hapo wote wanakaribia kustaafu bado miaka miwili, wengine mna safari ndefu mimi na wale tulishastaafu kwa hiyo kazi yetu sasa ni kushika kiboko kuwasimamia nyie na makatibu wakuu.”

“Nimeona meseji nyingi wengine wanasema afadhali Lukuvi katoka, hajatoka yupo, wengine wameanza kumletea meseji za ajabu wakijua atagombania uspika, hatagombania ana kazi na mimi msianze kumchafua ametumikia Taifa hili kwa uadilifu kwa muda mrefu muacheni aende na mimi tumalizie kazi atakayopangiwa,” alisema Rais Samia.


Kwa nini Lukuvi, Kabudi

Profesa wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bakari Mohamed amesema Rais Samia amewarudisha Profesa Kabudi na Lukuvi kwenye Baraza la Mawaziri, kwa lengo la kujipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Amesema awali aliwaondoa kutokana na upepo ulivyokuwa ukienda na asingeweza kuwamudu kwa wakati huo.

“Wakati kiongozi anaingia madarakani kwanza anakuwa anajiweka sawa, hivyo anatafuta watu ambao atakuwa anawamudu ili aonyeshe kwanza uongozi wake. Sasa wakati ule Profesa Kabudi na Lukuvi walikuwa ni mawaziri waandamizi na wenye ushawishi mkubwa.”

“Pia wakati ule wa mtangulizi wake, hayati John Magufuli, kuna urithi aliokuwa ameuacha na wale walikuwa ni mawaziri waandamizi waliokuwa karibu naye na kulikuwa na malalamiko mengi katika utawala huo, hivyo alitaka ajitenge na lawama ili ajenge kwanza utawala wake,” amesema Profesa Mohamed.

Amesema kwa sasa Rais Samia amewarejesha kwa kuwa ameshajiweka sawa na anajiandaa kwa chaguzi zijazo, hivyo hao ndio wanaomfaa kwa sasa.

“Ni maandalizi ya uchaguzi tu. Kwa Profesa Kabudi kwanza amemweka Wizara ya Katiba na Sheria kwa sababu ni mtaalamu wa sheria na pia anaweza kukabiliana na madai ya mabadiliko ya Katiba. Pia mawaziri hao wawili ni wataalamu wa propaganda hivyo wanaweza kukabiliana na mikikimikiki ya uchaguzi wakati huu,” amesema.

Kuhusu Lukuvi, amesema ni mwanasiasa mkongwe na amewahi kuitumikia wizara aliyopangiwa kwa sasa: “Ana uzoefu katika wizara hiyo na anaweza kulidhibiti Bunge na uratibu wa sera.”

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Deus Kibamba, amesema Profesa Kabudi na Lukuvi hawakuwa wameondolewa serikalini, kwani tangu awali Rais Samia alisema watabaki kuwa washauri wake.

“Aliposema watabaki kuwa washauri wake maana yake hao hadhi yao ni sawa na mawaziri, yaani ni wazee wa kumshauri Rais,” amesema.

Kibamba amesema wamerejeshwa kutokana na mambo kutokwenda kama alivyotarajia.

“Ukiona Rais anafanya mabadiliko haya ujue kuna mahali pameyumba, yaani mambo hayaendi sawa. Profesa Kabudi na Lukuvi walikuwa ni wachezaji wa akiba, sasa ukiona mchezaji wa akiba ameingia uwanjani maana yake wale walio ndani wamechoka.

“Kwa kweli hawa wazee wametoa mchango mkubwa sana katika kumshauri Rais na ndiyo maana mwenyewe ameona waingie kufanyia kazi yale waliyokuwa wakimshauri,” amesema.

Ametolea mfano wa masuala ya mikataba akisema kwa siku za hivi karibuni, Tanzania imeingia kwenye changamoto ya kushitakiwa kwenye mahakama za kimataifa kwa kuvunja mikataba ya uwekezaji, hali inayoashiria kuwepo kwa changamoto katika usimamizi wa mikataba ya kimataifa.

“Rais alisema Profesa Kabudi atabaki kuwa mshauri wake wa mikataba, sasa ukiangalia hivi karibuni Serikali imekuwa ikiingia mikataba bila kuwa na umakini halafu inaivunja na kisha ikishitakiwa inashindwa. Ukiangalia hapo unaona ameona amwingize mshauri wake wa mikataba na Mwanasheria Mkuu wa Serikali naye amebadilishwa,” amesema.

Mwanasiasa mkongwe ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema: “Hawa wawili ni watu wazito, wanaweza kutuliza bahari inapoyumba, Rais ameona aongeze wazee kwenye baraza la mawaziri.”

“Unajua Lukuvi anaweza kuzungumza na kusikilizwa vizuri, tunakwenda kwenye uchaguzi na ndani ya Bunge lijalo kutakuwa kwa moto kwani kila mbunge anataka kurudi, sasa lazima uwe na mtu anayeijua siasa ya Bunge.”


Profesa Kabudi ni nani?

Profesa Kabudi ni msomi, mwanasheria, na mwanasiasa maarufu. Anafahamika kwa mchango wake katika sekta ya sheria na nafasi mbalimbali za uongozi alizohudumu serikalini.

Akiwa katika taaluma ya sheria, Profesa Kabudi alifundisha na kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali ya sheria, ikiwa ni pamoja na sheria za kimataifa, haki za binadamu na sheria za mazingira.

Profesa Kabudi aliingia katika siasa na kushika nafasi mbalimbali serikalini zikiwamo za Waziri wa Katiba na Sheria (2017-2019). Mwaka 2017, hayati Rais Magufuli, alimteua kushika wadhifa huo, miongoni mwa kazi alizosimamia ni uandaaji wa sheria mpya na usimamizi wa haki nchini.

Alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mwaka 2019-2021. Aliongoza diplomasia ya Tanzania katika ngazi ya kikanda na kimataifa, akiwakilisha nchi katika mikutano na majadiliano ya kimataifa.

Profesa Kabudi amekuwa na mchango katika mchakato wa kuandaa Katiba mpya ya Tanzania na mara nyingi amehusishwa na jitihada za kurekebisha mfumo wa sheria, ili kuendana na mahitaji ya sasa. Pia, amekuwa mshauri wa kisheria katika masuala ya sera na maendeleo.


Lukuvi ni nani?

Lukuvi ni mwanasiasa na kiongozi wa muda mrefu nchini Tanzania. Anafahamika zaidi kutokana na nafasi mbalimbali za uwaziri alizoshikilia, hasa kama Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi.

Alianza siasa akiwa kijana kupitia chama cha Tanu baadaye CCM akishika nafasi za uongozi ndani ya chama hicho.

Alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira) na Waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi.

Aliongoza jitihada za kuboresha usimamizi wa ardhi nchini, kupunguza migogoro ya ardhi na kuimarisha utoaji wa hati miliki za ardhi. Alijulikana kwa utendaji kazi wenye msimamo mkali katika kutatua migogoro ya ardhi na kudhibiti uporaji wa ardhi.