Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu za vioja kufanywa bungeni

Muktasari:

  • Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amepiga marufuku vioja na vituko vinavyofanywa na wabunge wanapochangia mijadala, akisema vitendo hivyo ni kinyume na kanuni za mhimili huo wa dola.

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amepiga marufuku vioja na vituko vinavyofanywa na wabunge wanapochangia mijadala, akisema vitendo hivyo ni kinyume na kanuni za mhimili huo wa dola.

 Dk Tulia ametoa msimamo huo baada ya kuwapo kwa mfululizo wa matukio ya wabunge kuleta vituko kwa wengine kuingia na vitu visivyoruhusiwa, ingawa wenyewe wanajitetea kuwa wanafanya hivyo ili kufikisha ujumbe.

Akitoa mwongozo juzi, Spika Tulia alisema mambo kama hayo ni marufuku kwa kuwa hayamo hata kwenye kanuni za Bunge, hivyo kufanyika kwake ni kinyume na utaratibu hivyo akataka yaachwe kabisa.

Dk Tulia alitoa kauli hiyo juzi, kufuatia mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Igalula, Venance Protas aliyetaka kujua kama kanuni zinaruhusu mambo hayo.

“Kwa hawa ambao wameshafanya tuache lakini ni marufuku kufanya vitendo vya ajabu humu ndani ya Bunge. Sisi ni watu wenye hadhi na tunatakiwa kufanya mambo yenye hadhi si vinginevyo, naagiza kuanzia sasa iwe marufuku,” alisema Dk Tulia.

Matukio ya namna hiyo yalianza kujitokeza tangu Bunge la 10 pale aliyekuwa Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alipoingia na vazi aliloliita la kininja na akachangia akiwa amelivaa hadi alipomaliza.

Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio kama hayo yaliyoanzia kwa Mbunge wa Kahama, Jumanne Kishimba aliyeingia na sare na madaftari ya shule akitenganisha kati ya sare na madaftari ya shule za umma na yanayotumiwa katika shule binafsi.

Baada ya Kishimba, alifuata Mbunge wa Momba, Candester Sichalwe ambaye aliingia na chupa kadhaa za pombe kali alipokuwa anatetea kuhalalishwa kwa gongo inayotengenezwa mahali kwingi nchini huku mamlaka zikiiharamisha.

Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango Malecela aliingia bungeni akiwa na kifurushi cha tangawizi, wakati Jerry Silaa wa Ukonga alimwaga machozi huku Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay akiruka sarakasi juu ya meza na Mbunge wa Viti Maalumu, Jacquline Ngonyani akipiga magoti alipotoa hoja yake.

Kuhusu kulia ndani ya Bunge, Spika alisema hakuna madhara kwani kitendo hicho ni hisia ya mtu pale anapojisikia kuguswa na jambo husika.

Wengine wafunguka

Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango Malecela alitetea uamuzi wake kuwa ulikuwa wa maana kubwa kwani amefanikiwa alichokuwa anakihitaji, tofauti na miaka yote ambayo huwa anakizungumzia kiwanda cha tangawizi kilichopo jimboni kwake.

Kilango alitaja sababu za kuingia na tangawizi bungeni kwamba ilikuwa ni kupeleka ujumbe moja kwa moja na Watanzania wengine wajue kwamba Same kunahitaji kuwekewa nguvu kwa kuwa kilimo hicho ni tegemeo kwa wananchi.

“Na kweli nilifanikiwa, huwezi kuamini Waziri Bashe (Hussein) alikubaliana na hoja yangu na mara moja akaagiza wataalamu waende kule, lakini watu wa utafiti wa magongwa ya tangawizi wamenipigia simu wanataka kutangulia nami nikawaambia wanisubiri mwisho wa mwezi ujao nitakwenda nao,” alisema Kilango.

Kama asingefanya hivyo, alisema angeendelea kupigwa danadana kama inavyofanywa siku zote lakini kupeleka tangawizi bungeni imeleta faida kubwa, ikiwamo kukitangaza kiwanda ambacho kinajulikana kote.

Kwa upande wake Maasay alisema sarakasi kwake ni sanaa ya kufikisha ujumbe kama ambavyo wamekuwa wakifanya watu wengine, wakiwamo waimba mashairi.

Kwa mujibu wa Maasay, anaamini mchango wake mwaka huu katika barabara ya Hydom kwenda Mbulu ndio wenye tija zaidi kuliko miaka iliyopita hivyo itajengwa.

Maoni ya wadau

Mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, Dk Kedmon Mapana alisema kinachofanywa na wabunge hakipaswi kubezwa, kwani kuna ujumbe unaoifikia jamii moja kwa moja.

Dk Mapana alisema wabunge mara nyingi wanaona Serikali haiwasikilizi hivyo wanaamua kujiongeza ili kufikisha ujumbe kwa vitendo wakijua watapewa nafasi zaidi, lakini akakumbusha kuwa kwa wenye uwezo wa kujenga hoja, sio lazima wafanye vitu kama hivyo.

Hata hivyo msomi huyo alitilia mashaka kuwa wakati mwingine wabunge wanaweza kutumia ujanja wa namna hiyo kuvuruga ajenda makini inayokuwa machoni kwa Watanzania wengi.

“Kila kitu kina pande mbili, hawa watu lazima tujiulize wanamaanisha nini wanapoingia bungeni na baadhi ya vitu visivyoruhusiwa. Inaweza kuwa wanalenga kujengea hoja au wakawa na namna ya kuzima hoja ya msingi ambayo bila kufanya hivyo ingeweza kuwa kubwa,” alisema msomi huyo.

Kiongozi mstaafu wa Chama cha Mapinduzi aliyeomba asitajwe jina gazetini, alisema uamuzi wa namna hiyo ni kiashiria kuwa Bunge linakwenda kufanya kazi ya wananchi.

Hata hivyo, mkongwe huyo ambaye amewahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM alitaka umakini uwekwe kwenye matumizi ya vitu hivyo, kwani ingawa si hatari ila vikiachwa vinaweza kusababisha hatari wakati mwingine.

Alisema ujumbe wa mbunge unatakiwa kufika mahali husika hata kama hajatumia vitu vingine kama ushahidi, kwani kazi yake ni kuwasemea wananchi, siyo kuwaachia maswali kwenye utumishi wake na akashauri vitu kama hivyo vipigwe marufuku.


Kanuni za bunge

Bunge linaongozwa kwa kanuni na sheria na moja ya sheria hizo inaagiza kukaguliwa kwa kupitisha kwenye mashine maalumu kila kinachobebwa na mbunge ama mgeni anayeingia ndani ya viwanja vya bunge.

Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Teya Ntala alisema wakati Sichwale anaingiza gongo bungeni alifuata taratibu zote za kuomba kibali kutoka kwa mamlaka.

Hata hivyo, hakutoa ufafanuzi wa pombe hiyo kueleza mbunge huyo aliitoa wapi na namna alivyoisafirisha hadi kuiingiza bungeni na haikufahamika baada ya hapo pombe hiyo ilipelekwa wapi.

Kwa utaratibu uliopo katika malango yote ya kuingilia bungeni, hairuhusiwi mbunge au mgeni kuingia hata na maji ya kunywa, kwani mashine zilizopo zina uwezo wa kung’amua kilichomo mwilini mwa binadamu hata kwenye mikoba hivyo haijulikani namna gani vitu hivyo vinaingizwa.

Kuhakikisha kila anayeingia anakuwa salama, ni sharti kwa kila mbunge au mgeni kuvua mkanda, viatu au chochote chenye asili ya chuma kabla ya kupita kwenye mashine ya usalama iliyopo katika kila geti la kuingilia mjengoni hapo.

Katika hatua nyingine, Dk Tulia aliwaagiza askari waliopo katika malango yote yanayoingia viwanja vya Bunge kutowaruhusu wabunge wasiovaa mavazi ya staha ndani.

Dk Tulia alisema kanuni ziko wazi ambazo zinaelekeza namna gani mbunge anatakiwa kuvaa wakati wote anapokuwa kwenye shughuli za kibunge na akasema baadhi ya wabunge wanakuwa tofauti kabisa na takwa hilo, hivyo wasiruhusiwe kuingia mpaka wabadilishe mwonekano wao kuwa ule unaokubalika kwa mujibu wa kanuni zao.

“Hebu jiandae hata unapotoka nyumbani kwako, je, uko sahihi na ukiona hauko sahihi basi jiweke sawa ndiyo uje. Hapa tunataka mavazi ya staha na kuanzia leo nawataka maaskari wetu huko magetini kuwazuia kabisa waheshimiwa wabunge ambao wataingia na mavazi yasiyokuwa ya staha,” alisisitiza Spika Tulia.

Kuhusu suti kwa wanaume alisema hairuhusiwi mtu kuvaa nguo inayong’aa zaidi, badala yake kanuni zinataka nguo zao ziwe ni zenye rangi za kufifia kidogo.