Sabaya awataka watendaji Hai kuzitapika Sh600 milioni

Thursday April 08 2021
maagizosabayapic

Mkuu wa Wilaya ya Hai , Lengai Ole Sabaya

By Florah Temba
By Fina Lyimo

Moshi. Watendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Hai watalazimika kulipa zaidi ya Sh600 milioni wanazodaiwa na wazabuni baada ya mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya kuwapa wiki moja kulipa kiasi hicho cha fedha.

Sabaya ametoa maagizo hayo  leo Alhamisi Aprili 8, 2021 wakati akisikiliza malalamiko ya wazabuni waliohudumia halmashauri hiyo.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na kaimu mkurugenzi wa halmashauri, Herick Marsham, kaimu mweka hazina, Velda Kimaro na baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo, Sabaya amewasimamisha wanaodai mmoja baada ya mwingine na walifichua madeni ya zaidi ya Sh600 milioni.

Katika uamuzi wake, Sabaya amewapa kaimu mkurugenzi huyo na watendaji wake wanaohusika na mapato kuhakikisha ndani ya siku hizo saba wawe wamelipa madeni hayo ambayo mengine yana zaidi ya miaka minne.

Awali Kimaro alikiri halmashauri hiyo kudaiwa na wazabuni pamoja na taasisi mbalimbali na kuahidi kutekeleza agizo lililotolewa na mkuu huyo wa wilaya katika muda aliousema.


Advertisement
Advertisement