Sabaya mgonjwa, kesi yaahirishwa

Uvimbe uliopo kichwani mwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya ambapo anatakiwa kwenda kufanyiwa upasuaji

Muktasari:

Mawakili wa upande wa utetezi kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kuahirisha kesi hiyo ili Sabaya apelekwe hospitali kutibiwa kutokana na uvimbe alionao kichwani.

Moshi. Mawakili wa upande wa utetezi kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kuahirisha kesi hiyo ili Sabaya apelekwe hospitali kutibiwa kutokana na uvimbe alionao kichwani.

Akitoa ombi hilo leo Jumanne Juni 7, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Salome Mshasha, Wakili Hellen Mahuna amesema mshitakiwa namba moja ambaye ni Sabaya ni mgonjwa hivyo anapaswa kwenda kufanyiwa upasuaji.

"Mshitakiwa namba moja ni mgonjwa kutokana na uvimbe uliopo kichwani alioupata akiwa kazini, hivyo tunaomba kesi hii iahirishwe ili akafanyiwe upasuaji," amesema Wakili Mahuna

Wakili wa upande wa mashtaka,Verediana Mlenzi ameileza mahakama hiyo kuwa upelelezi bado haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.

Hata hivyo hakimu Mshasha amewataka upande wa mashitaka kutekeleza na kuzingatia kauli yao ya mara ya mwisho waliyoieleza mahakamani Juni Mosi kuwa upelelezi umekamilika.

Mahakama hiyo imeiahirisha kesi hiyo hadi Juni 20 mwaka huu.


Wanawake wamuangukia Rais Samia

Wanawake jamii ya kimasai kutoka Wilaya ya Hai pamoja na ndugu wa Sabaya wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati kesi.

 Wakiangua vilio huku wakiwa wameshika majani ya masala nje ya mahakama hiyo, wamemuomba Rais Samia ayakumbuke mazuri aliyofanya Sabaya wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.

"Ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa tunajua mwenye mamlaka ni wewe Rais wetu mama Samia tunaomba kwa huruma yako ya umama tunajua Sabaya amefanya kazi nyingi akiwa serikalini, tunaomba utekeleze neno moja tuu la huruma tunajua kama ni kufundishwa amefundishwa tunaomba huruma yako mama Samia kwa ajili ya hawa watoto” amesema mwanamke mmoja aliyetambulika kwa jina la Anna Msuya huku akitokwa na machozi

“Serikali ya Tanzania tunaomba ituhurumie tunaomba uingilie kati mama," amesema mwanamke hyo akiwa amepiga magoji pamoja na wanawake wengine nje ya mahakama