Safari ya miaka 81 ya Harith Bakari Mwapachu

Wednesday February 17 2021
By Luqman Maloto

Kifo kimemtenganisha na dunia, Harith Bakari Mwapachu. Safari yake ya kimaisha iliyoanza Julai 25, 1939, ilifikia tamati Februari 12, mwaka huu, Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar es Salaam.

Safari ya maisha ya Bakari ina uzani wake. Ndani ya utumishi wa umma mpaka siasa.

Bakari alipanda ngazi ya utumishi wa umma hadi kufikia kuwa Meneja Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, iliyoongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Uzuri, Bakari ni mtoto wa Hamza Kibwana Bakari Mwapachu, ambaye alipata kufanya kazi na Mwalimu Nyerere katika tawi la kilichokuwa chama cha harakati za wafanyazi (TAA).

Hamza na akiwa Rais wa TAA, tawi la Tabora, Mwalimu akiwa Katibu Mkuu. Hiyo ilikuwa mwaka 1947.

Hamza alikuwa tabibu katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora, Mwalimu Nyerere alikuwa akifundisha Shule ya Misheni ya St. Mary’s. Hamza na Mwalimu walikutana Tabora mwaka 1947, wote wakiwa wametokea Chuo cha Makerere, Uganda, kila mmoja kwa fani yake.

Advertisement

Na kipindi wakiwa Makerere, Hamza na Mwalimu Nyerere, walianzisha chama cha kutetea haki za wanafunzi wa Kitanganyika chuoni hapo. Chama hicho kiliitwa, “Tanganyika African Welfare Association (Tawa)”. Baadaye chama hicho kikatumika kama tawi la TAA.

Mambo mawili; kwanza Mwalimu Nyerere alipomteua Bakari kuwa Meneja Mkuu wa ATC (Air Tanzania Corporation), dhahiri alitambua ni mtoto wa nyoka.

Mwana wa mwanaharakati mwenzake wa kupigania ukombozi wa Mtanganyika. Bahati mbaya, Hamza alifariki dunia Septemba 1962, ikiwa ni miezi tisa baada ya Tanganyika kupata uhuru na miezi mitatu kabla ya Tanganyika kuwa Jamhuri.

Kipindi Hamza anafariki dunia, alikuwa na umri wa miaka 49. Bakari ameaga dunia akiwa na miaka 81.

Cheo cha mwisho kushikwa na Hamza hadi mauti yalipomkuta ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje.

Endapo utafungua faili la Bakari, utaona jinsi alivyofika mbali kimadaraka kuliko yale ya baba yake.

Kutoka utumishi wa umma, Bakari alikwea na kushika vyeo vikubwa vya kisiasa, akawa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, kisha mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uwaziri ukafuata.

Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, alipoingia madarakani, Novemba 1995, alimteua Bakari kuwa mbunge, kisha akampa uwaziri wa Katiba.

Mwaka 2000, Bakari aligombea ubunge jimbo la Tanga na kushinda, na kwenye muundo wa Baraza la Mawaziri katika muhula wa pili wa Rais Mkapa, Bakari aliendelea kuhudumia wizara hiyo ya Katiba na Sheria. Kwa kifupi, katika miaka 10 ya Rais Mpaka, ukiachana na Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye, mawaziri ambao hawakubadilishwa wizara kwa mihula yote miwili ni wawili, Bakari na Waziri wa Mambo ya Nje, Jakaya Kikwete. Kisha, Kikwete aliposhinda urais mwaka 2005, alipoteua Baraza la Mawaziri Januari 2006, alimpa Bakari uwaziri wa Usalama wa Raia.

Mwaka 2008, baada ya kashfa ya mradi wa kufua umeme wa dharura kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Wizara ya Nishati na Madini na kampuni ya Richmond, iliyosababisha kuvunjika kwa Baraza la Mawaziri, Bakari hakujumuishwa kwenye muundo wa baraza jipya lililoundwa Februari 2008.

Siku ya kutangaza baraza jipya, Rais Kikwete alisema “wanasiasa wakongwe” waliokuwa mawaziri walimuomba kupumzika. Bila shaka Bakari ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 68, alikuwa mmoja wa walioomba kukaa kando.

Hiyo ni kwa kukopa maneno ya Kikwete. Baada ya kuwa pembeni ya Baraza la Mawaziri, Bakari aliendelea kuhudumia nchi kupitia Bunge hadi mwaka 2010, alipostaafu rasmi siasa.

Tangu alipoamua kujiweka kando na majukwaa ya kisiasa, Bakari alichagua kuishi maisha ya ukimya hadi kifo kilipomchukua.

Ni familia kubwa

Bakari ni mtoto wa Hamza na Juliana ambao walikutana mwaka 1937, kisha wakafunga ndoa mwaka 1938.

Bakari ambaye alizaliwa mwaka mmoja baada ya ndoa hiyo kufungwa, ndiye mtoto wa kwanza.

Baada ya Bakari kuzaliwa, walifuata Rahma Mwapachu, maarufu kama Rahma Mark Bomani.

Rahma ni mjane wa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mzawa wa Tanzania, Jaji Mark Bomani. Hivyo, kama ulikuwa hutambui, Bakari na Mark walikuwa wakiitana “shemeji”.

Mbali ya Bakari na Rahma, watoto wengine wa Hamza na Juliana Mwapachu ni Juma Volter Mwapachu, Wendo Mtega Mwapachu, Tunu Mwapachu na Jabe Jabir Mwapachu.

Kwa ufafanuzi, Juma Volter ndiye Balozi Juma Mwapachu ambaye amepata kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na vyeo vingine vingi.

Hivyo, Bakari alitokea kwenye koo kubwa ya Mwapachu, ambayo ilisheheni tunu nyingi, kuanzia kwa baba yao hadi ndugu zake.

Miaka yake 81 imetosha mbele ya Mungu. Na hakika, kazi ya Mungu haijawahi kukatiwa rufaa.

Advertisement