Sakata la nyani wilayani Rombo latua bungeni

Muktasari:

  • Sakata la nyani katika wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro limetinga bungeni, huku mbunge ameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana nalo.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Zuena Bushiri ameiomba Serikali kuchukua jitihada za haraka kukabiliana na changamoto ya nyani katika maeneo ya wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

 Septemba 29, 2023katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Samanga kilichopo kata ya Kirongo, wilayani humo, wananchi walimtaka mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda kuwaondoa nyani hao katika makazi ya wananchi.

Nyani hao wamekuwa wakiingia ndani ya nyumba na kula vyakula, mifugo na hata mazao yaliyopo shambani, haliiliyowafanya wananchi hao kutelekeza mashamba yao wakihofia mazao yao kuliwa.

Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake leo Aprili 8,2024, Zuena amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya utalii, kuna changamoto katika msitu unaozunguka Mlima Kilimanjaro.

Amesema matukio mengi yamekuwa yakitokea ya  kuathirika kwa nyani na imefika mahali nyani walio katika msitu  wanafika  hadi nyumbani kwa watu  na wakikosa kitu cha kula wanachukua watoto.

Amesema Profesa Mkenda aliwatafuta Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo alifika waziri, naibu wake na katibu mkuu wa wizara ambao walitoa ahadi kuwa watamaliza jambo hilo.

“Lakini ni miaka miwili halijatekelezwa, watu wanaoathirika kwa kiasi kikubwa ni wanawake wamekosa amani hawaamini kwamba wanaweza kumuacha mtoto dakika tano hamuoni machoni bila kujua usalama wake,” amesema.

Amesema katika wilaya hiyo, nyani alimchukua mtoto akampeleka chini ya bonde na wananchi waliokuwepo walikimbizana wakatafuta ndizi na kisha kumrushia.

“Alimuacha mtoto akakimbilia ndizi, watu wakaenda kumuokoa. Nini wizara itafanya kwa jitihada za haraka sana kuhakikisha kuwa nyani hao wanapotea katika makazi ya wananchi,” amesema.

Amesema anatambua Rais Samia Suluhu Hassan anajali usalama wa watoto na anafahamu kuwa kama mwanamke hana ukakika na usalama wa mtoto hawezi kufanya shughuli yoyote ya kiuchumi.

Ametaka kuchukuliwa kwa hatua za haraka kukabiliana na changamoto hiyo.