VIDEO: Wanaume Rombo walalamikia nyani wa kiume kusumbua wake zao

Muktasari:

  • Wanaume wanaoishi pembezoni mwa Mto Mlembea, Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro wamelalamika wake zao kuvamiwa na nyani wa kiume na wakati mwingine kuhatarisha usalama wao.

Moshi. Wanaume wanaoishi pembezoni mwa Mto Mlembea, Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro wamelalamika wake zao kuvamiwa na nyani wa kiume na wakati mwingine kuhatarisha usalama wao.

Wamesema nyani hao wamekuwa ni tishio kwa wake zao na watoto na kwamba wakati mwingine huwavamia wakiwa mashambani, kuiba watoto wadogo wa kike na wakati mwingine wakitaka kuwabaka.

Pamoja na uvamizi huo wa nyani, wamesema nyani hao wamekuwa wakiingia ndani na kula vyakula, kula mifugo na hata mazao yaliyopo mashambani hali ambayo imewafanya kutelekeza mashamba yao wakihofia mazao yao kuliwa.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Ijumaa Septemba 29, 2023 katika Kijiji cha Samanga kilichopo kata ya Kirongo Samanga wilayani humo, wananchi hao walimtaka Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda ambaye alikuwa kwenye mkutano huo kuwaondoa kwenye makazi ya wananchi na kukwepa usumbufu huo.




Akijibu kero hiyo ya wananchi Profesa Mkenda ambaye ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia alisema hajaridhika na uondoaji wa nyani katika maeneo ya wananchi kwa kuwa bado ni wengi na wamekuwa kero kwa wananchi.