Sakata la ugonjwa usiojulikana lamponza daktari wa Chunya

Sakata la ugonjwa usiojulikana lamponza daktari wa Chunya

Muktasari:

  • Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Doroth Gwajima ameagiza kusimamishwa kazi Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chunya, Dk Felista Kisandu kufuatia sakata la kusambaa kwa taarifa ya mlipuko wa ugonjwa usiofahamika kata ya Ifumbo.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Doroth Gwajima ameagiza kusimamishwa kazi Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chunya, Dk Felista Kisandu kwa kukiuka mwongozo wa utoaji wa taarifa za milipuko kama ilivyoelezwa kwenye Sheria ya Afya ya Umma (Public Health Act) ya mwaka 2009.

Akitoa tamko leo Jumapili Februari 7, 2020 Dk Gwajima amesema Dk Kisandu anapisha uchunguzi kufuatia sakata la kusambaa kwa taarifa ya mlipuko wa ugonjwa usiofahamika kata ya Ifumbo wilayani Chunya.

“Kutokana na kadhia hii ambayo imeleta taharuki isiyo ya lazima naiagiza mamlaka ya ajira ya Dk Felista Kisandu ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chunya ichukue hatua za kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi chini ya Baraza la Madaktari na taarifa nipate ndani ya siku 10,” amesema Dk Gwajima.

Amesema katika Kata ya Ifumbo, Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya hakuna mlipuko wa ugonjwa wowote uliothibitishwa wala hakuna janga lolote la kiafya kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari.

Dk Gwajima amesema, timu ya wataalamu imefanya mahojiano na wananchi na kubaini hakuna vifo 15 kwa mara moja vya wagonjwa wanaodaiwa kuwa na dalili za kutapika damu kama ilivyoripotiwa na diwani wa Kata ya Ifumbo na takwimu hizo hazijawahi kuripotiwa popote.