Samia aahidi kutatua migogoro ya ardhi
Muktasari:
- Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameahidi kutatua changamoto ya migogoro ya ardhi inayoukabili mkoa wa Kilimanjaro kwa sasa.
Siha. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameahidi kutatua changamoto ya migogoro ya ardhi inayoukabili mkoa wa Kilimanjaro kwa sasa.
Amesema changamoto zote ambazo ameziona kupitia mabango yenye ujumbe nyingi ni za migogoro ya ardhi, maji na maslahi ya watumishi huku akiahidi kwamba, atazichambua na kuzipatia ufumbuzi.
Soma zaidi:Rais Samia kuanza ziara Kilimanjaro kesho
Rais Samia ameyasema hayo Ijumaa Oktoba 15, 2021 wakati akizindua barabara ya Sanya Juu - Elerai iyojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 32.2 na kugharimu kiasi cha Sh62.7 bilioni.
"Tunapita kuangalia yaliyotendeka na kuona changamoto zilizopo na hapa naona mabango mengi, kuna migogoro ya ardhi na maslahi ya wafanyakazi naomba tuyakusanye halafu tutakwenda kuyafanyia kazi.
"Changamoto hizi tutakwenda kuzifanyia kazi na ahadi yetu CCM ni kuangalia kero za wananchi na kuzifanyia kazi," amesema Rais Samia na kuongeza:
"Najua hapa Kilimanjaro kuna changamoto ya maji na migogoro ya ardhi ambayo ndio kubwa zaidi n azote hizi nimeziona kwenye mabango hivyo, nitazichukua kwenda kuzichambua na kuzifanyia kazi."
Hata hivyo, Rais Samia amesema wapo baadhi ya wananchi waliojenga kwenye maeneo ya Serikali na wametakiwa kuondoka hivyo, ataangalia namna bora ya kushughulikia changamoto hiyo na kuipatia ufumbuzi.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Rogatus Mativila amesema ujenzi huo ulianza mwaka 2019.