Samia akerwa upigaji miradi ya maendeleo

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kagera katika Maadhimisho ya Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru ambayo yamefanyika uwanja wa Kaitaba, Bukoba - Kagera Oktoba 14, 2022. Picha na Ikulu
Muktasari:
- Aiagiza Takukuru, Zaeca na vyombo vingine kuingia kazini
Bukoba. Rais Samia Suluhu Hassan amehitimisha siku 195 za mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba jana kwa kuonyesha hadharani kuchukizwa na taarifa za kila mwaka za uwepo wa vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizinduliwa Aprili 2, mkoani Njombe na kufikia kilele jana ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999.
Akihutubia juzi, Rais Samia alisema si sahihi taarifa za rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma zijirudie kila mwaka katika ripoti za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) huku kukiwa na vyombo na taasisi zenye dhamana ya kudhibiti vitendo hivyo.
“Kila mwaka tunapokea taarifa za kilele cha mbio (za Mwenge wa Uhuru) au taarifa ya CAG tunasomewa na kutajiwa maeneo ambayo Mwenge umekataa kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ambayo utekelezaji wake umekiuka kanuni za ujenzi au kutumia fedha nyingi ikiwa chini ya kiwango kinachokubalika,” alisema Rais Samia.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Sahili Geraruma walieleza kuwa jumla ya miradi 65 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh12 bilioni ilikataliwa na Mwenge katika Halmashauri 43 kutokana na kasoro kadhaa.
Miongoni mwa kasoro hizo ni miradi kutekelezwa chini ya kiwango, uwepo wa vitendo vya rushwa, kukosekana kwa nyaraka na nyingine kutolingana na thamani halisi ya fedha.
Pamoja na miradi kukataliwa, Mwenge wa Uhuru pia ulibaini baadhi ya halmashauri hazijarejesha zaidi ya Sh2.2 bilioni za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya mikopo kwa vijana nchini.
Kutokana na taarifa hizo, Rais Samia aliiagiza Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca) kuchunguza vitendo vyote vya rushwa na ubadhirifu vilivyoibuliwa
Akionyesha msisitizo, Rais Samia alisema “hapa kuna swali kubwa la kujiuliza wakati miradi hii inajengwa, viongozi tupo na tunaona, lakini hakuna kinachozungumzwa wala kusema hadi Mwenge wa Uhuru upite, huu sio mtindo mzuri,” alisema. Aliwaagiza viongozi wote, kila mmoja kwenye eneo na mamlaka yake kusimamia matumizi mazuri ya fedha za umma, ikiwemo kudhibiti tabia ya baadhi ya watendaji wasio waaminifu wanaotoa kandarasi za miradi kwa wakandarasi wasio na uwezo na wazembe.
“Haya yanatokea viongozi tukiwa tupo katika ngazi zetu tofauti, kuanzia Taifa, mikoa, wilaya hadi halmashauri...tunasubiri vijana wakimbiza Mwenge (ndio) waje kusema miradi mibovu na haiendani na (thamani ya) fedha zilizotumika,” alisema Rais Samia.
Pia aliviagiza vyombo vingine vya ulinzi na usalama kushirikiana na Takukuru na Zaeca kuchunguza vitendo hivyo, huku akivipa changamoto ya kujipekua na kujichunguza vyenyewe kwanza kama vipo sawa kabla ya kushughulikia rushwa katika taasisi nyingine.
Kiongozi mbio za Mwenge
Kiongozi wa mbio za Mwenge, Sahili Geraruma alitaja baadhi ya kasoro zilizogundulika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni miradi kugharimu fedha nyingi ukilinganisha na thamani halisi, makosa katika mikataba na makadirio makubwa ya kitaalamu katika miradi.
“Pia lipo tatizo la ukwepaji wa ulipaji wa kodi, kodi ya zuio haikuwa katika miradi mingi inayotekelezwa, hata inapokatwa haiwasilishwi TRA. Matumizi duni ya vifaa vya ujenzi na ukiukwaji wa taratibu zake.
“Katika utekelezaji wa miradi ya elimu na afya, madaktari na walimu wamebebeshwa majukumu mazito ambayo hawana weledi nayo la kusimamia miradi ya ujenzi kama wahandisi, wahasibu, watunza vifaa, maofisa manunuzi na masuhuli. Utarartibu huu umekuwa chanzo cha dosari katika miradi,” alisema Geraruma. Upotevu na kuficha nyaraka za miradi inayosababisha malipo hewa na upotevu wa fedha za umma ni mwanya mwingine uliobainika kufuja fedha za umma katika miradi kadhaa.
Imeandikwa na Alodia Dominick (Bukoba), Saada Amir (Mwanza na Bakari Kiango (Dar)