Samia akerwa wakuu wa mikoa kutosikiliza wananchi

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amesema mkuu wa mkoa ni mwakilishi wake katika eneo alilopewa

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameonekana kutoridhishwa na kitendo cha baadhi ya wakuu wa mikoa kutofanya kazi zao kikamilifu badala yake changamoto nyingi kutatuliwa anapokwenda kiongozi mkubwa akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Ametoa kauli hiyo leo Machi 13, 2024 katika hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali wakiwamo wakuu wa mikoa Ikulu jijini hapa.

Samia amesema, Rais wa nchi amekuwa mtu asiyelala, huku akitolea mfano kuwa mvua inaponyesha mara zote hujiuliza wapi kumezama, wapi atasikia daraja limeporomoka.

“Jua, likitoka hulali, je wakulima watapata chakula kweli, vyanzo vya maji vitakauka, je itakuwaje, nanyi wakuu wa mikoa mnatakiwa kuwa hivyo kwenye mikoa yenu, nimeona kesi nyingi hadi aje Waziri Mkuu azunguke huko, akafungue nini, wakuu wa mikoa mpo,” amesema Samia.

Amesema wakuu hao wa mikoa waliwaapisha wakuu wa wilaya ambao walipewa vipande vya ardhi kuviendesha lakini mambo hayaendi.

“Nataka niwakumbushe kwamba, ninyi ndiyo marais wa maeneo yale, shida yoyote ya eneo lile ni shida yako, kama nilivyo mimi nina mawaziri makatibu wakuu nanyi mnao mna wakuu wa wilaya, makatibu tawala hao wote wamewekwa kuwasaidia kazi,” amesema Rais Samia.

Amesema si vyema nchi kwenda huku ikisubiri kiongozi kama Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda apite ndiyo asikilize kero si sawa huku akimtaka kila mtu kusimama katika eneo lake.

“Shida yoyote ya pale ni yako, mradi wowote ulioletwa usimamie ni wako hata kama ni wa sekta binafsi, tumesema tunakwenda kufanya kazi pamoja na sekta binafsi, hivyo hakikisha anaweka mradi ule unakwenda kusaidia na kufanya nini,” amesema Samia.

Amesema anapoamua kumuuliza mkuu wa wilaya anakuwa na lengo la kujua kama anafahamu kinachoendelea lakini mtu sahihi wa kuulizwa ni mkuu wa mkoa na waziri.

Pia, amewataka kusimamia kero za wananchi, huku Makonda alipozunguka wameona mfano namna wananchi walivyo na kero ambazo nyingine ni nyepesi zinazoweza kutatuliwa.

 “Wasiposikilizwa zile ndiyo kura zetu, wasiposikilizwa akipita mwingine akiwambia mimi nikiingia nitawasikiliza watampa, kwamba sisi tumewapuuza hatuwasilikizi, kule ndiyo uliko ushindi wa chama kilichowaweka, vinginevyo watapita wengine watabeba ushindi waondoke nao,” amesema Samia.

Amesema baadhi ya wakuu wa mikoa wamekuwa wakiwasiliza wananchi na wamekuwa wakiangalia namna wanavyotatua kero zao kupitia ‘video clip’ anazozipata.

“Wale ambao hamjaanza au mnafanya kidogokidgo mjini hamshuki chini hebu nendeni, muwa surprise (muwashangaze) wakuu wa wilaya wasijue kuwa mnakwenda, fika pale sema mnasikiliza wananchi muone wananchi watakavyokuja,” amesema Samia.