Samia ateta na walimu, amtaka Biteko kumfikiashia kero zao

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kutatua changamoto zilizopo kwenye Sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya walimu kote nchini.

Bukombe. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kutatua changamoto zilizopo kwenye Sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya walimu kote nchini.

 Akizungumza kwa simu kutoka nchini Qatar wakati wa maadhimisho ya siku ya walimu duniani yaliyofanyika katika Wilaya ya Bukombe, Rais Samia amesema alikua ashiriki pamoja nao lakini anawatia moyo wafanye maadhimisho mazuri na maazimio watakayopitisha yatafanyiwa kazi na Serikali.

Bila kutaja changamoto zilizotatuliwa Rais Samia amesema walimu ni jeshi kubwa na Serikali ipo tayari kusikiliza changamoto zinazopwakabili na kuzifanyia kazi na kwamba tayari wameanza kuzipunguza ili hali za walimu ziwe nzuri.

“Mama yenu niko Qatar nahangaika kutafuta, nikitoka hapa nitaenda India na kwenyewe naenda kutafuta, niombeeni nirudi na neema tuje tujenge nyumbani; nimemwambia Naibu Waziri Mkuu awasikilize vizuri alafu aniletee yale mtakayokubalina tuone namna tutakavyoyatekeleza,” amesema Rais Samia.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambae ni Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda amesema tayari Serikali imeanza kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya elimu ikiwemo kulipa mbalimbikizo ya mishahara.

Kazi nyingine iliyofanywa ni kuwapandisha walimu madaraja, kujenga miundombinu ya shule ununuzi wa vifaa vya shule pamoja navile vya Tehama.

Amesema kwa mwaka 2022/23  Serikali imetoa afua mbalimbali zinazolenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji  kwa kumthamini mwalimu na kutambua utaalam wake ili kufikia mpango wa maendeleo ya sekta  ya elimu ya mwaka 2025.

“Uboreshaji huu umejikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo mapitio ya rasimu ya sera ya elimu ya mafunzo ya mwaka 2014 na kuandaa rasimu ya sera ya 2014 na tolep la 2020 na rasimu ya elimu iliyoboreshwa kuanzia ngazi ya awali, msingi, sekondari na vyuo,”

Aidha amesema Serikali imejikita kwenye mapitio ya sera ya elimu na mafunzo sera na mitaala ya ngazi mbalimbali pamoja na kukarabati na kujenga shule mpyaambapo alisema kwa mwaka 2022-23 shule mpya 883 zilijengwa maeneo mbalimbali nchini.

Maboresho hayo yameenda sambamba na kuajiri walimu zaidi ya 13,000 wakiwemo wakufunzi 200 wa vyuo pamoja na walimu 4,241kupata mafunzo yenye lengo la kuwasaidia kufundisha kwa umahiri.

Akizungumzia sekta ya elimu Mkoani Geita Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema mkoa huo unashule 963 na kwenye uongozi wa amu ya sita madarasa 2,441 yamejengwa na kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.

Amesema Kwa kipindi cha miaka miwili shule mpya zaidi ya 120 zimejengwa,maabara za sayansi 116,nyumba za walimu 65 zilizopunguza changamoto za makazi kwa watumsihi pamoja na mabweni 74 yaliyowezesha watoto wa kike kusoma kwenye mazingira rafiki na kuwaepuhsa na vishawishi njiani.

Katika kuboresha sekta ya walimu watumsihi zaidi 10,000 walipanda madaraja mkoani humo na kati ya hao zaidi ya 8000 ni walimu.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa NIshati ambae pia ni mbunge wa jimbo la Bukombe aliyeshirikiana na walimu kuandaa siku hiyo amewashukuru walimu kwa moyo wao wa kufundisha na kufanikiwa kuinua sekta ya elimu katika Wilaya hiyo.

“Kazi yenu tunaitambua na kuithamini na tunaamini bila ninyi hatuna Bukombe iliyobora zaidi tunatamani kujen ga Bukombe bora kuliko tuliyoikuta na hatuwezi kuifikia bila ninyi walimu”alisema Biteko.

Baadhi ya walimu Hamis Juma na Betha Emanue wakizungumzia changamoto zinazowakabili walisema pamoja na serikali kuwapandisha madaraja lakini bado wapo walimu ambao bado hawajafikiwa.

Changamoto nyingine ni wingi wa wanafunzi usioendana na uwiano wa walimu waliopo,madai ya malimbikizo pamoja na wingi wa wananfunzi darasani.