Rais Samia awapigia walimu simu akiwa Qatar, awapa ahadi nzito

Sehemu ya umati wa walimu wa Wilaya ya Bukombe waliohudhuria hafla ya maadhimisho ya siku ya walimu duniani yanayofanyika Oktoba 6, kila mwaka. Maadhimisho hayo yamefanyika mjini Ushorombo, Makao Makuu ya Wilaya ya Bukombe. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

Maadhimisho ya siku ya Walimu duniani hufanyika Oktoba 6 kila mwaka ambapo kwa mwaka huu, walimu wa Wilaya ya Bukombe wamewawakilisha wenzao kote nchini kuadhimisha siku hiyo muhimu huku Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akiwa mgeni asmi.

Bukombe. Rais Samia Suluhu Hassan amewataa walimu kote nchini kuchapa kazi kwa bidii, weledi na kujitolea huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto kero na changamoto zote zinazoikabili sekta ya elimu.

Akizungumza kwa njia ya simu leo Oktoba 6, 2023 akiwa nchini Qatar, Rais Samia amesema Serikali itaendeleoa kuboresha mazingira na miundobinu ya kufundishia na kujifunzia katika taasisi za elimu za umma.

Kupitia simu ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuadhimisha ya Siku ya Walimu Duniani inayiadhimishwa Oktoba 6, kila mwaka ambayo kwa mwaka huu yamefanyika wilayani Bukombe, Mkuu huyo wa nchi amesema Serikali iko tayari kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili walimu na tayari imezipunguza kwa kiwango kikubwa kulingana na uwezo wa kibajeti.

Rais Samia ameuambia umati wa walimu wa Wilaya ya Bukombe waliohudhuria hafla hiyo kuwa; “Mama yenu niko Qatar, nahangaika kutafuta na nikitoka hapa naenda India; na kwenyewe naenda kutafuta. Niombeeni nirudi na neema tuje tujenge nyumbani,’’

Huku akionyesha kufahamu uwepo wa hafla hiyo, Rais Samia amesema amemwagiza Dk Biteko kuwasikiliza walimu hao na kuwasilisha kwake hoja na maazimio ili Serikali ione namna ya kuyashughulikia.

Akizungumza na washiriki, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda amewahakikishia walimu kuwa Serikali itashughulikia na kutatua kero zote zinazoikabili sekta ya elimu huku akitaja malipo ya malimbikizo ya madai ya walimu kama ishara ya nia njema ya Serikali.

Ametaja mambo mengine yanayofanywa na Serikali kutatua kero na changamoto za muda mrefu za walimu kuwa ni kuwapandisha madaraja, kujenga na kukarabati miundombinu katika shule za umma.

Maboreshaji na mapitio ya sera ya elimu ya mafunzo ya mwaka 2014 ni eneo lingine linalotajwa na Waziri Mkuu mstaafu huyo kuonyesha nia ya Serikali ya kurekebisha kasoro zinazoikabili sekta ya elimu.

Ajira mpya kwa walimu zaidi ya 13,000 wakiwemo wakufunzi 200 vyuoni na mafunzo ya umahiri kwa walimu 4,241 ni mambo mengine aliyoyataja Pinda kuwa yanaonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha sekta hiyo muhimu.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema dhamira ya Serikali katika maendeleo ya sekta ya elimu inaonekana mkoani humo kupitia ujenzi na maboresho ya miundombinu katika shule za umma 963 za mkoa huo.

‘’Kwa mkoa wa Geita pekee, Serikali imejenga vyumba 2, 441 vya madara, shule mpya zaidi ya 120, maabara za sayansi 116, nyumba 65 za walimu 65 na mabweni 74 kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule,’’ amesema RC Shigella

Akizungumza na walimu hao, Dk Biteko ambaye pia ni mbunge wa Bukombe amewaomba walimu nchini kufanya kazi kwa moyo wa kujitolea ili kujenga jamii bora ya sasa na siku zijazo.

“Serikali inatambua na kutamini kazi kubwa inayofanywa na walimu nchini; bila walimu hatuna Bukombe na Tanzania bora sasa na hata baadaye. Hakuna jamii inayoweza kupiga hatua kimaendeleo katika sekta zote bila mchango wa walimu,’’ amesema Dk Biteko

Mmoja wa walimu waliohudhuria hafka hiyo, Hamis Juma amepongeza hatua ya Serikali ya kuwapandisha madaraja walimu huku akiomba jambo hilo litekelezwa kwa wote wanaostahili.

Mwalimu Betha Emanue yeye ameiomba Serikali kuendelea kutoa nafasi za ajira mpya kwa kada ya ualimu kuondoa tatizo la uwiano usio sawa kati ya idadi ya walimu na wanafunzi.