Samia atoa tani 300 za chakula kwa  waathirika wa mafuriko ya Rufiji

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele muda mfupi baada ya kupokea msaada wa vyakula uliotoka nyumbani kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili kusaidia waathirika wa mafuriko wilayani Rufiji mkoani Pwani. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Raisi Samia Suluhu Hassan ametoa msaada binafsi wa tani 300 za vyakula kwa waathirika wa mafuriko wilayani Rufiji mkoani  Pwani.

Rufiji. Rais Samia Suluhu Hassan leo amekabidhi msaada wa tani 300 za chakula ukiwemo mchele, unga na maharage kwa watu walioathiriwa na mafuriko Rufiji mkoani Pwani.

Msaada huo umekabidhiwa leo Jumatatu Aprili 15, 2024 kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge huku utaratibu wa kuwafikia walengwa ukiendelea kufanyika.

" Rais ameleta msaada huu kutoka kwake yeye binafsi na siyo kutoka serikalini, ili usaidie waathirika wa mafuriko," amesema Kunenge.

Amesema leo amepokea tani 32 za mchele huku  kiasi kingine kinatarajia kufikishwa wakati wowote.

Mkuu huyo wa mkoa amesema ofisi yake itahakikisha msaada huo unawafikia walengwa kwa kufuata utaratibu utakaopangwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele amesema msaada huo umefika wakati muafaka kwa sababu hitaji la vyakula kwa waathirika ni kubwa hivi sasa.

“Kwa hiyo tutahakikisha kila mlengwa tunamfikia na tunamshukuru sana Rais Samia kwa kuwakumbuka wananchi hawa,” amesema Meja Gowele.

Innocent Mbilinyi aliyewasilisha msaada huo amesema kiasi kingine kitawasili wakati wowote ili kutimiza idadi ya tani 300.

Wananchi wa Wilaya ya Rufiji wameendelea kupata adha ya mafuriko yanayotoka na mvua zinazoendelea kunyesha, huku baadhi yao wakipoteza makazi na mali.