Samia awasili Uganda, kushuhudia kusainiwa mkata bomba la mafuta

Muktasari:

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya ziara ya siku moja nchini Uganda kwa mwaliko kuhudhuria hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka nchini humo mpaka jijini Tanga.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewasili nchini Uganda kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa bombo la mafuta kutoka Hoima mpaka Chongoleani jijini Tanga kati ya Serikali ya Uganda na kampuni zinazouteleza mradi huo, East Africa Crude Oil Export Pipeline (EACOP).

Baada ya kuwasili Samia alikagua gwaride kabla ya kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Yoweri Museven.

Rais Samia amewasili nchini Uganda leo, Aprili 11 ikiwa ni ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipoapishwa kuiongoza Tanzania, Machi 19 baada ya kifo cha Dk John Pombe Magufuli kilichotokea Machi 17.

EACOP ni mradi unaotekelezwa na kampuni mbili za kimataifa ambazo ni Total na CNOOC huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na lile la Uganda (UNOC) yakiwa wabiwa wanaolinda masilahi ya Serikali.

Mkataba huo ulikuwa usainiwe Machi 22 lakini kutokana na kifo cha Rais Magufuli ulisogezwa mbele.

Hafla ya utiaji saini mkataba huo inafanyika Ikulu mjini Entebbe na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi zote mbili pamoja na wawkilishi wa kampuni zitakazotekeleza ujenzi wa mradi huo.