Samia aweka jiwe la msingi mnara wa mashujaa
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan ameweka mkuki na ngao huku akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa mnara mpya wa mashujaa ikiwa ni utekelezaji wa agizo lake alilolitoa Julai 25, 2022.
Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa mnara wa kumbukumbu ya mashujaa unaojengwa katika Mji wa Mtumba mkoani Dodoma.
Rais Samia ameweka jiwe leo Jumanne Julai 25, 2023, wakati wa maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya mashujaa.
Shughuli nyingine zilizofanyika ni kuweka mchanga wa ujenzi, Rais Samia kusaini kitabu maalum cha maombelezo ya mashujaa na kupigwa kwa mizinga miwili, ambapo kulifuatia hali ya ukimya kwa dakika moja.
Shughuli nyingine ni kikundi cha buruji ya kupiga wimbo wa mwisho na kisha kupiga wimbo maalum wa maombolezo.
Pia Rais Samia ameweka mkuki na ngao katika mnara wa kumbukumbu ya siku ya mashujaa na kufuatiwa na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda, ambaye ameweka sime.
Pia Kiongozi wa mabalozi aliweka shada na maua pamoja na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa David Mwamfupe kuweka upinde na mishale na shujaa wa Taifa aliyepigana vita vya Kagera Brigedia Jenerali Mstaafu Ambrose Bayeke kuweka shoka kwenye mnara.
Kwa mujibu wa taarifa toka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), siku hii muhimu katika historia ya nchi, ni maalum kwa ajili ya kuwakumbuka Mashujaa waliopoteza maisha yao, wakiutetea, kuupigania na kuulinda uhuru wa Tanzania.
Maadhimisho haya maalum hufanyika kila ifikapo Julai 25, na kitaifa; hufanyika katika mkoa ambao huteuliwa kwa ajili ya shughuli hiyo, ambapo mwaka huu maadhimisho hayo yamefanyika kitaifa mkoani Dodoma.
Shughuli ambazo hufanyika katika siku hiyo maalum, ni pamoja na gwaride rasmi la maziko, ambalo hufuatiwa na uwekaji wa vifaa mbalimbali kama ngao, mkuki, shada la maua na sime katika minara ya kumbukumbu za mashujaa.
Pia huambatana na kufanyika kwa dua na sala maalum ya kuwaombea mashujaa hao, lakini pia kuiombea amani nchi.