Samia: Jiandaeni kupokea ugeni

Muktasari:
- Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi na wakuu wa sekta na taasisi za umma kujipanga kuupokea ugeni unaotumia vyombo vikubwa vya habari vya kimataifa watakaokuja kuitangaza Tanzania.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi na wakuu wa sekta na taasisi za umma kujipanga kuupokea ugeni unaotumia vyombo vikubwa vya habari vya kimataifa watakaokuja kuitangaza Tanzania.
Amesema ugeni unakuja baada ya kuvutiwa Tanzania kuwa na rais mwanamke na wanaitaka kumtangaza kiongozi huyo pamoja na Taifa lake.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi ameeleza hayo leo Jumamosi Juni 26, 2021 wakati akihitimisha mkutano wa 12 wa Baraza la Taifa la Biashara (TBNC) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Wakati wowote unapoitwa kutoa taarifa jipangeni. Toeni hizo taarifa nendeni nao wanataka wakaone Ngorongoro nendeni nao, tunasema kuna kimondo Songwe kitayarishe wakija waende."
“Wanataka kuiambia dunia kuwa kuna huyu (Rais Samia) maisha yake kaanza hivi kafika hadi hapa. Lakini changamoto anazokabiliana nazo katika kuongoza ni hizi, tukiwasaidia hapa na hapa hii nchi itafika hapa,” amesema Rais Samia.
Amewaambia watendaji wa taasisi na sekta hizo ikiwemo ya usafiri na usafirishaji kuwa wana kazi ya kutoa taarifa namna walivyojipanga na mipango ikoje. Pia, sekta biashara ikoje, mipango, maeneo wanayotakiwa kuwekeza na malighafi inayopatikana.
“Hawa watu nitazunguka nao karibu Tanzania yote kuchukua picha na kuwaonyesha yaliyokuwemo . Ni programu ghali itakayoanza Septemba lakini ikimalizika itatunyanyua Tanzania, ule ukweli uliokuwa hausemwi kuhusu Tanzania kupitia mpango utausema.
“Hii programu haitumii fedha za Serikali wala za vyama vya siasa wanachukua kutoka taasisi za sekta binafsi kwa hiyo nitasambaza barua na naomba mnisaidie. Mnichangie ili tuikalimishe hii programu benki zote, mashirika tutaomba watuchangie,” amesema.
Pia, amewaomba wafanyabishara wanaojiweza kuchangia mchakato huo ili mpango huo utimie na hatimaye kuitangaza Tanzania pamoja na kuvutia wawekezaji.
Kwa mujibu wa Rais Samia, programu hiyo kwa Afrika imefanyika Rwanda pekee yake, akisema Tanzania itakuwa nchi ya pili katika mchakato huo. Amewaomba wafanyabiashara kutomwangusha katika mpango huo utakaokuwa na manufaa makubwa kwa Taifa.