Samia kupangua safu ya wasaidizi wake serikalini

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wajumbe wa mkutano mkuu wa 10 wa chama hicho, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Katika hali ya kubainisha kuwepo kwa mabadiliko ya ndani ya Serikali, Rais Samia amesema baadhi ya wa watu ndani ya Serikali hiyo hawaendani na kasi yake.

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake, amebaini kuwepo kwa baadhi ya watu wasioendana na kasi yake.

Ameyasema hayo leo Desemba 8, 2022 wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa 10 wa CCM Jijini Dodoma.

Kufuatia hali hiyo Rais Samia amewaomba wanachama hao kumuombea kwani anakwenda kuipanga Serikali yake.

“Yaliyoelezwa hapa ni utekelezaji wa miaka miwili lakini katika safari yangu ya miaka miwili nimeona kabisa kuna watu mwendo wao hauendani na kasi yangu,” amesema Samia.


Samia amesema katika safari ya miaka mitatu iliyobaki kabla ya kuwajibishwa kwa wananchi Serikali zote mbili zisimame kufanya kazi ili kupata kitu cha kuwaambia wananchi.

Aidha Samia amewataka wanachama hao kufanya mambo mazuri hata yasiyokuwa kwenye ilani ya CCM ikiwa yataleta matokeo chanya kwa Serikali na wananchi.

Wakati Samia akiyasema hayo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema CCM itaendelea kuenzi mema yaliyofanywa na waasisi wa Chama cha Mapinduzi kwaajili kuongeza ukakamavu kwenye chama hicho.

“Natoa ahadi kuendeleza mafanikio yote yaliyoanzishwa kwenye awamu zilizopita na kuzifanyia kazi changamoto zilizopo ili chama hicho kiwe imara,” amesema Dk Mwinyi.