Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia: Tanzania kujitosheleza kwa asilimia 60 dawa ifikapo 2030

Muktasari:

  • Ameeleza kuwa kuongeza uzalishaji wa ndani kutasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa hizo kutoka nje, sambamba na kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu nchini.

Dar es Salaam. Serikali imeweka lengo la kufikia asilimia 60 ya kujitosheleza kwa uzalishaji wa dawa na vifaa tiba ifikapo mwaka 2030, huku Rais Samia Suluhu Hassan akimtaka Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe, kuharakisha utekelezaji wa mkakati huo.

Akizungumza leo, Jumatano, Julai 1, 2026, Ikulu, Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, Rais Samia amesema viongozi hao wanaanza majukumu yao katika kipindi muhimu ambacho Serikali inaanza kutekeleza Mpango mpya wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Walioapishwa ni Dk Magembe, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Charles Kadonya, aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Norasco Kipanda, ambaye ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma.

Baada ya kuwaapisha, Rais Samia amesema viongozi hao wanapaswa kuanza kazi mara moja kwa kuwa hakuna nafasi ya kupoteza muda ikiwa Serikali inataka kufikia malengo ya maendeleo iliyojiwekea.

“Hakuna muda wa kupumzika. Nafasi hizi si za heshima tu, bali ni dhamana ya kuwatumikia wananchi,” amesema.

Amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji taasisi imara, uongozi wenye uwajibikaji na viongozi wanaotoa matokeo yanayopimika.


Akimuelekeza Dk Magembe, amesema Serikali imejipanga kupunguza utegemezi wa dawa na bidhaa za afya kutoka nje ya nchi kwa kuimarisha uzalishaji wa ndani.

“Lengo letu ni kufikia asilimia 60 ya kujitosheleza kwa dawa na vifaa tiba ifikapo mwaka 2030. Hakikisha mnawavutia wawekezaji kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa, vifaa tiba na, hasa, chanjo hapa nchini,” amesema.

Ameeleza kuwa kuongeza uzalishaji wa ndani kutasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa hizo kutoka nje, sambamba na kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu nchini.

Pia, amemtaka Dk Magembe kuhakikisha bajeti ya Wizara ya Afya inasimamiwa kwa ufanisi, akisisitiza kuwa, pamoja na rasilimali za Serikali kuwa chache, matumizi mazuri yanaweza kuleta matokeo makubwa.

“Rasilimali hazitawahi kutosha, lakini matumizi sahihi yanaweza kuleta matokeo makubwa,” amesema.

Aidha, amemhakikishia ushirikiano kutoka Ofisi ya Rais, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa malengo hayo utafuatiliwa kwa karibu.

Kwa upande wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais Samia amemtaka Kadonya kulinda maslahi ya Tanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku akichangia kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

Amesema uzoefu wake katika masuala ya kikanda unapaswa kutumika kuhakikisha ushiriki wa Tanzania ndani ya jumuiya hiyo unazaa manufaa ya moja kwa moja kwa nchi.

“Kalinde maslahi ya Tanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku ukihakikisha jumuiya inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema.

Kwa upande wa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Norasco Kipanda, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha tume hiyo inazingatia haki, uadilifu na usawa katika kushughulikia masuala ya watumishi wa umma.

Amesema kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya watumishi kuchukuliwa hatua za kinidhamu bila kuzingatia haki, hivyo ameitaka tume kurejesha imani kwa kufanya uamuzi unaozingatia sheria na haki.