Prime
Saratani ya matiti inavyowatesa mabinti

Dar/Mikoani. Katika siku za hivi karibuni imebainika saratani ya matiti huwapata wagonjwa wakiwa na umri chini ya miaka 20 mpaka 40, tofauti na awali, ambao baadhi wamejikuta wakiondolewa matiti.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ongezeko la matumizi yasiyo sahihi ya dawa za homoni, zikiwamo za kuzuia na kutoa mimba; uzazi wa mpango, dawa zinazotumika kupunguza uzito, zamitishamba na vipodozi huchochea saratani ya matiti.
Madaktari bingwa wa magonjwa ya saratani, wanaonya iwapo hakutazingatiwa matumizi sahihi ya dawa hizo, itarajiwe kuwepo ongezeko la waathirika miaka michache ijayo.
“Kuna wagonjwa wanabainika na saratani ya matiti wakiwa na umri chini ya miaka 20 mpaka 40 tofauti na zamani. Katika hili tunaangalia ni vitu gani viliingia hapo nyuma hadi hali hii inaanza kutokea, tukiangalia miaka ya 1990 tulianza kula vyakula visivyo vya asili na ndipo hata uzito kupindukia ulipoanzia,” anasema mkurugenzi wa huduma za kinga Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Crispin Kahesa.
“Matumizi mengi ya dawa za homoni yameanza miaka ya 2000, lakini kufikia mwaka 2010 yakaanza kuwa makubwa, madhara yake tutayaona mwaka 2030, ikiwa ni miaka 20 baadaye,” anasisitiza Dk Kahesa.
Mfamasia na mkufunzi wa shule ya famasia kutoka Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas), David Myemba anasema dawa za kuongeza maumbile ambazo wanawake hutumia kwa lengo la kukuza makalio na matiti zina hatari kubwa zaidi.
“Miili yetu ina chembechembe hai nyingi ambazo huzaliana, hukua na kufa kwa mpangalio maalumu. Chembechembe hizi zinapobadilika na kuanza kuzaliana na kukua katika utaratibu ambao siyo wa kawaida ndiyo zinasababisha saratani.
“Sasa hizi dawa za kuongeza maumbile zinaulazimisha mwili kukuza hizo chembechembe iwe kwenye maziwa au makalio zinafanya hiyo kazi, zinaenda zinaongeza zile seli na hapo ndiyo chanzo cha saratani na inajitokeza baadaye sana,” anasema.
Mnyemba anasema dawa za homoni zinazojumuisha zile za uzazi wa mpango, vidonge vya dharura vya kuzuia mimba (P2) na baadhi ya vipodozi vyote vina homoni ya estrojeni ambayo ikizidi huleta madhara.
Anataja dawa zinazoongeza hatari ya kupata saratani ya matiti kuwa ni zenye estrojeni, ambazo pia huweza kusababisha kiharusi na udhaifu wa mifupa.
Njia za uzazi wa mpango
Uhusiano kati ya njia za uzazi wa mpango na saratani ya matiti bado hauko wazi, ijapokuwa kuna tafiti nyingine zinazoonyesha kidogo kuna ongezeko la saratani ya matiti kutokana na sababu hiyo, lakini nyingine zinaonyesha hakuna uhusiano.
Dk Lugina anasema, “katika utoaji dawa huwa tunaangalia faida na hasara. Vidonge vya uzazi wa mpango vina faida kuliko hasara ndogo inayoweza kusababisha saratani ya matiti. Katika visababishi vya saratani ya matiti, ambavyo vipo vingi, lakini ambavyo vina nguvu siyo vidonge ni visababishi vingine vinavyohusiana moja kwa moja kuliko vidonge vya uzazi wa mpango.”
Dk Lugina anasema matiti yametengenezwa mfano wa kiwanda, lazima kitumike na tafiti zinaonyesha mama anayenyonyesha kwa muda mrefu au watoto wengi inaweza kuwa kinga kwake na anaweza asipate saratani ya matiti.
Hata hivyo, wataalamu wanafafanua kuwa matumizi ya vidonge hivyo siyo shida, isipokuwa yaliyo holela na ya muda mrefu huchangia zaidi saratani hiyo.
Daktari bingwa wa upasuaji sanifu, rekebishi na matiti katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, Marianne Gnanamuttupulle aliiambia Mwananchi kuwa, saratani ya matiti inasababishwa na sababu mbalimbali, ikiwemo matumizi ya muda mrefu na makubwa ya vidonge vya uzazi bila ushauri wa madaktari.
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi KCMC, Dk Rafiki Mjema anasema tatizo ni baadhi ya kinamama kutumia vidonge hivyo holela bila ushauri wa kitaalamu.
Anasema uhusiano kati ya vidonge hivyo na saratani za matiti, takwimu zinaonyesha wengi wanaopata tatizo baada ya kutumia dawa hizo ni waliotumia kwa muda mrefu, jambo ambalo haliruhusiwi na wataalamu wa afya.
Dk Mjema anasema zipo njia nyingi za uzazi wa mpango ambazo ni za muda mfupi, muda mrefu na za kudumu na katika njia hizo kuna ambazo zinatumia homoni na zisizotumia.
"Katika njia ambazo zinatumia homoni katika muda huu mfupi ambao ni mwaka mmoja mpaka miwili, moja ya njia hizi tunakutana na vidonge vya uzazi wa mpango ambavyo vina homoni tofauti.
"Watu wanaotumia vidonge hivi wanaweza wakawa katika hali ya hatari ya kupata saratani na tatizo ni kwamba, wengi wanaotumia njia hizi hawaji kwa wataalamu wa afya kupata ushauri," anasema Dk Mjema.
"Shirika la Afya Duniani (WHO) limeweka vigezo, kwamba kila mtu kutokana na hali yake kuna aina fulani ya njia ya uzazi wa mpango inayomfaa, sasa tukija kwenye hivi vidonge mara nyingi hatupendi kuwapatia watu ambao wana presha kubwa, sukari na watu ambao wana hatari ya kugandisha damu katika mishipa."
Takwimu za ugonjwa
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2017, vifo vitokanavyo na saratani ya matiti vinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2030, huku idadi ya wagonjwa wapya ikitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 82.
Dk Marianne anasema changamoto kubwa ni kwamba, wagonjwa wengi wa saratani ya matiti wanakwenda hospitali wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo.
“Karibu asilimia 83 ya wagonjwa wa saratani ya matiti wanafika hospitali wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa, jambo ambalo ni hatari,” anasema.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha wengi kupoteza maisha kwa ugonjwa huo, akisema Hospitali ya KCMC imekuwa ikifanya upasuaji wa matiti kwa wagonjwa zaidi ya wanane kwa mwezi.
Anasema kwa kuchukua tahadhari madhubuti, inawezekana kuzuia ugonjwa huo usitokee na hivyo kuudhibiti.
Dk Marianne anasema katika hospitali hiyo wanapokea wagonjwa wapya wa saratani ya matiti kati ya wanne mpaka watano, huku kwa mwezi wakifanya upasuaji wa kuondoa matiti kwa wagonjwa wanane mpaka tisa.
“Tunapokea wagonjwa wengi wa saratani ya matiti na kwa wiki tunagundua wagonjwa wapya wanne hadi watano, hii kitu imetushtua sana na KCMC imeanza kupunguza tatizo hili kwa kufanya screen mapema na kujenga uelewa kwa wananchi juu ya ugonjwa huu.
“Pia, tumekuwa tukifanya upasuaji wa aina mbalimbali, lakini wengi wanafanyiwa wa kuondolewa matiti na kwa mwezi wanaweza kuwa wagonjwa wanane hadi tisa, inategemea,” anasema.
“Nimefanya utafiti wa saratani ya matiti hapa KCMC, nimegundua wanawake wengi wanafika hospitali wakati saratani imesambaa na kufikia hatua mbaya. Ukigundua mapema unaweza kupona na kupata maisha marefu,” anaeleza Dk Marianne.
Mkakati wa kudhibiti
Dk Marianne anasema moja ya mikakati waliyonayo ni kutoa elimu kwa wananchi kufanya uchunguzi mara kwa mara, wakibainika kupata matibabu mapema pindi kunapokuwa na viashiria au ugonjwa huo.
Anasema pia idara ya saratani katika hospitali hiyo, imeandaa programu ya kufanya uchunguzi wa saratani, ikiwamo ya matiti, ili kuwabaini wenye tatizo mapema kabla ya kufikia hatua mbaya.
“Idara ya upasuaji hapa KCMC imeandaa warsha kusaidia hospitali zilizopo kanda ya kaskazini, zikiwamo za wilaya na rufaa za mikoa na madaktari wanafundishwa namna ya kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti na kujenga uelewa, ili kufanya ukaguzi kwa wagonjwa na kusaidia kubaini tatizo mapema,” anasema.
Mtindo wa maisha watajwa
Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani Ocean Road, Emanuel Lugina anakiri kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa saratani ya matiti, hasa katika umri mdogo, hatua anayotaja imetokana na vitu viwili.
Anataja mabadiliko ya mfumo wa maisha akisema kwa miaka ya hivi karibuni, mfumo wa maisha kwa watu wengi umekuwa wa kisasa zaidi ukilinganisha na mfumo wa asili.
Dk Lugina anataja ulaji usiofaa, kutofanya kazi ngumu za kushughulisha mwili, vyakula vya mafuta, matumizi ya pombe kuongezeka hali inayosababisha kuwa wanene, hivyo kuwa moja ya viashiria vya magonjwa.
“Kingine inawezekana pia ni kutokana na uelewa, siku hizi mtu akishapata dalili tu haraka anaanza kuelewa huenda zikawa ni za saratani ya matiti, hivyo anakwenda hospitalini kwa haraka ikilinganishwa na zamani, sasa wanabainika wakiwa na umri mdogo,” anasema Dk Lugina.
Anasema kwa sasa kuna vipimo vingi vya kugundua mapema na vya kisasa zaidi ikilinganishwa na zamani ambapo wengi wanabainika mapema.
“Kwa hospitali ya Ocean Road tunapata zaidi ya wagonjwa 5,000 wa saratani kwa mwaka na kwa idadi hii karibu wagonjwa 600 wanabainika na saratani ya matiti, inayoshika nafasi ya pili kwa ukubwa ambapo kati yao asilimia 20 wanakuwa wa umri wa miaka 25 hadi 40, lakini asilimia kubwa ni miaka 40 na kuendelea,” anasema.
Anasema ili kuepuka kupata saratani za mapema ni vizuri kuzingatia mtindo bora wa maisha na kupima mara kwa mara ili kubaini viashiria.
“Tunapendekeza wanawake miaka 30 na kuendelea wawe na tabia ya kuchunguza afya zao kwa kukagua matiti ili kubaini viashiria mapema na wale wenye historia kwa familia kuugua saratani wafike hospitali kwa uchunguzi zaidi,” anasema.
Dk Lugina anasema ukubwa wa saratani hiyo ni kwa maeneo yote, lakini wanaoathirika zaidi ni wale wa kutoka mijini, lakini wa vijijini hufika katika hatua za mbele zaidi za ugonjwa, hali inayokuwa ngumu kutibika.
“Kwa sasa wanafika katika hatua ya tatu au nne ya ugonjwa ukilinganisha na zamani asilimia 90 walifika katika hatua ya nne ya ugonjwa,” anasema Dk Lugina.
Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani Hospitali ya Rufaa Mbeya, Irene Nguma anasema takwimu zinaonyesha wagonjwa wapya wa saratani ya matiti kwa Mbeya kwa kipindi cha mwaka 2022/23 ni 360.
Anasema kwa sasa kuna haja kwa mabinti ambao kuna mama zao, mama mdogo ama dada zao ambao katika nyakati mbalimbali waligundulika na saratani za matiti, ni vyema nao wakafika hospitali kwa ajili ya uchunguzi fatilizi kwa muda watakaopangiwa na daktari ili kama kuna tatizo kwao pia lipatiwe ufumbuzi mapema.
“Wajichunguze pia, ukiona mabadiliko yasiyo ya kawaida ama titi lina uvimbe ni vyema ufike hospitali kwa uchunguzi mapema zaidi.”
Kanda ya ziwa
Akizungumzia hali ya saratani ya matiti Kanda ya Ziwa, Mkuu wa Idara ya Saratani Bugando, Dk Nestory Masalu anasema tangu kuanzishwa kwa idara hiyo mwaka 2009, Bugando imehudumia watu 3,000 wenye saratani ya matiti.
Dk Masalu anasema kati yao wagonjwa 2,400 sawa na asilimia 80 ni wanawake wenye umri zaidi ya miaka 40, huku 60 wakiwa wanawake wenye umri chini ya miaka hiyo.
Anasema Bugando inabaini wastani wa wagonjwa wapya wa saratani ya matiti 60 kila mwaka, kati yao, 40 saratani yao hukutwa hatua ya tatu na nne ambazo ni ngumu kutibika, hivyo huishia kufanyiwa upasuaji wa kuondoa titi lililoharibika ama kupewa tiba shufaa ili kupunguza maumivu.
"Wagonjwa wengi tunaowaona wanakuwa katika hatua hiyo kwa sababu uelewa vijijini walipo bado ni mdogo, tunaomba hii taarifa ikiwafikia basi wananchi hasa wanawake waamke wakafanyiwe vipimo kujua iwapo wana dalili za saratani ili waanze matibabu ikiwa katika hatua za awali ambazo ni ya kwanza na pili," anasema.
Dk Masalu anasema mgonjwa mmoja kati ya wapya 60 wa saratani ya matiti wanaobainika kila mwaka hospitalini hapo ni mwanamume, huku akitaja sababu kuwa wanaume wana (vichochezi) homoni za kike na tishu za matiti na kudokeza kuwa saratani yao haitibiki kirahisi kwa kuwa inasambaa kwenye kifua.
Anasema saratani ya matiti ni ya pili kwa kuwatesa wanawake, ikitanguliwa na saratani ya shingo ya kizazi na kudokeza kuwa asilimia 25 ya wagonjwa wote wanaotibiwa hospitalini hapo wanasumbuliwa na saratani ya matiti.
"Ni saratani ambayo ikigundulika mapema inatibika kwa urahisi kwa sababu hata namna ya kuitambua haichukui muda mrefu, ndani ya siku mbili tunaweza kuwa na majibu yake," anasema.
Anataja sababu zinazochangia ugonjwa huo kuwa ni wanaowahi kuvunja ungo na kuchelewa kufikia ukomo wa hedhi (kuanzia miaka 45) kuwa wako hatarini kuugua saratani.
"Kama nyumbani kuna kioo unaweza kujipima kwa kukaza kiuno chako na kuangalia ukubwa wa matiti yako upoje. Kwa kawaida titi la kushoto ni kubwa kuliko kulia kwa sababu kushoto kuna moyo, lakini ikitokea ni kubwa kuliko kawaida hiyo ni dalili ya saratani," anasema.
Mtaalamu huyo anasema kawaida mtu mwenye saratani hupata uvimbe kwenye titi, tezi zinavimba, ngozi ya titi hubadilika, chuchu hurudi ndani, titi kutoa maji linapobinywa na kubadilika rangi.
"Kama una mwenza wako mwambie akusaidie kufanya uchunguzi huo kama huna kioo. Hakikisha unafanya kwa kuzingatia tarehe unazofanya, kama umefanya tarehe moja basi hata mwezi ujao ufanye tarehe kama hiyo, ukibaini dalili hizo wahi kituo cha afya kwa uchunguzi zaidi," anasema
Saratani inaambukiza
Dk Masalu, ambaye ni daktari bingwa mbobezi wa ugonjwa huo, anasema saratani inaambukiza kutoka kizazi kimoja kwenda kingine na kuonya kuwa mwanamke mwenye saratani ya matiti ana uwezekano mkubwa wa kujifungua mtoto mwenye saratani ya tezi dume.
Sambamba na hilo, alisema watu wenye wazazi ama ndugu wa karibu waliofariki kwa saratani wanatakiwa kufanya uchunguzi wa ugonjwa huo kila baada ya miaka miwili ili kutambua hali yao kiafya kabla ugonjwa huo haujafika hatua mbaya.
"Kama mama ana saratani ya matiti kuna uwezekano mkubwa zaidi kumwambukiza mtoto wake anapozaliwa. Vinasaba hivi vina tabia ya kuhama kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto," anasema
"Tunashauri wanawake wafike kwenye vituo vya afya kupimwa saratani, hasa wanapofikisha miaka 40. Ukifikisha umri huo gundua kwamba huna uvimbe kwenye titi ama kwapa katika kituo cha afya, utaambiwa urudi baada ya miaka miwili, akikuta kiashiria chochote utahitajika kupima kila mwaka," anasema.
Washuhudia
Jasmine Salum (33) anasema aligundulika kuwa na saratani ya matiti akiwa na miaka 29 n a alipokuwa akifanyiwa uchunguzi madaktari walimuuliza iwapo alikuwa akitumia dawa za uzazi wa mpango.
Anasema madaktari walimshauri aondolewe titi kwa kuwa umri wake ulikuwa bado mdogo, hivyo kuizuia isisambae kwa haraka.
Jasmine anaeleza alikubali na kupatiwa tiba hiyo, ikiwemo mionzi ambayo alisimulia ilikuwa ni tiba ghali lakini iliyokuwa na changamoto kubwa.
“Tangu nimemaliza matibabu ni mwaka na miezi kama sita,” anasema Jasmine ambaye kwa sasa anatoa ushauri kwa kinamama waliopata saratani ya matiti katika Taasisi ya Ocean Road.
Wanawake wengi wanapougua saratani katika umri mdogo, huachwa na wenza wao kama ilivyokuwa kwa Jacqueline Chammafwa (45), ambaye miaka mitano iliyopita aligundulika kuwa na saratani ya matiti.
Jacqueline alipata uvimbe uliokuwa ukitoa damu, ambao baada ya vipimo iligundulika kuwa ni saratani ya titi.
“Niligundulika ikiwa hatua ya pili, kwa hiyo wakaamua kuliondoa titi lote. Ninamshukuru Mungu nimemaliza matibabu ya mwanzo mwaka jana na naendelea vizuri. Hata hivyo, daktari aliniambia kuna uwezekano wa kuhamia sehemu nyingine kwa haraka,” anasema.
Maisha bila titi
“Ukikatwa ziwa kusema kweli ile hali inatia simanzi, ni mpaka mtu aikubali na kuizoea, inachukua muda ila kwa sababu ni matibabu, ukipata hilo tatizo bora ukatwe maana niliwaona ambao linaoza hadi linamwaga maji lenyewe,” anasema Jasmine.
Anasema uzuri ni kwamba, kwa sasa kuna maziwa ya bandia kwa hiyo angalau yanatoa uhuru na kujiamini anapokuwa barabarani.
Mtunza kumbukumbu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Kija Masare (34), alibainika kuwa na saratani ya titi iliyofika hatua ya tatu Novemba 2021 kabla kufanyiwa upasuaji wa kuliondoa.
Kija, mkazi wa jijini Mwanza, anasema pamoja na kuwa mtumishi katika taasisi ya afya, haikuwa rahisi kubaini dalili za ugonjwa huo mapema.
Naye Miriam Olomi, mkazi wa jijini Mbeya anasema kabla ya kugundulika kuwa na ugonjwa huo ilitokea uvimbe. Anasema mwaka 2018 akiwa na miaka 32, aliondolewa titi.
Imeandaliwa na Herieth Makwetta (Dar) Mgongo Kaitira (Mwanza), Flora Temba (Moshi) na Sadam Sadick (Mbeya)