Saudi Arabia yatoa shehena ya tende kwa wakimbizi Tanzania
Muktasari:
- Ufalme wa Saudi Arabia umetoa tani 36 za tende kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) kwa lengo wa kuwagawia wakimbizi waishio nchini.
Dar es Salaam. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) leo Julai 29, limepokea mchango wa tani za 36 za tende zenye thamani ya Dola za Kimarakeni 88,437 kutoka Ufalme ya Saudi Arabia kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wanaoishi mikoa ya Kusini-Magharibi mwa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na WFP leo imesema shehena hiyo ya tende itakuwa nyongeza kwa msaada wa chakula unaotolewa kila mwezi kwa zaidi ya watu 50,000.
Imewataja wafaidika wa chakula hicho kuwa pamoja na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na makundi mengine ya watu wanaoishi katika mazingira magumu katika kambi za Mtendeli, Nduta na Nyarugusu katika mkoa wa Kigoma.
Akizungumza katika sherehe ya makabidhiano ya msaada huo iliyofanyika katika Ubalozi wa Saudi Arabia jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi na Mwakilishi wa WFP Tanzania, Sarah Gordon-Gibson, mbali na kushuruku amesema mchango huo umekuja wakati ambao shirika hilo likiwa na ombwe katika ufadhili na hivyo kubaki na asilimia 68 tu ya utoaji wa chakula kwa wakimbizi nchini.
“WFP inakishukuru Kituo cha Msaada wa Binadamu na Usaidizi cha Mfalme Salman kwa msaada wake endelevu. Tunafurahi sana kwamba Falme ya Saudi Arabia bado ni mmoja wa wafadhili wetu tunaowathamini, wanaotusaidia kuwafikia watu wanaoishi katika mazingira magumu,” alisema Sarah.
Taarifa hiyo inasema wakimbizi wanaitegemea WFP pekee yake kukidhi mahitaji yao ya chakula.
“Wanapokea kikapu cha chakula chenye mchanganyiko wa vyakula mbalimbali ukiwemo unga maalum uliochanganywa soya na mahindi, kunde, chumvi, mafuta yanayotokana na mimea na unga wa mahindi uliotiwa virutubisho.
“Ugawaji wa tende hizi utafanyika mwezi huu na utawanufaisha walengwa zaidi ya 50,000 na kuwapatia virutubisho wanavyohitaji,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, WFP inasaidia zaidi ya wakimbizi 235,000 kutoka Burundi na Kongo waliopo katika kambi za Mtendeli, Nduta, na Nyarugusu mkoani Kigoma.
“Kati ya sasa na Juni, 2022, WFP ina upungufu wa fedha wa takriban Dola za Kimarekani milioni 29.6 kwa ajili ya shughuli zake zinazohusiana na wakimbizi.”