Sekta tano nchini kunufaika na mikopo NCBA
Muktasari:
- Watanzanzania wanaotoka sekta tano nchini ikiwemo usafirishaji milango wazi kunufaika na mikopo kutoka Benki ya NCBA itakayotunisha thamani na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
Dar es Salaam. Katika jitihada za kuchochea ukuaji uchumi nchini, sekta tano ikiwemo usafirishaji zinatarajiwa kunufaika na mikopo itakayotolewa na benki ya NCBA ili kuongeza thamani ya utendaji wa shughuli zao.
Sekta zingine ni za uzalishaji bidhaa, usambazaji, uagizaji wa mafuta, ujenzi na utalii ambazo kampuni za maeneo hayo zimekuwa zikilalamikia changamoto ya mitaji kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Claver Serumaga kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni mpya iliyopewa kina la 'Maisha ni Hesabu' mahususi kwa sekta hizo.
Amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuwafikia Watanzania waliopo kwenye sekta hizo na moja ya sifa mitaji yao inatakiwa kuanzia Sh5 bilioni pamoja na mnyororo wao mzima unaowazunguka.
"Tunazinduka kampeni yetu Maisha ni Hesabu kwa ajili ya wateja wetu wakubwa tukiendelea kusisitiza tumekuwa katika soko hili tukilenga kuongeza thamani ya maisha ya Watanzania kupitia biashara zao," alisema.
Amesema wananchi watarajie huduma nzuri kama wanaohitaji mkopo katika sekta ya usafirishaji basi wasaidiwa kuhakikisha wanakuwa na gari za kutosha ili kusafirisha bidhaa.
"Tunataka uzalishaji uongezeke, kama upo kwenye utalii tutakuwezesha tunakusaidia unakuwa na viundombinu ya kukufanya uwafikie watalii wengi zaidi," amesema.
"Leo tunazindua kampeni yetu ya ‘Maisha ni Hesabu ambayo ni kiungo muhimu kwenye mbinu mpya za kibiashara za NCBA Tanzania, zilizotengenezwa mahsusi kuendana na muunganiko wa Taasisi za NIC na CBA katika kutoa huduma bora zaidi za kibenki kwa wateja wetu," amesema.
Awali, Mkuu wa kitengo cha wafanyabiashara wakubwa, Godson Biyengo amesema katika dunia ya kibiashara, kila namba ina uzito wake, kila tarakimu inaelezea hadithi, huku akieleza kuwa benki hiyo imejikita kuwa chachu ya mafanikio kwa Watanzania.
"Muunganiko wetu ni ushahidi tosha wa uwepo wa imani, uadilifu, na ubunifu. Sisi sio benki tu, bali mwenza wako wa mafanikio katika kila hali," amesema.
Amesema lengo lao ni kutoa huduma za kifedha zenye ubunifu. Hivyo wanaamini katika kutumia nguvu ya teknolojia na kufanya huduma za kibenki zipatikane kwa urahisi kwa kila mmoja.
"Kama nyongeza katika huduma zetu za kidigitali, tumejikita katika kusaidia jamii inayotuzunguka. Miradi yetu endelevu sio tu ni katika kutimiza majukumu yetu kwa jamii, ila ushuhuda katika imani yetu ya kuleta mabadiliko chanya," amesema