Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kitakachokukuta ukimtelekeza mgonjwa wa akili

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Akili, Sura ya 98 (Marejeo ya 2023), mtu anayemtunza mgonjwa wa afya ya akili anatakiwa kuhakikisha anapata matibabu, uangalizi unaostahili na kulindwa dhidi ya ukatili, unyanyasaji au uzembe.



Dar es Salaam. Je, unajua kuwa kumtunza ndugu mwenye ugonjwa wa akili si suala la hiari au huruma ya kifamilia?

Kama hufahamu, basi tambua kuwa nchini Tanzania suala hili limepewa uzito wa kisheria, ambapo familia na walezi wana wajibu wa kuhakikisha mtu huyo anapata matibabu na huduma stahiki.

Kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Akili, Sura ya 98 (Marejeo ya 2023), mtu anayemtunza mgonjwa wa akili anatakiwa kuhakikisha anapata matibabu, uangalizi unaostahili na kulindwa dhidi ya ukatili, unyanyasaji au uzembe.

Sheria hiyo pia inazitaka taasisi za afya kushirikiana na familia ili kuhakikisha mgonjwa husika anaendelea na matibabu na huduma zinazohitajika, huku ikitambua kuwa familia ndiyo nguzo muhimu katika safari ya mgonjwa kuelekea kupona.

Licha ya uwepo wa sheria hiyo, bado yapo matukio ya watu wenye changamoto za afya ya akili kufungiwa ndani ya nyumba, kutengwa na jamii au kuachwa bila matibabu kutokana na imani potofu, hofu ya unyanyapaa au ukosefu wa uelewa kuhusu ugonjwa huo.

Akizungumzia hilo mwanasheria Jamal Abdulwakil amesema sheria hiyo inalenga kulinda haki, utu na usalama wa watu wenye changamoto za afya ya akili, ambao mara nyingi hukabiliwa na ubaguzi na kunyimwa huduma muhimu.

“Zipo familia ambazo huamua kumficha mgonjwa wa afya ya akili kwa hofu ya unyanyapaa, huku wengine wakiamini tatizo hilo linatokana na nguvu za kiroho au ushirikina badala ya ugonjwa unaohitaji matibabu.

"Itambulike kuwa hili si jambo la hiari tena. Pale familia inapomtelekeza mgonjwa, inamfungia ndani bila matibabu au inamzuia kupata huduma za afya kwa uzembe, inaweza kuwajibika kisheria," amesema Abdulwakil.

Ameeleza kuwa sheria inatambua kufanya ukatili, unyanyasaji au uzembe dhidi ya mtu mwenye changamoto ya afya ya akili ni kosa la jinai.

"Adhabu yake ni faini isiyopungua Sh500, 000, kifungo cha hadi mwaka mmoja au vyote kwa pamoja, kutegemeana na mazingira ya tukio na ushahidi uliopo," amesema.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, hatua ya kumfungia mgonjwa ndani ya nyumba kwa muda mrefu bila matibabu, kumtelekeza au kumzuia kufikishwa hospitalini inaweza kutafsiriwa kama uzembe au ukatili, endapo uchunguzi utaonyesha alinyimwa huduma muhimu.

Amesema badala ya kuficha wagonjwa majumbani, familia zinapaswa kushirikiana na wataalamu wa afya ili waweze kupata uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji unaohitajika.

Hata hivyo, Wakili Bashiri Yakub amesema wajibu huo hutegemea mazingira ya mtu husika, umri wake, mahusiano ya kifamilia pamoja na uwepo wa uangalizi maalumu wa kisheria.

Amesema kwa mtoto ambaye hajafikisha umri wa miaka 18, mzazi au mlezi wake ana wajibu wa kisheria wa kuhakikisha anapata uangalizi na huduma zinazohitajika, ikiwemo pale mtoto huyo anapokuwa na changamoto za afya ya akili.

"Kama ni mtoto chini ya miaka 18, huo ni wajibu wa mzazi au mlezi wake kuhakikisha anamwangalia na kumhudumia kwa kila kitu. Wajibu maana yake ni kitu cha lazima," amesema.

Hata hivyo, amesema hali hubadilika pale mtu anapokuwa amefikisha umri wa utu uzima, kwa kuwa si kila ndugu anakuwa na wajibu wa moja kwa moja wa kumhudumia mtu mzima mwenye matatizo hayo.

"Kama amepitisha umri wa miaka 18, huwa si wajibu moja kwa moja isipokuwa kuwepo mazingira maalumu yanayoweka wajibu huo kisheria," amesema.


Wanandoa wana wajibu

Kwa upande wa wanandoa, wakili huyo amesema ndoa huleta wajibu wa kisheria kati ya mume na mke, hivyo mmoja wao anapopata matatizo ya afya ya akili, mwenzake anaweza kuwa na wajibu wa kumwangalia.

"Kama ni mume ameoa, maana yake ni wajibu kwa mke wake. Na kama ni mke ameolewa, maana yake ni wajibu kwa mume wake," amesema.

Amesema wajibu huo unatokana na uhusiano wa ndoa ambao huweka majukumu mbalimbali kati ya wanandoa, ikiwemo kusaidiana katika changamoto zinazojitokeza ndani ya familia.


Wasimamizi wa mali wamo

Aidha, amesema kuna mazingira ambayo mtu anaweza kuwa na wajibu wa kumtunza mtu mwenye matatizo ya akili kutokana na usimamizi wa mali zake.

Ametoa mfano wa mzazi aliyefariki na kuacha mali kwa mtoto au ndugu mwenye changamoto ya afya ya akili, huku akimkabidhi mtu mwingine jukumu la kusimamia mali hizo.

"Kuna wazazi walifariki wakamwachia mtu mali, na mali hizo ziko chini ya mtu fulani. Huyo mtu amepewa wajibu wa kumwangalia kwa sababu pia anaangalia mali zake. Hata kama ni mtu mzima," amesema.

Amesema katika mazingira hayo, msimamizi wa mali hawezi kujitenga na wajibu wa kuhakikisha masilahi ya mwenye mali yanalindwa.

Wakili Yakub amesema sheria pia inaweza kuweka wajibu kwa mtu kupitia eneo la sheria linalojulikana kama Tort (sheria ya makosa ya kiraia), hasa pale mtu anapokuwa amepewa jukumu la kumwangalia mwingine.

"Moja ya wajibu wake ni kumwangalia. Huyu lazima amwangalie. Ni wajibu wa kisheria na akishindwa anaweza kuchukuliwa hatua," amesema.

Akizungumzia hilo mkazi wa Kimara, Neema Mwakalobo amesema familia nyingi bado zinaogopa kuwapeleka hospitalini ndugu wenye matatizo ya akili kwa kuhofia unyanyapaa kutoka kwa jamii.

"Watu wengi wanaogopa kuitwa familia ya wenye wazimu, ndiyo maana wengine huwaficha wagonjwa ndani ya nyumba. Lakini tukipata elimu zaidi tutaelewa kuwa hawa ni wagonjwa kama walivyo wagonjwa wengine na wanahitaji matibabu," amesema.

Kwa upande wake Juma Mshana, mkazi wa Mbagala, amesema alikuwa hafahamu kuwa sheria inawawajibisha familia kuhakikisha wagonjwa wa akili wanapata matibabu.

"Nimekuwa nikidhani ni jukumu la hiari la familia. Sasa nikijua kuwa sheria inalitambua suala hili, naamini itawafanya watu wengi kubadili mtazamo na kuwahi kuwapeleka wagonjwa hospitalini badala ya kuwafungia ndani," amesema.


Wapatiwe matibabu

Akizungumzia umuhimu wa matibabu ya mapema, daktari wa magonjwa ya akili Dk Mohamed Said amesema magonjwa mengi ya afya ya akili yanatibika au kudhibitika iwapo mgonjwa atafikishwa hospitalini kwa wakati.

"Watu wengi bado wanaamini kuwa matatizo ya afya ya akili hayawezi kutibiwa, jambo ambalo si kweli. Wagonjwa wengi wanaopata matibabu mapema huendelea na maisha yao ya kawaida, kufanya kazi, kusoma na kushiriki shughuli za kijamii kama watu wengine," amesema.

Amesema kuchelewesha matibabu kunaweza kufanya ugonjwa kuwa mgumu zaidi kutibika na kuongeza hatari ya mgonjwa kujidhuru, kuwadhuru wengine au kudhurika kutokana na mazingira yanayomzunguka.

"Kinachohitajika ni kumfikisha mgonjwa katika kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu. Familia inapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, si chanzo cha mateso kwa mgonjwa," amesema Dk Said.

Daktari huyo ameongeza kuwa wagonjwa wengi wanaohudhuria kliniki na kutumia dawa kwa kufuata maelekezo ya wataalamu, hupata nafuu na kuendelea na shughuli zao za kila siku, jambo linalodhihirisha kuwa afya ya akili inaweza kudhibitiwa kama ilivyo magonjwa mengine.

Kwa upande wake, mwanasaikolojia Suzan Malya amesema unyanyapaa unaohusishwa na afya ya akili bado ni miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya wagonjwa kukosa huduma kwa wakati.

"Wakati mwingine familia huamua kumficha mgonjwa kwa kuhofia aibu au maneno ya jamii. Lakini kufanya hivyo kunamnyima haki ya kupata matibabu na kunachelewesha kupona kwake," amesema Suzan.

Ameeleza kuwa mtu mwenye changamoto za afya ya akili anahitaji mazingira salama, upendo, uelewa na usaidizi wa karibu kutoka kwa familia pamoja na jamii ili kuongeza nafasi ya kupona.

"Afya ya akili ni sehemu ya afya kwa ujumla. Kama ilivyo kwa magonjwa mengine, mgonjwa anahitaji matibabu, si kulaumiwa, kufichwa au kutengwa," amesema.

Mtaalamu huyo amesisitiza jamii inapaswa kuachana na dhana kwamba kila mtu mwenye changamoto ya afya ya akili ni mkatili au hawezi kupona, akieleza kuwa imani hizo zimekuwa zikiwafanya wagonjwa wengi kuchelewa kupata huduma za kitaalamu.