Selasini: Lowassa katuacha kama alivyotukuta

Mbunge wa Rombo (chadema), Joseph Selasini

Muktasari:

  • Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amesema kuondoka kwa Lowassa upinzani hakuwezi kuwa pigo Chadema na kikubwa ni kwamba amewacha kama alivyowakuta.

 

Moshi. Mbunge wa Rombo (chadema), Joseph Selasini amesema kuondoka kwa Edward Lowassa Chadema hakuwezi kuwa pigo kwa chama hicho kwani amewaacha kama alivyowakuta.

Selasini ambaye amelazwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, amesema Lowassa kurudi CCMni dhahiri kwamba ameenda kupumzika akidai kuwa siasa za mikikimikiki haziwezi.

"Tunamtakia mapumziko mema, sisi tutasonga mbele hatupoi, hatupumziki na hatuogopi mpaka kieleweke," amesema Selasini.

Ameongeza, "kwa wenzetu wa CCM wanaendelea kuudhihirishia umma kwamba bila Chadema hawawezi kuwa na amani na wala kuwa na viongozi imara, daima tumekua chuo cha kuwaandalia viongozi na kuwapa tiba sahihi wale waliofikiri kwao wamechuja na hatimaye kuwarejesha kwa gharama kubwa," amesema.

"CCM kuwaza kuua upinzani au kuwatesa viongozi wa upinzani kama wanavyofanya sasa waelewe tu bila upinzani CCM hakuna kitu zaidi ya majungu, fitna na makundi yanayowatafuna kila kukicha,"amesema Selasini.

Amesema Chadema  hawatasahau mchango wake ndani ya chama hicho na kamwe hawatamdharau.

"Lowassa alikuja kwetu baada ya kudharauliwa, kubezwa na kukataliwa na chama ambacho alikitumikia kwa muda mrefu, tulimchukua tukijua alikua na mchango katika kukuza demokrasia nchini na kwa maendeleo ya Taifa hili, ni dhahiri upo mchango wake ambao aliongeza katika chama chetu na hatuwezi kuudharau," amesema Selasini.

Selasini pia amesema anamtakia kila la kheri na kusema bado wanaamini mabadiliko yanatoka upinzani.