Serengeti Festival ni bandika bandua mpaka asubuhi
Muktasari:
Tamasha la Serengeti Festival limeanza leo Jumamosi Desemba 26, 2020 katika viwanja vya Uhuru, Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Tamasha la Serengeti Festival limeanza leo Jumamosi Desemba 26, 2020 katika viwanja vya Uhuru, Dar es Salaam.
Tamasha hilo linahusisha wasanii zaidi ya 60 ambao watatumbuiza jukwaa moja, wakiwemo wasanii wa muziki wa kizazi kipya waliotamba miaka ya nyuma, vikundi vya ngoma za asili, sarakasi na michezo ya kuigiza.
Katika ufunguzi jukwaa la Serengeti Festival lilishambuliwa na kikundi cha ngoma za asili cha Disciples Flow Choir ambalo lilitumia dakika 25 kutoa burudani.
Ofisa sanaa mwandamizi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Abel Ndaga ameieleza Mwananchi Digital kuwa, vikundi 13 vya ngoma vitatumbuiza mpaka saa 1 jioni kisha wasanii wa muziki wa kizazi kipya watapewa nafasi.
"Vikundi vitatumbuiza mpaka saa moja, kisha Bongofleva ndo itaanza na msanii wa kwanza kupanda atakuwa Nini. Kimsingi watatumbuiza mpaka asubuhi, " amesema.
Tamasha hilo litafanyika kwa siku mbili katika mikoa miwili tofauti. Leo ni Dar ea Salaam na kesho Desemba 27 itakuwa zamu ya wakazi wa Bagamoyo mkoani Pwani.
Wilayani Bagamoyo tamasha hilo litafanyika katika viwanja vya Tasuba.
Imeandikwa na Kelvin Kagambo