Serikali, EU zajipanga kuendeleza kilimo
Muktasari:
Mafanikio yamepatikana katika kupanuka kwa kilimo na upatikanaji wa masoko kwa wakulima wadogo.
Wakati awamu ya pili ya mpango wa kusaidia biashara na kilimo (TASP II) ukielekea ukingoni, Serikali inajipanga kutekeleza nyingine ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
TASP II inayotekelezwa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) ambao umetoa Euro 15 milioni (Sh39 bilioni) kuanzia mwaka 2012 unafikia ukingoni mwakani, huku mafanikio yakionekana zaidi katika mazao ya chai, kahawa mbogamboga na matunda.
Mkuu wa kitengo cha ushirikiano cha EU, Jose Correia-Nunes amesema mafanikio yaliyodhihirika ni pamoja na kupanuka kwa kilimo na upatikanaji wa masoko kwa wakulima wadogo na kusaidia taasisi za utafiti kupata mbegu ambazo zinastahimili magonjwa yaliyokuwa yakiwasumbua wakulima kwa muda mrefu.
“Tunashirikiana kwa karibu na Serikali ili kubaini mpango utakaofuata baada ya TASP II. Tathmini ya kina imefanyika ili kuona fursa za kuendeleza mnyororo wa thamani, kuzalisha ajira, kukuza kipato na kuondoa umasikini. Tunafanya haya kwa kuzingatia vipaumbele vya mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo,” amesema Correia-Nunes alipozungumza na gazeti hili.
Ingawa mpango mpya bado haujaidhinishwa, lakini uzoefu wa TASP II unaonyesha chai, kahawa, mbogamboga na matunda ni miongoni mwa mazao yaliyoendelezwa zaidi hivyo kuwanufaisha wakulima.
Ofisa kutoka ofisi ya muidhinishaji mkuu wa fedha za EU katika Wizara ya Fedha na Mipango inayosimamia TASP II, Jonathan Mpuya amesema Serikali inaandaa mapendekezo ya mpango ujao.
Amesema miongoni mwa mafanikio yaliyojitokeza ni mabadiliko hasa ya ushiriki. “Kuna maeneo, chai na kahawa kwa mfano, ilikuwa inalimwa na wakulima wakubwa tu lakini sasa hata mtu mmoja mmoja analima. Programu imesaidia kupata mbegu bora ambazo zinastahamili magonjwa.”
Pia, ametoa mfano wa mikoa ya Mtwara na Lindi ambayo ilikuwa inaagiza mboga za majani na matunda kutoka mikoa mingine lakini sasa inazalisha kiasi cha kutosheleza mahitaji hata kutafuta masoko nje ya Tanzania.
“Hata hivyo, changamoto ni kwenye uzalishaji wa mbegu na hasa za kahawa na chai, hakuna kampuni binafsi zinazozalisha mbegu kwa wingi ili wakulima wadogo wazipate kwa urahisi. Usambazaji wa mbegu hizi bora ni fursa ambayo kampuni binafsi za kilimo hazijaiona,” amesema.