Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali: Hali ya usalama wa mpaka wa Msumbiji haitabiriki

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024 leo. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga (JKT) imewasilisha bajeti yake kwa mwaka 2023/24 huku ikizungumzia kuhusu hali ya mipaka ya Tanzania na nchi za jirani.

Dodoma. Serikali imesema hali ya usalama katika mpaka wa kati ya Tanzania na Msumbiji ni ya wastani na isiyotabirika kutokana na uwepo wa kundi la kigaidi la Ansar Al Sunna Wal Jammah (AASWJ).

Kundi hilo lipo Kaskazini mwa Msumbiji, katika maeneo ya mwambao na mpaka mkabala na Mkoa wa Mtwara.

Kundi hilo limeweka ngome katika Wilaya ya Macomia, Cabo Delgado na limeendelea kuhatarisha amani na usalama katika eneo hilo.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Innocent Bashungwa ameyasema hayo leo Mei 24, 2023 wakati akiwasilisha bungeni bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24.

Aidha, Bashungwa amesema kundi hilo limebuni mbinu isiyotumia nguvu (Non – Violence Radicalization) ya kuwafikia na kuwalingania washirika wapya kwa njia ya amani.

“Vilevile, limeendelea kujiimarisha kwa kupata wafuasi na silaha kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo kwa kupora kutoka vikundi vya ulinzi na usalama nchini Msumbiji,”amesema.

Amesema hatua zilizochukuliwa kukabiliana na hali hiyo ni pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji kwenye nyanja za mafunzo, kubadilishana taarifa na kufanya operesheni za kijeshi za pamoja.

Kuhusu mpaka wa Tanzania na Kenya, Bashungwa amesema ipo changamoto ya kuharibiwa kwa alama za mpaka na wahamiaji haramu katika Mkoa wa Tanga ambao wanahatarisha usalama wa nchi, kwasababu baadhi yao hujihusisha na vitendo vya kihalifu.

Ametaja changamoto nyingine ni kutotambulika kwa mpaka wa Tanzania na nchi ya Kenya katika eneo la Bahari ya Hindi, hasa kwa wananchi wa kawaida. “Hali hiyo imechangia baadhi ya wavuvi wa Tanzania kukamatwa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Kenya kwa kosa la kuvuka mpaka,”amesema.

Amesema kazi ya kuimarisha mpaka huo inayotekelezwa na timu ya wataalamu kutoka Tanzania na Kenya inaendelea vizuri, ambapo kwa sasa kazi hiyo inaendelea kati ya eneo la Namanga na Ziwa Jipe.