Serikali kubeba gharama mazishi ya watano wa familia moja waliozama bwawani
Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro wakishirikiana na wananchi kuushusha mwili wa mmoja wa waliofariki dunia kufuatia ajali ya mtumbwi iliyotokea katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, Kata ya Arusha Chini wilayani Moshi.
Muktasari:
- Ajali hiyo ilitokea Julai 23, 2026, wakati waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kijiji cha Chemchemi wilayani Moshi walipokuwa wakielekea kanisani Kitongoji cha Mikocheni 'B' kuhudhuria kongamano la Idara ya Wanawake.
Moshi. Serikali imeahidi kugharamia majeneza na usafiri wa mazishi ya watu watano wa familia moja waliopoteza maisha baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupinduka katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Ahadi hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alipofika kutoa pole kwa familia ya wafiwa katika Kijiji cha Chemchemi kilichopo Kata ya Arusha Chini.
Ajali hiyo ilitokea Julai 23, 2026, wakati waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Kijiji cha Chemchemi walipokuwa wakielekea kanisani katika Kitongoji cha Mikocheni ‘B’ kuhudhuria kongamano la Idara ya Wanawake.
Katika ajali hiyo, wanawake wawili na watoto watatu wa familia moja walipoteza maisha huku watu wanane wakinusurika. Waliofariki dunia wametajwa kuwa ni Maria Andrea, Yustina Lazaro, Raima Andrea, Happy Andrea na Kelvini Andrea.
Akizungumza na familia hiyo, Mnzava amesema Serikali imeguswa na msiba huo na imeamua kupokea maombi ya familia ya kupata msaada wa maandalizi ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika Jumatatu, Julai 27, 2026.
“Tumelichukua hilo na tutalifanyia kazi. Serikali itaandaa usafiri, lakini pia itabeba gharama za majeneza yote matano kama sehemu ya faraja na namna tulivyoguswa na msiba huu uliowakuta,” amesema Mnzava.
Pamoja na kutoa pole, Mnzava ametumia fursa hiyo kuwatahadharisha wananchi wanaoishi na kufanya shughuli zao kandokando ya Bwawa la Nyumba ya Mungu kuchukua tahadhari kutokana na hali ya hewa kutokuwa salama.
Amesema Mamlaka ya Hali ya Hewa na uongozi wa eneo hilo umekuwa ukitahadharisha mara kwa mara kuhusu upepo mkali na kuongezeka kwa kina cha maji.
“Wananchi wanapaswa kuepuka shughuli zisizo za lazima bwawani kwa kipindi hiki, na wavuvi pia wanatakiwa kuzingatia kanuni na tahadhari zote wanapokuwa majini,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi, aliyefika eneo hilo kuungana na Serikali, amesema msiba huo umeumiza jamii nzima kutokana na waliofariki kuwa katika safari ya kiimani.
Makoi amechangia vyakula na vinywaji ikiwamo katoni 50 za maji, lita 20 za mafuta ya kupikia, kilo 50 za mchele na kreti 20 za soda, huku diwani wa eneo hilo,Leonard Waziri akichangia kilo 30 za mchele kusaidia msiba huo.
Kwa niaba ya wafiwa na wanakijiji, mzee Lawrence Ngonyani ambaye amepoteza mwali na wajukuu watatu, ameishukuru Serikali, wananchi na viongozi wa jimbo hilo kwa kujitokeza kwa pamoja kuwafariji.
“Sijawahi kuona Mkuu wa Wilaya, Mbunge na Mkurugenzi wakifuatana kwa pamoja kuja kutoa pole kijijini kwetu. Hili ni tukio la kwanza na limetupa faraja kubwa sana katika kipindi hiki kigumu,” amesema Ngonyani.
Miili ya marehemu kwa sasa imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi mjini Moshi.