Serikali kugharamia msiba watu 10 waliofariki ajalini Kilimanjaro

Muktasari:
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema Serikali mkoani humo itabeba msiba wa watu 10, waliopoteza maisha katika eneo la Dachikona, Kijiji cha Wiri, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Siha. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema Serikali mkoani humo, itabeba gharama za msiba wa watu 10; waliopoteza maisha katika eneo la Dachikona, Kijiji cha Wiri, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Babu ameyasema hayo leo Agosti 18 mara baada ya kumtembelea majeruhi mmoja aliyenusurika katika ajali hiyo ambaye amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Siha.
Babu amesema katika ajali hiyo iliyoua watu 10, sita ni wanawake na wanne ni wanaume huku majeruhi akiwa ni mmoja.

"Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa pole na amepokea kwa mshituko mkubwa msiba huu mzito wa Watanzania 10 na sisi serikali ya mkoa kwa maelekezo tutaubeba msiba huu na kuwahudumia wenzetu waliopoteza maisha,” amesema.
"Kwa hiyo nimewawelekeza wakuu wa Wilaya ya Siha na Hai ili wale wananchi tujue wanatoka katika hizo wilaya lakini kuna mmoja nimeambiwa anatoka Tabora naye pia tutamhudmia kwa ajili ya kumpeleka hadi Tabora. Kuna mmoja ambaye hajatambuliwa na ndugu zake jitihada zinafanyika ili aweze kutambuliwa na akishatambuiliwa anatoka maeneo gani katika mkoa wetu wa Kilimanjaro naye tutamhudmia," amesema RC Babu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Migwa amesema ajali hiyo imetokea saa sita mchana na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni gari aina ya Kirikuu kupoteza mwelekeo na kwenda kugongana uso kwa uso na lori la polisi.
"Ni kweli ajali hiyo imetokea saa sita mchana Wilaya ya Siha, dereva wa Kirikuu wakati anakuja alikamatwa mara ya kwanza kwa kosa la kubeba abiria kinyume na utaratibu kwasababu Kirikuu ni kwa ajili ya mizigo, akapigwa faini, Jambo la kushangaza mbele akawa amebeba tena watu wengine wakati anakwenda akakutana na gari ya polisi wakati inashuka akahama kutoka upande wake anaelekea upande wa lori la polisi na kupelekea kugongana uso kwa uso na kupelekea vifo vya watu 10," amesema.
"Tunaendelea kusisitiza watu waache matumizi mabaya ya magari, huyu mtu kapigwa faini kwa kosa la kubeba abiria bado unapoachana na askari unabeba tena, sasa utii wa sheria bila shuruti hauhitaji mpaka uonekane na laiti pengine angeweza kutii, haya yasingeweza kutokea na mimi nisisitize ufuatiliaji utakuwepo na tunaendelea kufuatilia kwenye minada ili tuhakikishe magari yote yanayobeba abiria yanafuata utaratibu kwa mujibu wa yalivyotengenezwa," amesema RPC Maigwa.
Miili ya watu hao 10 imehifadhiwa katika Hospitali ya Kibong'oto kwa taratibu za mazishi.