Serikali kujenga bandari ya uvuvi Kilwa

Muktasari:

Serikali imesema imepanga kujenga bandari ya uvuvi ya kisasa Kilwa ili kusaidia sekta ya uvuvi kukua na kufanikisha uchumi wa buluu.

Kilwa. Serikali imesema imepanga kujenga bandari ya uvuvi ya kisasa Kilwa ili kusaidia sekta ya uvuvi kukua na kufanikisha uchumi wa buluu.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 26, 2022 na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete alipokua akizungumza katika maadhimisho ya siku ya usafiri wa maji duniani ambayo kitaifa imefanyika mkoani Lindi.

 Mwakibete amesema sababu ya kujenga bandari wilani humo ni kutokana na upatikanaji wa samaki kwa wingi samaki na kina cha maji kuwa chini.

"Tumekuwa tukiimba wimbo ule wa uchumi wa buluu sasa ili ufanikiwe ni lazima tuwe na vyombo muhimu vya kufanya ufanikiwe, kwa hakika uchumi wa nchi unakwenda kuimarika lakini na tunakwenda kuandika historia," amesema.

Pia, Mwakibete amebainisha kuwa Serikali ina lengo la kununua au kujenga meli nane ambazo nne kati ya hizo zitapelekwa Tanzania visiwani na nyingine zitabaki Tanzania Bara lengo likiwa ni kuimarisha uchumi wa nchi.

Akizungumzia miradi hiyo inatarajiwa kukamilika lini, Mwakibete amesema kinachosubiriwa hivi sasa ni ukusanyaji wa sampuli za udongo wa majini na nchi kavu kisha kuwa na upembuzi yakinifu na baada ya hapo zabuni itatangazwa ndipo kazi ianze kwa kuwa mikakati yake ipo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23.