Serikali kunoa mawakili 600 Dodoma

Wakili Mkuu wa Serikali Dk Boniphace Luhende  akizungumza na wanahabari jijini Dodoma

Muktasari:

  • Mafunzo hayo yatafanyika kuanzia Juni 6 hadi 8, 2023 ambapo mawakili wa serikali wametakiwa kuripoti Dodoma ifikapo Juni 5, 2023

Dodoma. Zaidi ya Mawakili 600 wa Serikali wanatarajia kukutana jijini Dodoma kwa ajili ya mafunzo ya siku tatu ili kuwanoa katika masuala mbalimbali ikiwemo suala la mafuta na gesi.

Kauli hiyo hiyo iletolewa jijini Dodoma leo Alhamisi Juni Mosi, 2023 na Wakili Mkuu wa Serikali Dk Boniface Luhende wakati akielezea juu ya maadhimisho ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo.

Mafunzo hayo yatafanyika kuanzia Juni 6 hadi 8, 2023 ambapo mawakili wa serikali wametakiwa kuripoti Dodoma ifikapo Juni 5, 2023.

Dk Luhende amesema kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajia kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambayo yataambatana na maonyesho yanayobeba kauli mbiu tumetoka wapi, tulipo na tunapokwenda.

Wakili Mkuu amesema wamewaandaa watoa mada wazuri kutoka jopo la majaji wabobezi na wanasheria wengine ili kuwanoa mawakili katika kutambua mambo ya gesi, usuluhishi na migogoro katika siku hizo tatu Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini hapa.

“Mambo mengi tutayaeleza siku hiyo ikiwemo kesi ngapi zilizofanikiwa kupitia ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali lakini Watanzania watambue kuwa kwenye kesi tunazokwenda kusuluhisha huwa tunaitwa kama wenye kesi wengine,” amesema Dk Luhende.

Akizungumzia kuhusu matukio ya kushindwa mitihani kwa wanafunzi wa shule kuu ya sheria, alisema Serikali inakitegemea chuo hicho kuzalisha mawakili wa serikali kama ilivyo kwa wale wanaofanya kazi kwa kujitegemea huku akisisitiza kuwa wakati mwingine Serikali huwa na mawakili wazuri zaidi.

Hata hivyo Wakili Mkuu amesema kuwa kuna mambo mengi ambayo Ofisi ya Wakili Mkuu imeyafanya lakini ni mapema kueleza kwani kila kitu kitazungumzwa kwenye mafunzo hayo.

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ilianzishwa februari 13, 2018 kupitia hati idhini ya Rais iliyotolewa kwa mujibu wa ibara 36(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.