Serikali kuongeza kasi matumizi ya LPG

Serikali kuongeza kasi matumizi ya LPG

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema itahakikisha inaongeza kasi ya matumizi ya gesi ya kupikia (LPG) kwa lengo la kupunguza athari za mazingira na afya za watumiaji wa mkaa na kuni hususani akina mama.

Akizungumza leo Alhamisi, Agosti 4, 2022 wakati wa Kongamano la Kimataifa la Nishati 2022, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Modestus Lumato amesema mamlaka hiyo inaandaa mpango wa kuanzisha utaratibu wa uagizaji wa pamoja wa gesi ya LPG hatua itakayoongeza kiwango cha matumizi na kupunguza gharama za manunuzi

“Tunahitaji uagizaji wa pamoja ili kufikia angalau tani 20,000 badala ya tani tani 5,000 zinazoingia bandarini kila baada ya siku saba,” alisema Lumato katika wasilisho lake mbele ya ugeni huo.

“Matumizi ya kila mtanzania kwa sasa ni wastani wa kilo 2.3 kila siku kutokana na tani 136,652 zilizotumika mwaka jana nchini. Hadi Juni mwaka jana asilimia 52 walitumia mitungi ya kilo sita, na asilimia 33 wakitumia mitungi ya kilo 15, matumizi makubwa ni mijini na wialayani.”

Jana katika wasilisho lake, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema serikali imeweka mkakati huo  eneo la nishati safi ya kupikia ni muhimu na linagusa sehemu kubwa ya maslahi ya watanzania. “Itakuwa ni vyema sana tukijadili eneo hili kwa kuwa lineonekana kuwa sehemu ndogo sana ya mijadala.”