Serikali kupanua mkongo wa Taifa kuboresha mawasiliano
Muktasari:
- Shirika la Mawasiliano nchini (TTCL) limeanza kupanua mkongo wa Taifa na kuongezea uwezo wake ili kufikisha mawasiliano pande zote nchini kwa gharama nafuu.
Mwanza. Wakati baadhi ya wananchi wakilalamikia gharama za vifurushi vya intaneti kuwa juu, Shirika la Mawasiliano nchini (TTCL) limeanza kupanua mkongo wa Taifa na kuuongezea uwezo wake ili kufikisha mawasiliano pande zote nchini kwa gharama nafuu.
Wakizungumza leo wakazi wa mkoani Mwanza wamesema bei za vifurushi vya intaneti zinawaumiza hasa wajasiriamali wanaofanya shughuli zao mitandaoni.
“Mimi nauza mapambo ya nyumbani kwenye mitandao ya kijamii, natangaza napata wateja kule lakini inanigharimu sana maana nikinunua kifurushi cha Sh3,000 kwa wiki kinaisha ndani ya siku moja kwahiyo inakuwa gharama sana na kumbuka wakati mwingine hupati wateja,”amesema Verediana Japhet
Haruna Msekwa ameiomba Serikali kuangalia namna ya kurahisisha gharama za intaneti akidai ulimwengu unaamia kidijitali ambapo bila uwepo wa mtandao wa uhakika na rahisi watakao baki nyuma ni watu wenye hali duni.
Leo Alhamisi Aprili 4, 2024 wakati wa Iftar iliyoandaliwa na TTCL katika hoteli ya Malaika jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Zuhura Muro amesema Serikali imesikia kilio cha bando cha wananchi na tayari inahakikisha pande zote nchini zinakuwa na mawasiliano ya uhakika na rahisi.
“Kuna Wilaya ambazo hazijafikiwa na mkongo tumejipanga vizuri. Ninavozungumza hapa kuna project managers (meneja miradi) zaidi ya wanane wapo field tunapanua mkongo wa taifa kwa kuuongezea uwezo ili uweze kukuza uchumi wetu kwa sababu hakuna mapinduzi ya kidijiti bila TTCL kwa muktadha huo lazima tuupanue mkongo tuweze kufikisha mawasiliano katika pande zote za nchi yetu,
“Pamoja na kuongeza nguvu kwenye kituo chetu cha kuweka data ili kiweze kuwahudumia watanzania wote…miundombinu ya TTCL iliyopo katika mikoa mbalimbali tunaibadilisha yote itakuwa ni data center (vituo cha data),”amesema
Muro amesema wanahakikisha mawasiliano yanapatikana kwa kiwango cha hali ya juu, cha ubora, kwa uraisi lakini pia yanapatikana kwa bei ambayo wananchi wanaiweza kwa kuimarisha miundombinu ili kushusha gharama.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Peter Ulanga amewataka waumini wa dini hiyo kufanya dua, kusamehana katika mwezi huu wa Ramadhani akidai kama shirika wametumia dhifa hiyo kukumbushana masuala mbalimbali ikiwemo ya kiutendaji.
“Shirika linaendelea na kazi yake kubwa ikiwemo ya kusimamia kwa weledi miundombinu ya mawasiliano ya kimkakati ikiwemo mkongo wa taifa na kituo cha kuhifadhi data,”amesema
Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Massala amesema dhifa ya kufuturisha ni ibada inayoleta umoja ndani ya jamii na faida za kiimani huku.