Kauli ya Mchechu CAG akianika utendaji wa mashirika ya umma

Muktasari:

  • Ni kwa mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yaliyopata hasara

Dar es Salaam. Baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuibua mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yaliyopata hasara, Serikali imetoa mwelekeo namna ya kushughulika nayo.

Mashirika yaliyoibuliwa na ripoti ya CAG iliyotolewa jana Machi 28, 2024 kuwa ni Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kampuni ya Uwekezaji TanOil na Shirika la Posta Tanzania.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Machi 29, 2024, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema watafanya uchambuzi wa kina na pale itakapohitajika kuchukua hatua watachukua.

Rais Samia akipokea ripoti ya CAG muda huu

“Pale ambapo itatuhitaji kuchukua hatua tutachukua, pale ambapo itatuhitaji kulisaidia shirika tutalisaidia mtaji au kile walichokwama,” amesema.

Mchechu ametoa mfano wa TTCL ambalo limepata hasara lakini lilisogea kutoka hasara ya Sh19.23 bilioni hadi chini ya bilioni moja, akisema wataangalia mwenendo wa mashirika yaliyopata hasara kama yanabebeka.

Amesema kwa mwaka huu, mashirika mengi yamejitajihidi ikilinganishwa na mwaka 2023, akiahidi watakuwa wakifanya uchambuzi kubaini mashirika ya kuyaunganisha au kuyafuta.

“Kila mara tutakuwa tunafanya uchambuzi, kuna mwaka tutafanya uchambuzi na utatupa majibu ama kufuta au kuyaunganisha; au uchambuzi utatuambia tatizo liko hapa ukilitatua hii kampuni ni nzuri na tutafanya hivyo,” amesema Mchechu.

Mwanzo mwisho CAG Kichere akisoma ripoti ya ukaguzi, ATCL,TTCL, TRC, MSD, TANOIL watajwa

Ndani ya Ripoti

CAG, Charles Kichere katika ripoti amesema ATCL ilipata hasara ya Sh56.64 bilioni mwaka 2022/23 kutoka hasara ya Sh35.24 ya mwaka uliopita.

Hasara hiyo imepatikana i licha ya ruzuku iliyotolewa na Serikali kwa ATCL ya Sh31.5 bilioni.

Kwa upande wa TRC, lilipata hasara ya Sh100.70 bilioni kutoka Sh190.01bilioni mwaka uliotangulia, TTCL imepata hasara ya Sh894 milioni kutoka Sh19.23 bilioni.

Kampuni ya Uwekezaji ya TanOil ilipata hasara ya Sh76.56 bilioni ikiwa ni ongezeko la Sh68.72 bilioni kutoka hasara ya 7.84 bilioni ya mwaka uliopita.

Hasara hii imetokana na kile CAG alichoeleza ni TanOil kushindwa kuwalipa wauzaji.

Jambo lingine ni gharama kubwa ya kuhifadhi mafuta ikiwa ni Sh12.9 bilioni ikilinganishwa na Sh6.1 bilioni waliyotumia mwaka jana.

Shirika la Posta lilipata hasara ya Sh1.34 bilioni ikilinganishwa na faida ya Sh16.21 bilioni kwa mwaka uliopita baada ya mauzo ya mali ya shirika.

Kwa nini hasara ATCL

Jumatano Machi 27, 2024 akichangia mjadala wa Mwananchi X Space ukiwa na mada isemayo, “kwa kiasi gani kununuliwa kwa ndege za ATCL kunapunguza changamoto katika usafiri wa anga nchini,” Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema lengo la ATCL ni kuunganisha Tanzania.

Ameeleza baadhi ya vituo wanavyoenda hivi sasa si kuwa vinawalipa bali kwa siku zijazo vitakuwa na faida kubwa na kwamba, faida katika mashirika mengi ya ndege duniani ni ndogo si tu kwa ATCL.

Matindi alisema mchakato ni mrefu hadi kuanza kupata faida na suala hilo ni la kuangalia kwa umakini zaidi.

“Soko la ndani limebadilisha fikra za Watanzania na mwonekano wa soko la anga, natumaini mwakani tutaongeza abiria wengi zaidi. Sikutarajia kama litakuwa hivi, tumejitahidi kuongeza ubunifu kwa kuangalia pato la Mtanzania," amesema.

Matindi amesema ili kupanua fursa zilizopo katika soko la ndani lazima kuwe na ndege, sambamba na kutoa huduma za uhakika, hivyo ununuzi wa ndege unamaliza changamoto ya usafiri.

Maoni ya wadau

Akizungumzia hasara ya ATCL, Mhadhiri wa Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo amesema shirika hilo lilikufa.

Amesema lilipofufuliwa lilikuwa na madeni ambayo bado limeendelea kuyarithi.

“Mashirika mengi ya nchi huwa hayapo kwa ajili ya faida ndiyo maana nchi zingine ziliacha kuwa na mashirika ya ndege ya Taifa. Shirika la ndege la Taifa linakuwepo kama chachu ya kuendesha uchumi,” amesema.

Profesa Kinyondo amesema uwepo wa shirika la ndege ni kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanafikika, hivyo hata linapopata hasara lakini linasaidia maeneo ya nchi kufikika, yakiwamo ya utalii, faida itakayopatikana itakuwa imechochewa na shirika la ndege.

“Tunapoangalia shirika la ndege hatuangalii faida na hasara kama yalivyo mashirika mengine, tunaangalia uwepo wake unafanya chachu kwenye sekta zingine? kama linafanya hivyo, shirika la ndege lipo sawa hata kama linapata hasara,” amesema.


Nini kifanyike

Kuhusu hasara katika mashirika mengine, Profesa Kinyondo amesema kinachotokea ni kutokuwa washindani na Serikali kujaribu kufanya mambo isiyoyaweza.

Amesema Serikali iliipa fedha TTCL na kuwalazimisha watumishi wa umma kutumia mtandao huo, lakini bado hali iliendelea kuwa mbaya.

Profesa Kinyondo amesema Serikali inapokuwa na shirika linaloshindwa kushindana na mengine lazima ichague maeneo machache ambayo sekta binafsi haiendi.

“Serikali yoyote iliyosahihi inajua jukumu lake ni kutoa huduma za jamii ambazo sekta binafsi haiwezi kutoa, kama inatoa kwa gharama kubwa, Serikali itatoa kwa gharama nafuu. Usiende kutoa huduma kwenye maeneo ambayo huna uwezo kushindana,” amesema Profesa Kinyondo.

Amesema Serikali haiwezi kuwa na shirika la simu, huku akishauri iingie ubia na mashirika binafsi na kuchukua hisa.

Profesa Kinyondo ameshauri TTCL liache kazi zote lishughulike kusambaza huduma zinazotokana na mkongo wa Taifa.

Akizungumzia TanOil, amehoji Serikali ililianzisha shirika hilo kwa kazi gani wakati ina hisa na Kampuni ya Puma inayouza mafuta.

Kwa upande wa TRC amesema halina sababu ya kupata hasara kwa kuwa lipo tangu wakati wa ukoloni na hakuna mshindani kwenye eneo hilo.

Profesa Kinyondo amehoji iwapo wanaopewa mashirika ya umma kuyaendesha kama wana uwezo wa kufanya kazi tarajiwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie amesema Serikali ikerwe na hasara inayopatikana kwenye mashirika hayo.

“Serikali ikikereka lazima itafute sababu ya mashirika kupata hasara na kutafuta suluhisho, ikiona hasara ni kawaida hakuna hatua itakayochukuliwa,” amesema.

Dk Loisulie ametaja jambo la lingine ni watumishi wa taasisi hizo kutafakari kama ni raha kila wakati kutajwa kupata hasara.

Amesema uongozi wa bodi na utawala usimame na kujitafakari kwa nini wanapata hasara.

Dk Loisulie amesema kama zipo changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi zifanyiwe na mabadiliko yaanze kuonekana.

“Wakati mwingine huenda hakuna tathimini ya kina inayofanyika kisayansi kuangalia ili mashirika hayo yafanye vizuri ni nini kinahitajika. Inawezekana tunabeba mizigo mingine ambayo haibebeki kwenye taasisi za Serikali,” amesema Dk Loisulie.

Amesema serikalini upo mtindo wa watu kufanya kazi ilimradi bila kuwa na malengo halisia yanayotekelezeka.