Serikali kutangaza viwango vipya vya vifuta jasho
Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki akizungumza wakati wa ufunguzi wa tamasha la utalii Wilaya ya Same lililopewa jina la 'Same utalii festival' ambalo limefanyika katika viwanja vya stendi ya mabasi wilayani humo. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amesema tayari zimetolewa zaidi ya Sh7.1 bilioni kwa ajili ya vifuta jasho hivyo.
Same. Wakati Serikali ikijiandaa kutangaza viwango vipya vya vifuta jasho kwa wananchi walioathiriwa na maafa ya wanyamapori nchini, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amesema Serikali imeshatoa Sh7.1 bilioni kwa ajili hiyo.
Amesema tayari wameshawasilisha Wizara ya Fedha mapendekezo ya viwango vipya vya fidia, kama vitaweza kulipika, watavitangaza.
Hata hivyo, amesema kupitia sheria iliyotolewa na Serikali kwa mujibu wa kanuni za kifuta jasho na machozi ya mwaka 2011, inasema mtu aliyeuawa na mnyamapori anapaswa kulipwa fidia ya Sh1 milioni na aliyejeruhiwa atalipwa Sh500,000.
Waziri Kairuki amesema hayo leo Jumamosi, Februari 24, 2024 wakati akifungua tamasha la utalii linalofanyika katika Viwanja vya Stendi ya mabasi wilayani Same. Maonyesho hayo yanakwenda sambamba na maonyesha mbalimbali ya utalii ya ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro.
"Kama Serikali, tunaangalia kiwango kipi kitahimili kutokana na changamoto tuliyonayo, kwa hiyo tumeshawasilisha Wizara ya Fedha mapendekezo yetu na sasa wanayachakata na muda si mrefu tutawatangazia kiwango hicho,” amesema Kairuki.
Hata hivyo, Waziri Kairuki alipoulizwa na mmoja wa wananchi, Serikali ina mpango gani na wanyama aina ya tembo wanaoendelea kuingia na kuvamia makazi ya wananchi na kuwajeruhi na kuwaua, amesema changamoto hiyo ameichukua kwa uzito wake na Serikali imeweka mpango wa kukabiliana na hali hiyo.
“Tunaomba kufahamu serikali inatusaidiaje katika hili, maana tunaishi kwa wasiwasi kutokana na tembo kuwa wengi kwenye maeneo yetu," ameuliza mwananchi.
Hata hivyo, Waziri Kairuki amewahakikishia wananchi hao kuwa malalamiko yao ameyachukua kwa uzito na anakwenda kuyafanyia kazi.
“Niwaombe na niwape pole ndugu zangu wa Same, niwahakikishie tumelipokea kwa uzito mkubwa, tumeshaanza kujenga baadhi ya mabwawa kwenye hifadhi ya Mkomazi na tutaendelea kufanya hivyo katika maeneo mengine, ili wanyama hawa wasitoke nje ya hifadhi kufuata maji kwa sababu wakitoka nje kufuata maji watakutana na wananchi wetu na mazao ya wakulima.
"Kama Serikali hatufurahii kuona tembo hao wanakuja kumjeruhi mtu au kupoteza maisha ya wananchi wetu, tunachokifanya sasa chini ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan tunaangalia kiini au chanzo kinachofanya tembo watokea hifadhini na kuingia kwenye makazi ya watu ni nini," amesema.
Amesema kwa zaidi ya miaka mitano, zaidi ya Sh5.9 bilioni imetumika kama kifuta jasho na kifuta machozi kwa wale walioathiriwa na tembo kwa kujeruhiwa na kupoteza maisha.
"Najua Serikali haiwezi hata kidogo kufidia uhai wa mtu hata tukupe shilingi ngapi… tumeendelea kulipa kifuta jasho kwa wale ambao mazao yao yameathirika na tayari tumetoa Sh1.2 bilioni na tunaendelea kufanya hivyo," amesema.
Pia amesema zaidi ya Sh462 milioni kwa sasa zipo katika uhakiki na kadri fedha hizo zitakapopatikana zitalipwa mapema iwezekanavyo kwa wananchi hao.